Naibu
Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Michael John akitoa
tamko kuhusu Siku ya Soko la Afya iliyoandaliwa na Wizara hiyo kwa
kushirikiana na Shirika la GIZ , itakayofanyika Oktoba 2 katika ukumbi
wa Diammond Jubelee jijini Dar es salaam.
Naibu
Meneja wa Miradi ya Afya wa GIZ Bw. Christian Ptleiderer akizungumza na
waandishi wa habari kutoa wito kwa mashirika mengine yanayotoa huduma
za afya nchini kuendelea kusaidia na kusambaza huduma zao katika maeneo
yenye changamoto ya miundombinu na uhaba wa watumishi wa afya.Kulia ni
Mtaalam na Mawasiliano wa shirika la GIZ nchini Bi. Vida Mwasalla.
Na. Aron Msigwa – MAELEZO.
30/9/2014.Dar es salaa.
Wizara ya Afya na Ustawi wa
Jamii imesema kuwa itaendelea kushirikiana na Shirika la Ujerumani la
GIZ katika uanzishaji na uendelezaji wa programu mbalimbali za utoaji wa
huduma za afya zinazolenga kupunguza vifo vya watoto walio chini ya
umri wa miaka 5.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya
Afya na Ustawi wa Jamii, Michael John ameyasema hayo leo jijini Dar es
salaam wakati akitoa tamko kuhusu Siku ya Soko la Afya nchini
iliyoandaliwa na Wizara hiyo kwa kushirikiana na Shirika la Ujerumani la
GIZ itakayofanyika Oktoba 2, jijini Dar es salaam.
Amesema Tanzania na GIZ zimekuwa
zikishirikiana katika uboreshaji wa miradi mbalimbali ya afya kwa
kusogeza huduma za afya karibu na wananchi kuanzia ngazi ya taifa, mikoa
na Halimashauri za wilaya.
Ameeleza kuwa mikoa ya Lindi,
Mbeya, Mtwara na Tanga imeendelea kunufaika na miradi mbalimbali ya
ushirikiano chini ya shirika hilo inayolenga kuimarisha miundombinu ya
kutolea huduma za afya katika maeneo hayo, uimarishaji wa mifuko ya Afya
ya Jamii na ushiriki wa moja kwa moja kusaidia upatikanaji na
uendelezaji wa wataalam wa kutoa huduma za afya maeneo ya vijijini.
Ameongeza kuwa GIZ imekuwa
ikishirikiana na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii katika kuhakikisha
kuwa jamii inamudu huduma bora za afya kupitia Mifuko ya Hifadhi ya Afya
ya Jamii iliyopo katika maeneo yao.
Aidha, amebainisha kuwa
maonyesho ya siku ya Soko la Afya yatakayowahusisha wadau mbalimbali na
mashirika yanayotoa huduma za afya nchini yanalenga kuwakutanisha wadau
hao ili waweze kujadili changamoto za utoaji wa huduma za afya nchni,
kujifunza mafanikio yaliyopatikana katika baadhi ya maeneo na kuweka
mikakati ya kuyafikia maeneo mengi zaidi.
Kwa upande wake Mtaalam na
Mawasiliano wa shirika la GIZ nchini Bi. Vida Mwasalla ameeleza kuwa
maonesho ya mwaka huu yazilenga Wizara, Taasisi , Washirika wa
Maendeleo, Makampuni, Mashirika binafsi na Wakala zinazojihusisha na
utoaji na uendelezaji wa sekta ya afya nchini.
Amesema katika maonesho hayo GIZ
kwa kushirikiana na Wizara ya Afya itaonyesha mikakati mbalimbali ya
kuwaokoa watoto wadogo wenye matatizo ya afya, namna walivyofanikiwa
kuwapata watumishi wa afya katika maeneo ya Lindi na Mtwara, maeneo
ambayo hapo awali walikuwa hawakai katika vituo vyao.
Ameongeza kuwa mbali na Siku ya
Soko la Afya kuhusisha huduma za utoaji wa elimu, vipimo, machapisho
mbalimbali inalenga kuwaweka pamoja wadau hao ili waweze kubadilishana
uzoefu na kuweka mikakati ya kuchangia maendeleo ya sekta ya afya hapa
nchini.
Naye Naibu Meneja wa Miradi ya
Afya wa GIZ Bw. Christian Ptleiderer ametoa wito kwa mashirika mengine
yanayotoa huduma za afya nchini kuendelea kusaidia na kusambaza huduma
zao katika maeneo ambayo bado yanakumbwa na changamoto mbalimbali za
miundombinu na uhaba wa watumishi wa afya.
Amesema wao kama GIZ kwa kuanzia
wameanza na mikoa 4, na wanaendelea kujenga uwezo wa kuyafikia maeneo
mengi zaidi kwa kushirikiana na Serikali ya Ujerumani na Tanzania.
No comments:
Post a Comment