Na. Aron Msigwa –
MAELEZO
Chuo cha Elimu ya
Biashara kampasi ya Dar es salaam kimetoa tuzo kwa wanafunzi bora 12 waliohitimu
na kufanya vizuri katika masomo yao kwa mwaka wa masomo 2014/2015 ikiwa ni
sehemu ya utaratibu wa chuo hicho kuenzi na kuthamini mchango walioutoa katika maendeleo
ya taaluma chuoni hapo.
Akikabidhi tuzo hizo katika
hafla fupi iliyofanyika jana jijini Dar es salaam, aliyekuwa Kamishna Mkuu wa
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na mwenyekiti wa sasa wa wanafunzi waliomaliza chuo cha CBE, Bw. Harry Kitilya amesema
kuwa wahitimu hao wanayo nafasi kubwa ya kutumia elimu waliyoipata na kuwa
mfano katika kuleta mabadiliko nchini.
Amesema chuo hicho
tangu kuanzishwa kwake mwaka 1965 kimekua
mfano wa kuigwa kwa kuwajengea uwezo wanafunzi wanaohitimu ili waweze kutatua changamoto mbalimbali
zinazoikabili sekta ya Biashara nchini kwa kuongeza nafasi za ajira kwa kujiajiri wenyewe kupitia shughuli za ujasiriamali,uanzishaji
wa makapuni na miradi mbalimbali.
Bw.Kitilya amewataka
wahitimu hao kujiendeleza zaidi kielimu ili waweze kukabiliana na ushindani wa
ajira uliopo hususan katika soko la nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki na
kujenga utamaduni wa kufanya kazi kwa bidii na kuepuka vitendo vya rushwa na uzembe
pindi wanapoingia katika ajira.
Kwa upande wake Mkuu wa
Chuo hicho Prof. Emanuel Mjema akizungumza na wahitimu wa mwaka 2014 wakati wa
hafla ya utoaji wa tuzo ulioshuhudiwa na wanafunzi waliosoma miaka ya nyuma ni
utaratibu wa chuo hicho kuenzi na kuthamini juhudi walizozionyesha katika
taaluma.
Amesema utoaji wa tuzo hizo umehusisha fani za Uhasibu,Udhibiti wa Biashara,
Usimamizi wa Masoko,Manunuzi na Ugavi na kuongeza kuwa utafanyika katika kampasi
nyingine za chuo hicho zilizoko Zanzibar, Mbeya, Dodoma na Mwanza.
“Siku ya leo mbali na
zoezi hili la utoaji wa tuzo, wahitimu wote wa sasa na wa zamani wanakutana
kujadili namna ya uendelezaji wa chuo chetu, siku hii ni muhimu sana kwa kuwa
inaongeza ushiriki wao katika kujadili masuala mbalimbali ya kukiendeleza chuo”
Amesema Prof. Mjema.
Ameongeza kuwa lengo la
kuwakutanisha wahitimua wa miaka iliyopita ni kujenga umoja imara na kupata
mrejesho kutokana na huduma wanazozitoa kwa jamii, mahitaji ya soko la ajira na
mabadiliko ya kiuchumi yaliyopo.
Kwa upande wao baadhi
ya wahitimu wa mwaka 2014 na wale miaka iliyopita wakizungumza kwa nyakati
tofauti wakati wa hafla hiyo, wameiomba Serikali kendelea kupanua wigo wa Elimu
ya Biashara kwa kuongeza matawi mengi zaidi kwa lengo la kuwafikia wananchi
wengi katika maeneo yao.
Wameiomba Serikali
kupitia wizara ya Viwanda na Biashara kuwaendeleza na kuwawezesha wahitimu wanaoonyesha
nia ya kujiajiri wenyewe na kuanzisha makampuni yao hapa nchini.
Aidha ,wametoa wito kwa
walimu kutoa mafunzo yanayoendana na mabadiliko ya kiuchumi yanayotokea duniani
ili kuwawezesha kukidhi soko la ajira huku wakitoa wito kwa wahitimu wa vyuo kujenga utamaduni wa
kujitolea ili waweze kupata uzoefu.
MWISHO.
No comments:
Post a Comment