WAZIRI
wa Nishati na Madini, Mhe. Profesa Sospeter Muhongo jana ametia saini
Mkataba wa Mradi kujenga Miundombinu ya kuuziana umeme kati ya Zambia,
Tanzania na Kenya (ZTK) katika Mkutano wa Kumi wa kujadili mradi huo.
Katika utiaji saini Mkataba huo,
Profesa Muhongo alisema kuwa mchakato wa kuandaa Mkataba wa mradi huo
ulikwishafanyika tangu mwaka 2001 ambapo ulikuwa na vipengele ambavyo
kwasasa Mawaziri wa Nishati toka nchi zote tatu wameupitia na umefanyiwa
marekebisho.
Profesa Muhonga alisema kuwa
katika marekebisho hayo wamebadili kipengele kilichokuwa kinaeleza juu
ya uwepo wa Ofisi moja itakayosimamia mradi huo katika nchi zote tatu,
na badala yake wamekubaliana kuwa kila nchi ijisimamie yenyewe badala ya
kuwa na Ofisi moja pekee itakayosimamia mradi huo.
“Kwa upande wa Tanzania ujenzi
wa mradi huu umeshaanza kazi na mpaka hivi sasa asilimia 90 ya vifaa vya
ujenzi wa mradi vimeshawasili katika eneo la ujenzi,”alisema Profesa
Muhongo.
Akizungumzia maeneo ambayo mradi
huo utapita kwa upande wa Tanzania, Profesa Muhongo alisema kuwa, mradi
huo utapita maeneo ya mikoa ya Singida- Arusha-Namanga, na
Namanga-Isinya kwa Kenya, kwa upande wa Zambia utapita Mbeya–Iringa na
Iringa-Singida-Shinyanga. Ambapo unatarajia kusambaza umeme wa kuanzia
400kV.
Naye Katibu Mkuu wa Nishati
nchini Kenya, Mhandisi Joseph Njoroge alisema kuwa muungano huo wan chi
tatu utasaidia kupunguza tatizo la umeme katika nchi zote na Afrika kwa
ujumla kwani utapunguza gharama ya umeme pamoja na kuongeza ukuaji wa
uchumi katika uzalishaji.
Aidha aliongeza kuwa Serikali
yake itahakikisha kuwa Mkataba huo ndani ya siku Thelathini zijazo kabla
ya mkutano ujao kuanza, Mwanasheria Mkuu wa Kenya atakuwa umekwisha
usaini.
Kwa upande wake Waziri wa
Nishati na Madini nchini Zambia, Mh. Christopher Yaruma alisema kuwa
nchi yake imeshasaini Mkataba wa kuonyesha dhamira ya kuuziana umeme na
nchi ya Malawi, Namibia na Botswana.
Utiaji saini wa Mkataba huo
ulihusisha wadau mbalimbali wa maendeleo na wafadhili ikiwemo JICA,
COMESA, EU, Korea, Benki ya Dunia, AFD, Ufaransa na Mabalozi wa nchi
mbalimbali, ambapo wadau hao wameonyesha nia ya dhati katika kuendelea
kuisaidia Serikali hususani katika sekta ya Nishati.
Sambamba na hilo, mkutano wa
mwendelezo wa mradi huo badaa ya kuwa umesainiwa na viongozi wa Sheria
katika nchi husika unatarajiwa tena kufanyika mwanzoni mwa mwezi wa Kumi
na moja nchini Lusaka, Zambia.
No comments:
Post a Comment