Na mwandishi wetu, Arusha
JUMUIYA ya kimataifa imepitisha Azimio la Arusha lenye lengo la kukabiliana na ujangili na kuendeleza wanyama.
Azimio
hilo limepitishwa baada ya mkutano wa siku mbili ambapo pia imekubalika
kwamba hali ya baadae ya wanyama barani Afrika ni suala linalohitaji
uwajibikaji wa pamoja.
Aidha
nchi za Afrika zimetakiwa kuukomesha ujangili na kufanya juhudi ya
kuhakikisha wanyama walio katika hatari ya kutoweka wanalindwa na
kuhakikisha kundi hilo linakua.
Wanyamama ambao kwa sasa wapo hatarini kutoweka ni tembo, faru na simba.
Mkutano
huo uliojumuisha mataifa mbalimbali ya Afrika na jumuiya za kimataifa
na kufunguliwa na Waziri wa Mali asili na Utalii, Lazaro Nyalandu kwa
niaba ya rais Jakaya Kikwete, umetoa wito kwa mataifa yote kufanyakazi
kwa pamoja kukabili ujangili kwa kushirikisha wananchi wanaoishi na
kutegemea wanyamapori hao na mapori yenyewe.
Kwa
mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mtaalamu wa Mawasiliano wa Mashirika ya
Umoja wa Mataifa nchini, Hoyce Temu, baada ya mkutano ambao uliangalia
sheria zilizopo za kulinda mapori na wanyamapori,uhalisia wa mifumo ya
ujangili na uhifadhi, washirika wa maendeleo nao walielezea nia zao za
kuendelea kusaidia uhifadhi wa wanyamapori na mapori katika ukanda wa
Afrika ikiwamo Tanzania.
Mkutano
huo ambao ulishirikisha mataifa ya Afrika, wajumbe wa Bunge la Marekani
(Congress) Mashirika ya Umoja wa Mataifa, mataifa washirika wa
maendeleo, wanazuoni na wawakilishi wa taasisi zisizo za serikali
umeelezwa kuwa sehemu ya utekelezaji wa makubaliano ya London, Uingereza
ya kustawisha wanyamapori na mapori yanayowahifadhi.
Awali
akifungua mkutano kwa niaba ya Rais Kikwete, Waziri Nyalandu alisema
kwamba mataifa yasidharau nguvu ya pamoja katika kukabiliana na
ujangili.
Alisema
pia kwamba hali ya baadae ya wanyamapori katika bara la Afrika ni
wajibu wa kila mtu na kila taifa na mamlaka nyingine ambazo ni wadau.
Alisema
Tanzania katika mchango wake imeanzisha mkakati wa kukabiliana na
ujangili na kuunda mamlaka ya wanyamapori ili kuwa na uhakika wa
kuendeleza masuala yanayohusu hifadhi na changamoto zake kwa kasi na
karibu zaidi.
Washiriki
wa mkutano huo wa siku mbili walielezea umuhimu wa kulinda mali asili
hizo kwa kuwa ni msingi wa maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa nchi
zote.
Akizungumzia umuhimu wa mali asili Mratibu
Mkazi wa mashirika ya Umoja wa Mataifa na mwakilishi wa Shirika la
Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) nchini, Alvaro Rodriguez,
alisema ujangili na uhalifu mwingine kwa wanyamapori na hifadhi zao ni
changamoto kubwa kwa uchumi unaotegemea utalii, mazingira na maendeleo
endelevu.
Alisisitiza kwamba suala la uhalifu kwa wanyamapori na mapori yao ni lazima kufanyiwa kazi kitaifa na kimataifa ikiwamo kikanda.
Mratibu
huyo alisema kwamba Umoja wa Mataifa utaendelea kusaidia juhudi hizo za
kuhifadhi wanyama na mapori kwa kusaidia kutoa elimu na kutatua
changamoto za kiuchumi zinazokabili watu wanaoishi jirani na misitu
hiyo.
Alisema
Umoja huo utaendelea kusaidia kupeleka elimu ya menejimenti ya
wanyamapori na misitu ili wakazi wa maeneo hayo wafaidi raslimali hizo
na kuzitunza.
Hata hivyo alizitaka jumuiya za kimataifa na mataifa kushirikiana katika kufanikisha adhma hiyo.
Akizungumza
kwa niaba ya ICCF ambao ni wenyeji wenza wa mkutano huo, Makamu
Mwenyekiti Dk Kaush Arha, alisema mkutano huo ulikuwa na manufaa makubwa
hasa wito wa kuweka mikakati ya kurejesha makundi ya wanyama walio
katika hatari ya kutoweka kama tembo, faru na simba.
Aidha
mkutano umekubaliana juu ya masuala kadhaa ambayo yatasaidia Tanzania
kuingia makubaliano na majirani zake kuhifadhi wanyamapori.
Amesema
Jumuiya ya Ulaya ambayo imekuwa mshirika katika kukabilina na ujangili
na hifadhi ya wanyama imefurahishwa na mkutano huo kwa kuamini kwamba
kunatakiwa kuchukuliwa hatua za kikanda kuweza kunusuru wanyamapori kwa
kuchukua hatua za pamoja.
Ameipongeza
Tanzania na majirani zake kwa kuchukua hatua madhubuti za kikanda
kukabiliana na ujangili na uharibifu wa mazingira na kusema Jumuiya ya
Ulaya ipo tayari kusaidia katika juhudi hizo.
No comments:
Post a Comment