STATOIL YATAJA VIJANA WATANO WALIOINGIA TANO BORA YA SHINDANO LA MASHUJAA WA KESHO
Kampuni
ya Statoil Tanzania ina furaha kutangaza majina ya vijana watano
waliongia fainali za shindano la biashara la mashujaa wa kesho ambalo
lina dhumuni la kuhamasisha ujasiriamali kwa mikoa ya kusini mwa
Tanzania yaani Mtwara na Lindi.
Akitoa taarifa hii
meneja wa shindano hilo kutoka Statoil, Erick Mchome amewataja washindi
hao kuwa ni Razaki Kaondo, Edward Timamu and Sifael Nkiliye
(walioshiriki kama timu moja), Saleh Rashid Kisunga, Azizi Doa, na Yunus
Mtopa.
Shindano la Mashujaa wa Kesho lilihusisha
vijana wenye umri kati ya miaka 18 na 25 kutoka mikoa ya Mtwara na Lindi
kuwasilisha mawazo yao ya biashara ambayo baadae yalibadilishwa na
kuwekwa kwenye andiko la biashara.
Mwaka huu
shindano hili lilivutia vijana zaidi ya 400 ambao waliwasilisha mawazo
ya biashara zao zinazolenga sekta mbalimbali za uchumi kama kilimo,
ufugaji, mawasiliano, na biashara nyingine ndogondogo. Vijana
waliruhusiwa kushiriki mmoja mmoja au hata kuunda vikundi vya watu
wawili mpaka watatu.
Mwazo
bora yaliyopatikana kati ya 400 yalikuwa 60 na wamiliki wa mawazo hayo
ambao ni zaidi ya vijana 80 kutoka Lindi na Mtwara walipewa mafunzo
maalum ya kuandaa andiko la biashara ambapo yalishindanishwa tena na
kupatikana vijana kumi bora waliopelekwa mbele ya majaji ambao wiki hii
walichagua maandiko matano bora kati ya kumi waliyopokea.
“Vijana
hawa watano watawasili jijini Dar es Salaam wiki ijayo ili kuja kutetea
maandiko yao ya biashara mbele ya jopo la majaji ambao mwisho wake
wataamua nani anafaa kuwa mshindi wa shindano letu,” alisema Bwana
Mchome.
Mshindi wa shindano hili atatangazwa siku
ya Ijumaa tarehe 15 Aprili jijini Dar es Salaam katika hafla maalum
iliyoandaliwa na Statoil ili kumpongeza mshindi huyo na wenzake wanne
ambao wamefanikiwa kuingia fainali. Mshindi huyo atajinyakulia kitita
cha dola za kimarekani 5,000 wakati washindi wanne waliobakia watapata
dola 1,500 kila mmoja. Washindi wengine watano waliofanikiwa kuingia
kumi bora watapata dola 1,000.
“Statoil inaamini
katika kuwawezesha vijana wenye vipaji katika maeneo yote ambayo
tunafanya shughuli zetu na kwa kufanya hivi tunachochea maendeleo katika
maeneo hayo ambayo nasi ni sehemu yake kwani tunafanya shughuli zetu za
uendelezaji wa nishati kama gesi na mafuta.,” amesema Meneja Mkazi wa
Statoil Tanzania, Øystein Michelsen.
No comments:
Post a Comment