Katika maisha ya kila siku, mwananchi anapaswa kutambua wajibu wake katika jamii ikiwa ni pamoja na kutii Sheria bila shuruti.
Katika maisha ya sasa nchini
kumekuwa na vitendo vya ukiukwaji wa Sheria katika jamii na jamii
imekuwa ikihusika katika matendo makubwa ya kijinai ambayo ni kinyume na
sheria.
Hali hii imekuwa ikitokana na aidha jamii kutojua sheria, na muda mwingine ni kupuuzia tu maagizo na sheria mbalimbali.
Siku za hivi karibuni kumekuwepo
na ukatili mkubwa ukitendeka katika jamii kwa kutokea kwa mauaji ya
watu wenye ulemavu wa ngozi ambapo wasiojua nini maana ya utu kwa
makusudi wanakatiza uhai wa maisha ya binadamu wenzao na wengine
kuwakata baadhi ya viungo vyao kwa tamaa ya kujipatia fedha pamoja na
imani za kishirikina.
Jamii sio tu inaelewa kuwa
kumdhuru mtu ni kosa la jinai bali pia jamii inatambua kuwa kuua pia ni
kosa kubwa la jinai ambapo katika Sheria ya Kanuni ya adhabu Sura ya 16
kifungu cha 197 kimeeleza jinsi ambavyo kosa la kuua kwa kukusudia
linamgharimu mtu adhabu ya kifo, lakini licha kuwepo kwa sheria hiyo,
bado jamii inajihusisha na makosa ya kuua kila kukicha.
Katika mikoa ya Kanda ya Ziwa
Victoria, suala la mauaji ya watu wenye Ualbino limekuwa ni tatizo kubwa
kwani mauaji haya yanafanyika katika mazingira tu ya watu kuwa na imani
potofu za kuukwaa utajiri wa haraka haraka.
Wakili wa kujitegemea Bwana
Edwin Webiro anaeleza kuwa watu wengi wanafahamu kuwa kuua ni kosa kubwa
lenye adhabu ya kifo ama kifungo cha maisha, bado watu hao hawajali juu
ya uwepo wa Sheria ya kunyonga kwasababu wamekuwa wakiiona haitekelezwi
ipasavyo, jambo linalowafanya wao waone ni haki kwao kufanya unyama
wowote kwa watu wasio na hatia (watu wenye ulemavu).
Katika hali nyingine jamii pia
imekuwa ikikiuka Sheria na kusababisha madhara makubwa pale ambapo ajari
nyingi zimekuwa zikitokea mfululizo hivi karibuni na kusababisha vifo
na kuacha ulemavu wa kudumu wa jamii.
Ajali hizi zimekuwa
zikisababishwa na uzembe wa baadhi ya madereva wa mabasi pamoja na
magari madogo kwani kumekuwa na ukiukwaji wa Sheria za barabarani ambapo
kwa makusudi madereva hao wamekuwa wakikiuka sheria mbalimbali na
kufanya mambo yanayosabisha ajari.
Sheria ya Usalama barabarani
Sura ya 168 Kifungu cha 44 Inazuia mtu kuendesha chombo cha moto akiwa
ametumia kilevi, lakini Sheria hii inajulikana vema kwa madereva lakini
kwa makusudi hawaijali wala kuizingatia na badala yake wamekuwa
wakitumia kilevi kabla ama wakati wakiwa wanaendesha vyombo vya moto.
Swali la kujiuliza ni kwamba, kwanini madereva wamekuwa wakitumia kilevi wakiwa wanaendesha magari?
Josephat Munishi ni Dereva wa
daladala moja linalofanya safari zake Jijini Dar es Salaam anaeleza kuwa
kutumia kilevi wakati wa kuendesha gari ni kosa kisheria.
“Muda mwingine kilevi kinakupa
nguvu na kujihisi kutochoka na unapata hamasa ya kuendesha gari, kama
unavyojua kazi yetu ni ngumu kutwa nzima unasumbuana na abiria, sasa
bila kinywaji kidogo hauwezi pata nguvu ya kufanya kazi’’, alisema
Munishi.
Jamii kwa mara nyingeine imekuwa
ikikiuka Sheria na kujikuta katika maovu makubwa ambapo baadhi ya
wasichana wamekuwa wakijihusisha na utoaji mimba (Abortion)kinyume na Sheria.
Kwa hali ilivyo sasa wasichana
wadogo hasa wanafunzi na hata watu wazima wamekuwa wakijihusisha sana na
utoaji mimba kinyume na sheria huku wengi wao wamekuwa ni wale ambao
wamepata mimba hizo katika mazingira ambayo hawakutegema.
Watoto wengi wa kike wamekuwa
wakijihusisha na mapenzi wakati bado wakiwa shule, na pindi
wanapojigundua kuwa wana ujauzito njia pekee ambayo wanahisi ni bora
kuepukana na matatizo hayo wamekuwa wakitoa mimba, kitu ambacho ni
kinyume na Sheria za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Katika kifungu cha 219 Cha
Sheria ya Kanuni ya adhabu Sura ya 16, kinaeleza wazi kuwa kitendo cha
kuharibu ujauzito ambao unapelekea kukatisha maisha ya mtoto ambaye
angezaliwa, ni kosa la jinai lakini sababu kubwa ambayo wamekuwa
wakiitoa wanawake wengi ni kuwa mimba hizo zinakuwa ni zile ambazo
hazikupangwa kutokea (unplanned pregnancy).
Jamii inapaswa kuzingatia Sheria
mbalimbali na iepuke kutoa sababu na visingizio za kutojua sheria hizo,
kwani ni vema kutii sheria bila shuruti kama vyombo vyetu vya Usalama
vinavyotutaka.
No comments:
Post a Comment