Mhe. Said Ali Mbarouk akiwa na
mwenyeji wake Waziri wa Habari nchini Oman Sheikh Dk. abdulla wakati
alipofanya mazungumzo katika ofisi yake tarehe 29 Septemba 2014 akiwa
katika ziara rasmi ya siku nne kutembelea sekta mbali mbali za Utalii,
Utamaduni na Michezo.
MUSCAT, OMAN 30/09/2014
Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo Mh. Said Ali
Mbarouk ameuelezea ushirikiano baina ya Oman na Zanzibar kuwa daima
utakuwepo na utaendelea kukua kutokana na kutanuka kwa maeneo mapya ya
ushirikiano katika Nyanja mbali mbali za maendeleo.
Amesema ni jambo la faraja kuona
kuwa hivi sasa Zanzibar na Oman zinatambua umuhimu wa kutanua maeneo
hayo ya ushirikiano katika sekta za uchumi, utalii na michezo kwa lengo
la kuwanufaisha watu wa pande zote mbili.
Mhe. Saidi Ali Mbarouk ameyaeleza
hayo katika nyakati tofauti wakati alipokuwa na mazungumzo na Mawaziri
wa sekta za Habari, Michezo, Utamaduni na Utalii mjini Muscat Oman leo,
akiwa katika ziara yake ya siku nne ya kukutana na viongozi mbali mbali
wa nchi hiyo kwa lengo la kukuza ushirikiano baina ya nchi hizo mbili.
Mapema akizungumza na Waziri wa
Habari wa Oman, Sheikh Dk. Abdulla Monaim Bin Mansoor Al Husani, alitoa
shukrani zake kwa Serikali ya Oman kwa misaada yake kwa Zanzibar na
kusifu nidhamu ya vyombo vya habari vya nchi hiyo katika kuwaunganisha
watu na kuwawezesha kujenga uchumi imara.
Alisema hatua hii ya mfano wa
kuigwa inatokana na usimamizi madhubuti kwa vyombo vya habari na
kujali kuwajibika kwa jamii kwa vile vinatoa nafasi ya kuwapatia taarifa
za kutosha juu ya harakati za kujiendeleza na kujenga ustawi na
maendeleo yao.
Ameshauri haja ya kuwepo na
utaratibu wa kubadilishana wataalamu na vipindi ili kila nchi iweze
kujifunza kutoka upande mwengine kwa kutambua maendeleo yanayofikiwa na
kila upande na hivyo kutoa fursa za kuwawezesha vijana na vyombo vya
habari kuongeza kasi ya utekelezaji wa majukumu yao kwa pamoja hasa kwa
vile ni tegemeo kubwa la taifa katika kujenga uchumi.
Katika ziara yake hiyo ya siku
nne, Mheshimiwa Saidi Ali Mbarouk pia alipata fursa ya kubadilishana
mawazo na Naibu Waziri wa Utamaduni na Mambo ya Kale, Sheikh Hamad Hilal
Al Maamari na Waziri wa Michezo, Sheikh Shallal Saad Moh’d Al Saad na
kutuwama zaidi katika masuala ya kubadilishana wataalamu wa michezo na
kuyahuisha majengo ya kihistoria yenye mnasaba na Oman.
Wakati huo huo, Mhe. Said Ali
Mbarouk ameitaka Oman kufungua fursa nyengine kwa kuisaidia Zanzibar
katika kuanzisha Hoteli za kitalii za Halal utaratibu ambao Oman tayari
imeuanzisha na kupata mafanikio yake.
Amefahamisha kuwa utaratibu wa
hoteli kama hizo za Halal ni muafaka katika visiwa vya Zanzibar kwa vile
zitaongeza soko la idadi ya watalii wanaohitaji kupumzika katika maeneo
yenye utulivu wa maadili ya kidini na kiutamaduni.
Katika ziara yake hiyo Waziri huyo
wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo alipata fursa ya kushiriki
katika karamu rasmi iliyoandaliwa kwa ajili yake na ujumbe wa watu
watatu aliyofuatana na Mwenyeji wake Waziri wa Habari wa Oman Sheikh Dk.
Abdulla Monaim iliyofanyika katika jumba la serikali la Opera mjini
Muscat.
IMETOLEWA NA IDARA YA HABARI HABARI AMELEZO ZANZIBAR
No comments:
Post a Comment