Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu mchimati@gmail.com au namba +255767869133.
Chama cha Walimu Tanzania (CWT)
Hivi karibuni Chama cha Walimu Tanzania (CWT) na Chama cha
Wafanyakazi wa Taasisi za Elimu ya Juu Tanzania (THTU) walitoa taarifa
kupitia vyombo vya habari wakieleza kuwa serikali ina mpango wa
kupunguza mafao ya pensheni ya wanachama wa mifuko ya LAPT na PSPF.
Tamko hilo la serikali lilitolewa jana jijini Dar es Salaam na
Kamishina wa Wizara ya Kazi na Ajira, Saul Kinemela, wakati akizungumza
na waandishi wa habari kuhusiana na tamko lililotolewa na CWT pamoja na
THTU na kueleza kuwa tuhuma hizo siyo za kweli kwani wanapotosha umma.
Alisema kuwa Wizara ya Kazi na Ajira ndiyo yenye dhamana ya sekta
ya hifadhi ya jamii Tanzania na ndiyo maana wameamua kutolea ufafanuzi
suala hilo ili jamii iweze kuelewa kwa kina dhidi ya upotoshaji huo.
"Wizara Kazi na Ajira inachukua nafasi hii kukanusha vikali taarifa
zilizotolewa na CWT na THTU ambazo kwa namna moja au nyingine zinalenga
katika upotoshaji," alisema
"Tunaomba wanachama wa mifuko ya hifadhi ya jamii na umma kwa
ujumla, uelewe wazi kuwa si SSRA wala serikali zimetoa tamko lolote
kuhusiana na upunguzaji wa mafao ya pensheni kwa wanachama wa mifuko ya
PSPF na LAPF," alisema Kinemela
Kinemela alisema kinachoendelea ni majadaliano ya wadau wa sekta ya
hifadhi ya jamii yenye lengo la kuboresha mafao ya wastaafu. Hata
hivyo, majadiliano hayo hakuna maamuzi wala tamko lolote lililotolewa
kuhusiana na upunguzwaji wa mafao ya wanachama.
Hata hivyo, alisema CWT na THTU ni moja kati ya wadau wa sekta ya
hifadhi ya jamii, wanayo haki kikatiba ya kukutana na kujadiliana
masuala mbalimbali yakiwemo mifuko hiyo ya kijamii na siyo vizuri
wakafanya upotoshaji kuhusu jambo hilo muhimu.
Alisema serikali inachukua fursa hiyo kuwatoa hofu wastaafu na
wanachama wote wa mifuko ya hifadhi ya jamii, hususani wale wa PSPF na
LAPF na walimu wote kwa ujumla kuwa maamuzi yoyote kuhusiana na mafao
yao yanafanyika kwa uwazi na kuwahusisha wadau wote.
CHANZO:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment