Dar es Salaam
KAMPUNI ya Insights Productions
Limited kwa udhamini wa Kampuni ya Azam Tanzania imeandaa maonesho
makubwa ya keki yanayotarajia kufanyika jijini Dar es Salaam na
kuwakutanisha wadau mbalimbali wa uandaaji na utayarishaji wa keki.
Maonesho hayo yatajulikana kama ‘Azam World of Cakes Exhibition’.
Akizungumza na vyombo vya habari
leo jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Kampuni ya Insights Productions
Limited, Marion Elias alisema maonesho hayo yanatarajiwa kuwakutanisha
wadau mbalimbali binafsi, makampuni na taasisi waandaaji wa keki nchini
Tanzania ikiwa ni sehemu ya kubadilishana uzoefu na kujifunza ubunifu
zaidi wa shughuli hizo.
Bi. Elias alisema dhumuni la
maonesho hayo ambayo yanatarajiwa kufanyika Desemba 6, 2014 jijini Dar
es Salaam ni pamoja na kusherehekea taaluma ya uokaji keki kwa kuonesha
ubunifu na utaalam wa utengenezaji na upambaji wa keki bidhaa
inayopendwa na watu wengi na kutumika katika shughuli anuai za kijamii.
Alisema washiriki wa tamasha hilo mbali na kushindanisha na kuonesha
bidhaa zao za keki pia wanatarajia kupata semina ya mafunzo juu ya
utengenezaji bora wa keki ikiwa na lengo la kuboresha zaidi taaluma zao.
Alisema washiriki hao pia
watafanya maonesho ya utayarishaji wa vyombo vya kutengenezea keki,
utayarishaji wa unga wa ngano kwa ajili ya kupikia keki, kutambua unga
bora wa keki, uchanganyaji wa unga na viungo vingine kwa ajili ya
uboreshaji wa radha ya keki.
Alisema maonesho mengine
yatakayofanywa na wadau hao wa keki ni pamoja na uhifadhi bora wa keki
kwa muda mrefu bila kuharibika na washiriki kuonesha maumbo mbalimbali
ya keki yenye mvuto kwa watumiaji wa keki na jamii nzima.
Alisema maonesho hayo
yanayodhaminiwa na Azam watengenezaji wa unga bora kwa ajili ya
kutengenezea bidhaa hiyo, yatawashindanisha wadau wa uandaaji keki na
pia washindi watakao tajwa na majaji wa maonesho watajipatia fedha
taslimu na bidhaa mbalimbali.
“…Onesho hili litahusisha jamii
yote inayojishughulisha na utengenezaji wa keki, upambaji wa keki,
wauzaji wa keki na wanaojishughulisha na bidhaa mbalimbali zinazotumika
kutengeneza keki kama vile unga wa ngano wa Azam,”
alisema Mkurugenzi wa Insights Productions Limited, Bi. Elias.
Akifafanua zaidi Mkurugenzi huyo
alisema onesho hilo litajumuisha bekari na hoteli mbalimbali, Vyuo vya
taaluma ya hotelia toka Tanzania na majirani (Afrika Mashariki) pamoja
na watengenezaji keki binafsi. Wananchi watakaotembelea maonesho hayo
ambayo hayata kuwa na kiingilio watapata fursa ya kujionea aina na
mitindo mbalimbali ya utengenezaji wa keki pamoja na kuonja bidhaa hiyo
kwenye maonesho ambayo yatafanyika Serena Hoteli jijini Dar es Salaam.
Akizungumzia maonesho hayo Mratibu
wa Matangazo na Uhusiano wa Umma wa kampuni ya SSB, Mohammed Ramadhan
alisema Azam ikiwa ni kampuni inayotengeneza unga bora wa kutengenezea
keki imeamua kudhamini ikiwa ni ishara ya kutambua taaluma hiyo ya
uokaji keki nje na ndani ya Tanzania.
*Imeandaliwa na www.thehabari.com
No comments:
Post a Comment