WANAFUNZI VYUO VIKUU KUMVAA PINDA KESHO
UMOJA
wa Wanafunzi wa Vyuo vya Elimu ya Juu (TAHLISO) umetangaza kufanya
maandamano ya amani kesho hadi Ofisi ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda,
kuishinikiza Serikali kulipa fedha zao kwa ajili ya Mafunzo kwa Vitendo.
Wanafunzi hao
wametangaza uamuzi huo ikiwa ni wiki ya nane sasa tangu walipotakiwa
kuripoti katika maeneo ya mafunzo ya vitendo, lakini kutokana na kukosa
fedha wameshindwa kufanya hivyo.
Akizungumza na
waandishi wa habari Dar es Salaam, Rais wa TAHLISO, Musa Mdede, alisema
awali waliipa siku saba Serikali ili iwe imewalipa fedha wanafunzi
lakini hadi sasa ni wiki ya nane hakuna fedha zilizopelekwa vyuoni.
Alisema mafunzo kwa
vitendo ni muhimu kwani hiyo ni sehemu ya masomo yao na ikiwa hilo
halitafanyika basi ni lazima mwanafunzi atarudia mwaka kutokana na
kukosekana kwa alama ambazo lazima ziwepo ili kukamilisha masomo yake.
"Tumefuatilia sana hadi
sasa, lakini hakuna kitu chochote kilichofanyika wanafunzi kutoka vyuo
saba havijapewa fedha hizo, kitu ambacho kinaweza kufanya wanafunzi
wengi kurudia mwaka," alisema na kuongeza;
"Baada ya kufuatilia
kwa muda mrefu na kutoa siku saba ili Serikali ilipe fedha hizo ambazo
ni sh. bilioni 1 hakuna kilichofanyika."
Mdede alisema kutokana
na hali hiyo wanafunzi kwa sasa wameanza kuwa na wasiwasi kama watapewa
fedha zao za kujikimu za mwezi Oktoba.
Alibainisha kuwa vyuo
ambavyo hadi sasa havijapata fedha hizo ni Chuo cha Usimamizi wa Fedha
(IFM),Theophilo Kisanji cha jijini Mbeya,Chuo cha Mt. Augustino cha
Mwanza,Tumaini Makumira cha Arusha,Chuo cha Mt. Augustine Tawi la
Tabora,Chuo cha Kumbukumbu ya Stephano cha mkoani Kilimanjaro,Chuo cha
Jordan cha mkoani Morogoro na Chuo cha Bugando cha mkoani Mwanza.
Akizungumzia hali hiyo,
Waziri wa Serikali ya Wanafunzi wa Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM),
Waziri Juma, alisema wamefuatilia kwa kipindi kirefu lakini uongozi wa
Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HEALSB) ulisema hauna fedha.
"Tulikwenda Bodi ya
Mikopo kupeleka kilio chetu na bahati nzuri tulikutana na Mkurugenzi wa
Bodi hiyo na tulimwambia suala hilo, lakini alisema kama yeye angekuwa
na fedha basi angewapa... lakini hakuna fedha; na Hazina haijapeleka
fedha kwenye Bodi; hivyo fanyeni mnachoweza kufanya," alisema akimnukuu
Mkurugenzi wa HEALSB
Chanzo:Majira
No comments:
Post a Comment