VYAMA vya siasa nchini
vimetakiwa kuacha kutoa kauli za kuwashughulikia wajumbe wa Bunge Maalum
la Katiba wanaokiuka matakwa ama misimamo ya vyama vyao ili kusaidia
mchakato wa katiba.
Hayo yalielezwa jana
mjini hapa na Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba Tanzania (JUKATA) Deus
Kibamba, wakati akizungumza na waandishi wa habari katika Mkutano wa
wanachama wa Jukwaa la Katiba nchi nzima uliolenga kuwaelimisha juu ya
namna ya kujadili rasimu ya katiba.
Kibamba alisema kuwa
kauli zinazotolewa na baadhi ya viongozi wa siasa za kuwashughulikia
wajumbe waliokiuka maazimio ya kundi moja juu ya mchakato wa katiba
ndizo zinazaa mapigano miongoni mwao hivyo kuvuruga mchakato wa katiba.
"Kushughulikiwa kunazaa
kupigana,watu wanapigwa sababu ya rasimu ya katiba na hata anayeonesha
kutaka mchakato wa katiba usitishwe na yule anayesaliti msimamo wa UKAWA
anaambiwa atashughulikiwa...sasa wanatakiwa kuacha kauli hizo na
kushikana mikono ili kwa pamoja wajadili rasimu ya Katiba,' alisema
Kibamba.
Aliongeza kuwa wananchi
pamoja na wajumbe wa Bunge Maalum la katiba wanapaswa kuvumiliana kwa
hoja badala ya kujibizana kwa kuwa rasimu ya katiba ina mambo mengi ya
kujadili ambayo hayahitaji majibizano.
"Sisi tunaongeza nguvu
kwa Bunge Maalum kupitia mijadalatunayofanya na hawa wanachama wakirudi
katika wilaya zao wataelimisha wengine namna ya kujadili rasimu pasipo
kushikana mashati wala kushughulikiana," alisema Kibamba.
Kwa upande
wake,Humphrey Polepole alisema kuwa ni vema Watanzania wakiwemo
wanasiasa wakazuia tofauti za makundi na za vyama vya siasa ili kusaidia
kusudio la Rais Kikwete la kupata Katiba Mpya.
"Tukisema tuzuie
mchakato tutawapa nafasi watu wachache wasiotaka kupata Katiba
Mpya,tushikamane pamoja kupigania mchakato huu kwani kila Mtanzania ana
haki ya kushiriki kujadili katiba," alisema Polepole.
Chanzo:Majira
No comments:
Post a Comment