MTANDAO wa Wanawake na Katiba,
TGNP pamoja na mashirika mengine yanayotetea haki za binadamu wameahidi
kushirikiana kutoa elimu ya uraia na uhamasishaji juu ya Katiba
inayopendekezwa baada ya kutangazwa kwa muda rasmi wa kuanza kwa zoezi
hilo kwa jamii ili kuelimisha zaidi wananchi juu ya Katiba
nayopendekezwa. Kauli hiyo imetolewa katika Kongamano la Wanaharakati
Kujadili masuala muhimu kwenye mchakato wa Katiba Mpya lililofanyika
jijini Dar es Salaam na kuwashirikisha wanaharakati mbalimbali.
Akifafanua zaidi katika mada yake
aliyoiwasilisha kwenye Kongamano hilo, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa
TGNP, Lilian Liundi alisema endapo Bunge Maalum la Katiba Litapitisha
Rasimu ya Katiba inayopendekezwa kwa kura nyingi za ndiyo kwa Wajumbe wa
Bunge hilo, Rais Jakaya Kikwete atakabidhiwa rasimu hiyo na Kuwa Katiba
Inayopendekezwa.
Alisema baada ya hapo kwa mujibu
wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba utaratibu wa utoaji wa elimu na
uhamasishaji kwa Umma juu ya maudhui yaliyomo kwenye Katiba
inayopendekezwa na Kampeni ya Upigaji wa Kura ya maoni utafanyika zoezi
litakalofanywa na Tume husika na vyama vya siasa, vyama vya kijamii
vinaruhusiwa kushiriki kutoa elimu ya uraia na uhamasishaji juu ya elimu
hiyo.
“…Ratiba kamili ya muda wa kutoa
elimu kwa umma kuhusu maudhui yaliyomo katika Katiba inayopendekezwa
itatolewa kupitia Tanagazo la Gazeti la Serikali (Government Notice).
Kwa madhumuni ya kuelimisha na kuhamasisha wananchi kuhusu kuipigia kura
ya maoni Katiba inayopendekezwa, Tume italazimika, na vyama vya siasa
na vyama vya kijamii vinaweza kutoa elimu ya uraia na uhamasishaji juu
ya Katiba inayopendekezwa kwa muda usiozidi siku thelathini kuanzia siku
ya kuchapishwa katika Gazeti la Serikali,” alisema Bi. Liundi.
Alisisitiza kuwa kipindi hicho ni
muhimu kuwafanya wananchi wote waelewe kilichomo katika Katiba
inayopendekezwa ili waweze kuona kama masuala yao ya muhimu yameingizwa
katika katiba hiyo kabla ya kuipigia kura.
Aidha Mkurugenzi huyo alitoa wito
hasa kwa wanawake na makundi ya pembezoni kutumia kipindi hicho kuisoma
na kuielewa Katiba inayopendekezwa kwani ndiyo sheria mama na itakuwepo
kwa muda mrefu kwa ajili ya jamii yote na hata ya vizazi vijavyo, hivyo
ni muhimu kutambua kuwa katiba hiyo ni ya wananchi wote kwa ujumla na si
ya vyama vya siasa wala kundi fulani katika jamii.
“…TGNP Mtandao wa wanawake na
katiba pamoja na mashirika mengine yanayotetea haki za binadamu
tutaendelea kutumia fursa hiyo kuendelea kuelimisha na kuraghbisha
wananchi kuhusu Katiba inayopendezwa. Hii itasaidia sana wakati wa
kuipigia kura ya maoni juu ya Katiba inayopendekezwa wananchi wawe wana
uelewa wa kutosha kuhusu yaliyomo katika katiba hiyo na hatimaye wapige
kura wakiwa na maamuzi sahihi,” alisema Bi. Liundi.
Akizungumzia zoezi la kufanya
mabadiliko katika katiba ya 1977, kama walivyokubaliana wajumbe wa
Taasisi ya Kidemokrasia Tanzania (TCD) katika mazungumzo na Rais Jakaya
Kikwete hivi karibuni kwa mujibu wa vyombo vya habari, kwamba kwa kuwa
Katiba Mpya haitakuwa tayari katika uchaguzi mkuu ujao yafanyike
mabadiliko muhimu kwenye katiba ya mwaka 1977 ili iweze kutumika katika
uchaguzi huo.
Aliishauri serikali kutoa taarifa
rasmi kutoka katika mamlaka husika za serikali kuhusu suala hili zito na
nyeti kuhusu mabadiliko ya katiba ya 1977 kama sehemu ya maandalizi ya
uchaguzi ujao. Aliongeza kuwa pamoja na kwamba serikali haijatoa tamko
rasmi au mwongozo wa jinsi ya kuendesha zoezi hilo, baadhi ya vyama vya
siasa vimesha pendekeza mabadiliko wanayotaka yafanyiwe kazi.
“…Pamoja na mapungufu hayo ya
taarifa rasmi, sisi Mtandao wa Wanawake na Katiba tunatoa mapendekezo
yetu ya awali kuhusu mabadiliko katiba ya 1977 endapo yatalazimika
kufanyika.” Akitaja mapendekezo hayo Kaimu Mkurugenzi Mtendaji huyo wa
TGNP, alisema Mtandao wa wanawake na katiba unapendekeza uwiano wa
hamsini kwa hamsini katika nafasi zote za uongozi uingizwe katika
mabadiliko pamoja na uwepo wa tume huru ya uchaguzi masuala ambayo ni
kilio cha muda mrefu cha wananchi.
“Tunatarajia katika marekebisho ya
Katiba ya 1977 suala hili la 50/50 katika ngazi za maamuzi litapewa
kipau mbele. Tunadai pia katika mabadiliko ya Katiba ya 1977 sula la
mgombea huru lipewe kipaumbele kwani ni wananchi wengi hususan wanawake
wenye uwezo mkubwa lakini si wanachama wa chama chochote na hawana
utashi wa kujiunga na chama chochote. Iwapo suala la mgombea huru
litapitishwa wanawake na wanaume wengi watapata fursa ya kugombea nafasi
mbalimbali bila kufungwa na chama cha siasa. Hii itapanua demokrasia na
ushiriki katika masuala ya uongozi bila vikwazo na ubaguzi.”
*Imeandaliwa na www.thehabari.com
No comments:
Post a Comment