Mtaalamu
wa viwango kutoka mgodi wa Ngaka, Boscow Mabena akionyesha tofali
maalumu (briquette) zilizobuniwa na mgodi huo kwa ajili ya matumizi ya
kupikia majumbani na katika taasisi. Tofali hizo zina uwezo wa kuwaka
kwa zaidi ya saa nne.
………………………………………………………………
Na Mohamed Saif – Mbinga
Mgodi wa Makaa ya Mawe wa Ngaka
uliopo wilayani Mbinga mkoani Ruvuma upo mbioni kuanza kuuza makaa
yanayozalishwa na mgodi huo kwa ajili ya matumizi ya kupikia katika
taasisi na majumbani.
Hayo yalielezwa hivi karibuni na
Mtaalamu wa Viwango katika mgodi huo, Boscow Mabena alipokuwa
akizungumza na ujumbe kutoka Wizara ya Nishati na Madini uliofanya ziara
mgodini hapo kwa lengo la kufanya ukaguzi wa kimazingira.
Mabena alieleza kuwa utafiti wa
kupunguza joto katika Makaa hayo ili kuweza kutumika kwa ajili ya
kupikia umefanywa kwa kushirikiana na kikundi cha kina Mama cha
Mbarawala Women Group kilichopo wilayani humo pamoja na Chuo cha VETA-
Ruvuma.
Aliongeza kuwa utafiti huo
umefanyika kwa kipindi kirefu na tayari umekamilika na hivi sasa
kinachosubiriwa ni kibali kutoka Shirika la Viwango Tanzania (TBS) ili
makaa hayo yaanze kuuzwa.
Mtaalamu huyo alieleza kuwa
wamebuni tofali maalumu (briquette) kutokana na makaa hayo ambazo
zitatumika kwa ajili ya matumizi ya kupikia kwa kutumia majiko maalumu
ambayo yamebuniwa na wataalamu kutoka Chuo cha VETA.
Aidha, alibainisha kuwa tofali
moja la mkaa huo (briquette) lina uwezo wa kuwaka kwa saa zisizopungua
nne na hivyo kumuwezesha mtumiaji kupika vyakula mbalimbali kwa kutumia
tofali kimoja.
Kuhusu suala la bei, Mabena
alifafanua kuwa kila tofali litauzwa kwa kuanzia shilingi mia mbili na
majiko yatatofautiana bei kulingana na mahitaji ya mtumiaji. “Unajua
kuhusu jiko, inategemea mtu anahitaji jiko la namna gani, kuna majiko
makubwa ya taasisi na pia madogo, hivyo mteja atatuambia anahitaji jiko
la namna gani maana tuna uwezo wa kumjengea jiko maalumu
lisilohamishika,” alisema.
Mabena alisema matumizi ya mkaa
huo yanatazamiwa kupunguza uharibifu wa mazingira hususan ukataji hovyo
wa miti kwa ajili ya mkaa na kuni.
Alieleza kuwa, tayari taasisi
mbalimbali zimeonyesha nia ya kutumia majiko hayo. Mtaalamu huyo
alizitaja baadhi ya taasisi kuwa ni Magereza wilayani Songea pamoja na
Chuo cha Ualimu cha Songea. “Tulikuwepo siku ya Maonesho ya Nane Nane
hapo Songea na wananchi wengi walivutiwa na mkaa huu na hii ilitusaidia
tushike nafasi ya kwanza kwa ubunifu,” aliongeza.
No comments:
Post a Comment