Kipimo Abdallah
IDADI ya watu walioathirika na
ulaji wa chakula na unywaji wa togwa katika Kijiji cha Litapwasi Kata
Mpitimbi Wilaya ya Songea Vijijini Mkoa wa Ruvuma imefikia 325.
Kati ya hao hadi tunakwenda
mitamboni jana jioni watu 100 bado walikuwa wamelazwa ambapo 29 walikuwa
katika hospitali ya Peramiho na wengine 71 walikuwa wamelazwa katika
kituo maalum katika shule ya Msingi ya Kiwalawala.
Akizungumza na mwandishi wa
gazeti hili kwa njia ya simu jana, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ruvuma,
Kamishna Msaidizi wa Polisi Mihayo Msikhela alisema hadi kufikia jana
watu 225 waliokumbwa na kadhia hiyo walikuwa wameruhusiwa kutoka kwenye
vituo vya matibabu.
Kamanda Msikhela alisema tukio
hilo lilitokea katika sherehe ya kipaimara juzi jumapili kijijini
Litapwasi na limeacha majozi kwa watu wengi pamoja na ukweli kuwa hamna
mtu aliyepoteza maisha hadi sasa.
Msikhela alisema wataalamu wa
afya wanaendelea kuwapatia matibabu waathirika hao ili kuhakikisha kuwa
wanapata nafuu wote na kurejea majumbani mwao.
Kamanda huyo alisema
hadi sasa wamewashikilia watu watano ambao wanasadikiwa kuhusika na
tukio hilo ambapo mmoja wapo ni baba wa mtoto aliyekuwa anafanyiwa
sherehe, Enes Nungu ambaye pia ni mwathirika.
Msikhela alisema vyakula na
vimiminika vingine ambavyo vilivyohusika vitafikishwa Dar es Salaam kwa
Mkemia Mkuu wa Serikali kwa uchunguzi zaidi ambapo majibu yake yatakuwa
na mwanga wa kuwaongoza kwenye uchunguzi wao.
Katika tukio jingine, Kamanda
huyo alisema mwanachi mmoja aliyejulikana kwa jina la Nicolaus Pokela
amekutwa amekufa nje ya nyumba ya mdogo wake Gidion Pokela baada ya
kunywa sumu ambayo hutumika kuuwa wadudu wanaharibu kahawa.
Kamishna Msaidizi alisema
taarifa za awali zinaonyesha kuwa marehemu alikuwa anatuhumiwa kuchoma
nyumba ya mkewe ambaye walikuwa na ugomvi.
Pia Kamishna Msaidizi alisema
jana majira ya saa tatu usiku vijana wawili waliuwawa na wananchi baada
ya kuiba pikipiki na kukimbia nayo ambapo mmoja wao alinusurika na
kukimbia kusikojulikana
Msikhela alitoa wito kwa
wananchi kuacha tabia ya kuchukua sheria mkononi kwani kufanya hivyo ni
uvunjifu wa sheria za nchi na kuwataka watoe taarifa Polisi pindi
wakiwakamata watuhumiwa.
No comments:
Post a Comment