TAN

TAN

Bayport

Bayport

Kikoa

Kikoa

Myway entertainment

Myway entertainment

FORE PLAN CLINIC

FORE PLAN CLINIC

MPINGA CUP 2016

MPINGA CUP 2016

Mashujaa Fm 89.3, Lindi

Saturday, March 22, 2014

KAULI YA WAPINZANI KUHUSU HOTUBA YA JK BUNGE LA KATIBA


Wenyeviti wa vyama vya Upinzani vya Chadema, Chama cha Wananchi (CUF) na Chama cha NCCR-Mageuzi, jana usiku walikutana ili kutoa kauli ya pamoja, kutokana na hotuba ya ufunguzi wa Bunge kwa maelezo kuwa tayari Rais amevuruga mchakato mzima wa kupata Katiba Mpya.
Wakati viongozi hao wakikutana, Mwenyekiti wa Chama cha DP Mchungaji, Christopher Mtikila alisema, Rais ameingilia mchakato na kutoa maelezo jinsi ya  kuandika Katiba.
Wakizungumza na gazeti hili jana mara baada ya hotuba hiyo, Freeman Mbowe, James Mbatia na Profesa Ibrahim Lipumba, walisema wameipokea kwa masikitiko makubwa hotuba hiyo.
“Tunakwenda kujadili hotuba ya Rais na tutatoa msimamo wetu,” alisema Mbowe.
Awali Katibu wa muda wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Julius Mtatiro alisema Rais Jakaya Kikwete amevuruga mchakato wa Katiba, kwani walitarajia angetumia mamlaka yake kama Rais kuwaunganisha.
“Rais tulitarajia angeongea kama mkuu wa nchi, lakini amezungumza kama Mwenyekiti wa CCM na kutoa msimamo juu ya muundo wa Muungano jambo ambalo hatukulitegemea,” alisema Mtatiro.
Alisema kwa Rais kutoa msimamo ni sawa na mwongozo jambo ambalo limevuruga mchakato mzima.
Hofu ya kuvunjika Bunge
Wakizungumza nje ya Bunge, baadhi ya wajumbe wameeleza kuwa hotuba ya Rais Kikwete kama ikitekelezwa uwezekano wa kupata Katiba Mpya utakuwa mgumu.
Mjumbe Luhaga Mpina alisema kwa jinsi rasimu ilivyoandikiwa na kama muundo wa serikali mbili ukipita basi rasimu ya Katiba itabidi iandikwe upya.
“Rasimu yote imetengenezwa kwa mfumo wa serikali tatu sasa hapa kuna hatari ya Bunge kukwama ,” alisema.
Mtatiro kwa upande wake alisema sasa kuna hofu ya kushindwa kupatikana Katiba Mpya kwani Rais amewachanganya wajumbe na kama watapitisha maoni yake itabidi rasimu kuandikwa upya.
Mjumbe Mustapha Akoonay, alisema upatikanaji wa katiba upo shakani kwani sasa upinzani utakuwa mkubwa juu ya muundo wa muungano.
“Kwa sasa nadhani itabidi turudi upya kwa wananchi kupata kura ya maoni juu ya muundo wa muungano,” alisema.
Lucy Owenya alisema  Rais amegeuza mkutano wa Bunge kuwa ni mkutano wa Chama Cha Mapinduzi, kwani ameshindwa kabisa kutoa mwelekeo wa nchi na badala yake ametoa msimamo wa CCM.
“Kutokana na hili, naamini kabisa Bunge halitakuwapo na ni bora iwe hivyo kwa kuwa amejibu hotuba ya Warioba na kwa maana hiyo amepingana na mawazo ya wananchi.”
Godbles Lema alisema kuwa Rais hakuja kuhutubia taifa bali alikuja kufanya semina na kujibu hotuba ya Warioba.
Mjumbe huyo ambaye ni mbunge wa Arusha Mjini alionyesha shaka kuwa baada ya muda wa wiki tatu hakutakuwa na Bunge la Katiba kwa kuwa wako baadhi ya watu ambao hawatakubali kilichofanywa na Rais Kikwete.
“Waliochukua fedha ni vyema wakaenda kumalizia nyumba zao kwa kuwa kiongozi wetu amefanikiwa kwa kiasi kikubwa kuwafurahisha wanaCCM lakini kwa Watanzania hatutakubali,” alisema Lema.
John Cheyo alisema, “Mimi ninachokiona ni maridhiano tu, suala la kufumua rasimu halinipi shida kwa kuwa vitu vyote vinavyoletwa bungeni huwa ni mali ya Bunge na hivyo tutafanya tunavyoona sisi inafaa.”
Mchungaji Peter Msigwa, alisema kuwa kosa kubwa ambalo lilifanywa na upinzani ni kukubali na kuruhusu Jaji Warioba atangulie kuwasilisha rasimu yake akasema hilo ndilo lililowagharimu.
Alitaka Bunge livunjwe mara moja ili warudi kwa wananchi wakaamue na kuwahukumu kutokana na kile ambacho walikifanya katika Bunge ambalo kwa maoni yake wamekula fedha za walipa kodi bure.
Naye Waziri Mkuu Mstaafu, Edward Lowassa aliipongeza hutuba ya Rais Jakaya Kikwete ya uzinduzi wa Bunge la Katiba.
Lowassa ambaye pia ni Mjumbe wa Bunge la Katiba, alisema kwa kifupi hotuba ya Rais Kikwete ni nzuri. Lowassa alitoa kauli hiyo, wakati akitoka nje ya Bunge, muda mfupi baada ya Rais Jakaya Kikwete kumaliza hotuba ya uzinduzi wa Bunge hilo.

No comments:

Post a Comment