Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu mchimati@gmail.com au namba +255767869133
VYAMA
vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), vimetangaza
kuunganisha nguvu kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 kwa kuweka
mikakati ya pamoja itakayosaidia kuing'oa CCM madarakani.
Mkakati huo umetangazwa
Dar es Salaam jana na Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia, wakati
akifungua semina ya kuwajengea uwezo wanachama wa chama hicho kuhusiana
na namna ya kukabiliana na changamoto wakati wa uchaguzi wa Serikali za
Mitaa.
Mbatia alisema vyama
vinavyounda UKAWA vya NCCR-Mageuzi, CHADEMA na CUF vitaungana kwa pamoja
ili kuunganisha nguvu ya umma itakayosaidia kuing'oa CCM madarakani
katika uchaguzi wa 2015.
"Wananchi wamekuwa
wakilia kwa muda mrefu kutaka vyama kuungana na sisi tumelisikia hilo
ndilo la maana kwa sasa; tumeanzisha mazungumzo ya vyama vinavyounda
UKAWA kuungana na kuwa kitu kimoja ili kuleta pamoja nguvu ya umma kwa
ajili ya mwaka 2015," alisema Mbatia.
Alisema ili mtu aje
kuwa Rais lazima ajipange na kuonesha kile alichonacho kwa jamii na
baada ya hapo anaweza kutangaza nia yake, lakini si kukurupuka na ndio
maana wao wanajipanga ili kuona nguvu ya wananchi inaletwa pamoja
kupitia Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.
"Uchaguzi si mtu kuamka
usingizini na kuamua kutangaza nia, bali unatakiwa ujipange ili kuona
namna gani utaweza kuleta sera zako kwa jamii,mtu umeshindwa katika
ngazi ya familia na Chama; itakuwaje uweze kuongoza Taifa kubwa kama
Tanzania?" alihoji Mbatia.
Akizungumzia mchakato
wa Katiba, Mbatia alisema wao kama UKAWA hawasimamii mawazo ya Chama
kimoja; bali ni maoni ya wananchi kwa ujumla.
Alisema kitendo cha wao
kukataa kushiriki vikao vya Bunge Maalum la Katiba ni kuonesha jinsi
gani hata wakiamua kuungana lazima madaraka wayapate kwani wanasimamia
kile wanachotaka wananchi.
Alisema mapendekezo
yaliyopo kwenye rasimu ya Katiba ni ya muundo wa Serikali tatu. "Sasa
iweje leo watu wapindishe ukweli,Katiba si ya mtu mmoja bali ni mawazo
ya watu na sisi tutaendelea kusimamia msimamao wetu kwani hayo ndiyo
maoni ya wanachi waliyotaka wao," alisema Mbatia.
"Leo inashangaza watu
kudai kuna Muungano wakati Januari 12, mwaka huu wakati wa sherehe za
Mapinduzi, Rais Jakaya Kikwete alipoenda Zanzibar aliingia Uwanja wa
Amani kama si Rais, huku Rais wa Zanzibar akiingia kwa misafara na kwa
kushangiliwa na umati wa watu," alisema Mbatia na kuongeza;
"Jambo hili linaonesha
kuwa Zanzibar ni nchi na kilichopo shirikisho la nchi na ndo maana watu
wana hoji uhalali wa Serikali mbili."
Alisema Watanzania
wasahau kupata Katiba Mpya kwa sasa kwani licha ya Bunge hilo kuendelea
lakini kuna mambo mengi ya kuifanya katiba hiyo isipatikane likiwemo
kutokuwepo kwa Daftari la Kudumu la Wapiga kura.
"Kuendelea kwa Bunge
hilo ni sawa na kufuja fedha za umma, kwani Daftari la Kudumu la
Wapigakura ndilo linatakiwa litumike kwenye kura ya maoni ya kupitisha
katiba hiyo lakini mpaka sasa tume ya Taifa ya uchaguzi bado haijatoa
majibu ya kuaminika juu ya upatikanaji wa daftari hilo," alisema Mbatia
na kuongeza.
"Tuliitwa na Mwenyekiti
wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi tukaambiwa mpaka sasa tume hiyo haina
Daftari la Kudumu la Wapigakura na huu mfumo wa BRV wanaotaka kuutumia
unahitaji umeme wakati huko vijijini umeme wenyewe hakuna... nchi nyingi
zimejaribu mfumo huo zimeshindwa zikiwemo Kenya na Afrika Kusini, sasa
sisi tutauwezaje wakati hao wenzetu walioushindwa wametuzidi kiuchumi na
mpaka sasa bado hatujaona dalili za maandalizi juu ya Daftari hilo?"
alisema.
Alisema inashangaza
kuona hata wajumbe waliokuwa Dodoma wameongezewa siku na Rais kutoka 60
hadi 84 na kumfanya kila mjumbe kupata milioni 24.
Aliendelea kusema kuwa kinachotakiwa kwa sasa ni Bunge hilo kusitishwa hadi mwakani baada ya Uchaguzi Mkuu na wala si kuvunjwa.
Alisema Bunge la
Jamhuri likae na kufanya baadhi ya mabadiliko kwenye Katiba iliyopo ili
kuweza kuwa na uchaguzi ulio huru na haki.
"Bunge la Jamhuri likae
na libadilishe baadhi ya vipengele kwenye katiba ya sasa," alisema na
kuongeza kwamba, miongoni mwa vipengele hivyo; ni ili rais aweze
kutangazwa mshindi na ni lazima afikishe asilimia 50 ya kura zote.
No comments:
Post a Comment