Na Mariam Mziwanda
Muungano
wa Tanzania na Zanzibar umefananishwa na mgonjwa aliyelazwa kwenye
Chumba cha Wagonjwa Mahututi (ICU), hivyo Watanzania wametakiwa
kuunusuru kupitia Katiba Mpya inayotarajiwa kupatikana kabla ya uchaguzi
mkuu ujao mwaka 2015.
Kauli
hiyo ilitolewa jana jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi wa Utetezi na
Maboresho wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Harold
Sungusia, wakati akifungua mkutano wa siku tatu wa asasi za kiraia.
Alisema
ni muhimu kwa wananchi kupewa fursa ya kujadili Muungano na kuufahamu
kwa kina kuwa unahitajika ili kuepukana na chuki zinazopandikizwa kutoka
kwa wanasiasa wenye uchu wa madaraka.
“Kuna
wanasiasa wachache wanaotumia nafasi zao ndani ya jamii kupotosha
wananchi kuhusu muungano, wanapandikiza chuki kwa ahadi za kisiasa ili
wapate madaraka,” alisema.
Aliongeza
kuwa elimu ya faida za Muungano ikiwafikia vizuri wananchi na kupewa
fursa ya kujadili ipasavyo kwa muda uliopo kabla ya Bunge la katiba
inatosha kuufanya hudumu na kuwa matunda kwa vizazi vijavyo.
Alisema
Muungano uliopo unategemea kufa au kupona kutokana na maamuzi ya nchi
kupitia katiba mpya kwani umegubikwa na kero nyingi ambazo kwa muda
mrefu hazijapatiwa tiba.
“Muundo
wa Muungano ni tatizo hususani katika uundaji wa Serikali yenyewe hali
inayosababisha wananchi wa pande zote mbili kulalamika, lakini wakati
uliopo unatosha kupitia Bunge la katiba kunusuru muungano ulipo,”
alisema.
Akileleza
changamoto kubwa ambazo wananchi wanatakiwa kuzipatia majibu kupitia
katiba mpya ili kuwa nyenzo ya uhai wa Muungano huo alisema ni pamoja na
utatuzi wa suala la mapato katika mgawo wa asilimia nne kwa Zanzibar na
uwepo wa uhuru wa kuchagua viongozi.
Kwa
upande wa mjumbe wa AZAKI takriban 36, Baraka Mohamed Shamte, alisema
Watanzania bado wanahitaji Muungano na kwamba jambo la muhimu ni
kujadili matatizo yaliyopo na kuyafanyia kazi ili uendelee kudumu.
“Kuanzishwa
kwa Muungano hakukuwa kwa bahati mbaya historia ya Muungano wananchi
wake ni wamoja, vijana wa leo wakishasoma na kupata shahada wanafikiri
wanafahamu kila kitu, kulikuwa na sababu tosha za kuungana kwa nini
Muungano huo haukuwa na Kenya nchi nyingine ni vyema kuwa wa kweli
katika kuzungumzia Muungano,” alisema.
Kwa
upande wake Ramadhan Suleiman Nzori aliwataka vijana wasomi kutambua
kuwa wanategemewa sana katika kulinda na kuthamini Muungano na
wasichukue vitu vidogo vidogo na kuona ni rahisi kuvunja Muungano
uliopo.
No comments:
Post a Comment