Waziri Mkuu, Mizengo
Pinda akizungumza na Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu
(wapili kushoto) na Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Aggrey
Mwanri (kulia) baada ya kufunga Mkutano wa kupiga vita ujangili wa
wanayamapori na kuendeleza uhifadhi wa wanayamapori mjini Arusha
Novemba 8, 2014. Kushoto ni Mbunge wa Kahama, James Lembeli.Wapili
kulia ni Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika ya Mashariki, Dkt Richard
Sezibara(Picha na ofisi ya Waziri Mkuu)
…………………………………………………………………………….
* Ataka iundwe timu kufuatilia utekelezaji wa Azimio la Arusha 2014
WAZIRI MKUU Mizengo
Pinda amesema inahitajika dhamira ya kweli kutoka kwa wadau wote katika
kutekeleza Azimio la Arusha la kukabiliana na ujangili na kuendeleza
hifadhi za wanyama katika nchi za Afrika Mashariki na zilizo Kusini mwa Ikweta.
Akizungumza na waandishi
wa habari jana jioni (Jumamosi, Novemba 8, 2014) mara baada ya kufunga
mkutano wa kikanda wa siku mbili uliojadili mbinu za kupambana na biashara
haramu ya wanyamapori ulioandaliwa na Wizara ya Maliasili na Utalii
jijini Arusha, Waziri Mkuu alisema: “Suala hili linataka uwajibikaji wa
pamoja. Mashirika na taasisi, wananchi na viongozi sote kama wadau
wakuu, kila mmoja anapaswa kushiriki vita hii kama kweli tunataka
tuitokomeze.”
“Kwenye hili Azimio la
Arusha na nyie waaandishi wa habari pia mna sehemu yenu mmetajwa…
wamesema wanatafuta jinsi ya kushirikiana na vyombo vya habari ili
visaidie kutoa elimu kwa jamii kama njia ya kuelimisha umma,” alisema.
Waziri Mkuu aliwaeleza
waandishi hao kwamba Azimio hilo lina vipengele 20 ambavyo vinataka
utekelezaji katika ngazi ya nchi mojamoja, ngazi na kanda na ngazi ya
kimataifa kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo.
“Nimepata faraja kwamba mkutano huu haukuisha kijumlajumla tu, bali
umekuja na maazimio 20 ambayo yametengwa kwa ajili yetu sisi wa ndani,
mengine yanahusisha ushirikiano wa kikanda na yako mengine yanawahusisha
wadau wa maendeleo,” alifafanua.
Ili kutekeleza azimio
hili, nimeshauri iundwe timu itakayoshirikisha vyombo vingi zaidi badala
ya kuiachia Wizara ya Maliasili na Utalii peke yake. Timu hii ikutane
kila baada ya miezi sita ili kufuatilia utekelezaji wa maazimio haya na
ikibidi Waziri atoe taarifa bungeni kuhusu utekelezaji huo,” alisema
Waziri Mkuu.
Mapema, akizungumza na
washiriki wa mkutano huo wakati wa kuufunga, Waziri Mkuu alisema kuwepo
kwa watu wa ngazi tofauti kwenye mkutano huo ni kielelezo tosha cha
umakini wao na nia thabiti ya kutokomeza ujangili katika ukanda huu.
“Tumeanzisha vita,
tusisahau kwamba bado kuna kazi kubwa mbele yetu na vita haijaisha.
Tuzidishe mapambano katika sehemu tatu: kwenye nchi unakofanyika
ujangili, nchi ambazo nyara zinapitishwa na nchi zinazopokea ama kununua
hizo nyara,” alisema Waziri Mkuu.
“Nakubaliana nanyi
kwamba hakuna nchi inayoweza kukabili suala la ujangili ikiwa peke yake.
Tunahitaji tuwe na sera mahsusi, sera ya pamoja ya kutuunganisha na
kutuongoza wakati tukitekeleza Azimio hili kwa kusaidiana na wadau wa
maendeleo,” alisema.
Alisema Azimio hilo
litaipa kazi ya ziada ya Wizara ya Maliasili na Utalii ambapo kazi kubwa
itakuwa ni kusimamia na kuhakikisha utekelezaji wa wa Azimio hilo
unakuwa wa ufanisi.
Jumla ya nchi tisa
zimetia saini azimio hilo mbele ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda. Nchi hizo
ni Burundi, Kenya, Uganda, Msumbiji, Tanzania, Sudan Kusini, Zambia,
Rwanda na Malawi.
No comments:
Post a Comment