Waziri
Mkuu, Mizengo Pinda akifungua mkutano mkuu wa mwaka wa Afya (Annual
Health Summit ) kwenye Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Mwalimu
Julis Nyerere jijini Dar es salaam Novemba 14, 2014. (Picha na Ofisi ya
Wazri Mkuu) Baadhi
ya washiriki wa Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Afya (Annual Health Summit )
wakimsikiliza Waziri Mkuu,Mizengo Pinda wakati alipofungua mkutano wao
kwenye Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Mwalimu Julius Nyerere
jijini Dar es salaam Novemba14, 2014. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
……………………………………………………………………………….
WAZIRI MKUU Mizengo Pinda ameitaka Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii ipanue wigo wa utoaji huduma za msingi kwa kuishirikisha zaidi sekta binafsi nchini.
“Ninawasihi Waziri wa Afya na
Naibu wake kwa vile ni wapya bado wabadili mtizamo wa wizara hii kwa
kushirikisha zaidi wadau wa sekta binafsi kwenye utoaji wa huduma ili
wasaidie kupunguza mzigo mkubwa ilionao Serikali,” alisema.
Ametoa kauli hiyo leo mchana
(Ijumaa, Novemba 14, 2014) wakati akifungua Mkutano wa wa Kwanza wa
Kitaifa wa Sekta ya Afya wa mwaka 2014 ulioanza leo kwenye ukumbi wa
mikutano wa kimataifa wa Mwalimu Nyerere, jijini Dar es Salaam.
Waziri Mkuu ambaye amefungua
mkutano huo kwa niaba ya Rais Jakaya Kikwete aliyeko nje ya nchi kwa
matibabu alisema: “Kuna tatizo la kukumbatia utoaji wa huduma … tunazo
hospitali kubwa za wilaya zinazomilikiwa na taasisi za dini. Hivi ni kwa
nini kama Wizara msiwasaidie kuwahudumia watumishi wao au kuwapa ruzuku
kwenye dawa ili kuwawezesha kutoa huduma kwa ufanisi zaidi?,” alihoji
Waziri Mkuu na kushangiliwa na washiriki wa mkutano huo.
“Hata ukiangalia takwimu kwenye
utoaji wa huduma za afya kupitia mifumo ya bima ya afya utabaini kuwa ni
asilimia 18 tu wananchi wanatumia bima ya afya na kati ya hao, asilimia
15.3 ni mifuko ambayo imeanzishwa na Serikali. Ni kwa nini basi
msiwasaidie wadau wa sekta binafsi ili wachangie huduma hii na idadi wa
watumiaji wa mfumo huu iongezeke haraka?,” alihoji.
Akizumgumzia kuhusu uwiano kati
ya daktari na mgonjwa, Waziri Mkuu alisema uwiano uliopo ni mbaya na
kwamba hakuna njia ya haraka ya kupunguza tatizo hilo isipokuwa kwa
kuishirikisha sekta binafsi kwenye ujenzi wa vyuo vikuu vya elimu ya
tiba na sayansi za jamii.
“Uwiano wa sasa hapa nchini ni
daktari mmoja kwa wagonjwa 75,000 wakati viwango vya kimataifa vinataka
daktari mmoja awahudumie wagonjwa 7,000. Kwa wauguzi, hapa nchini
muuguzi mmoja anahudumia wagonjwa 6,000 wakati viwango vya kimataifa
vinataka muuguzi mmoja ahudumie wagonjwa 500,” alisema.
“Kwa uwioano huu safari bado ni
ndefu. Tunapaswa tuangalie tutafanyaje ili watu binafsi waje kuwekeza
kwenye elimu ya juu ya sayansi na tiba, wajenge vyuo vya tiba, wajenge
hospitali kubwa, na sisi pia kwa upande wa Serikali ni lazima tuseme
tunawapa vivutio gani hawa wawekezaji hadi wakubali kuwekeza kwenye eneo
hilo,” alisema.
“Tunataka mkutano huo uje na
mapendekezo ambayo mnataka Serikali iyafanyie kazi na hatimaye isaidie
kuboresha utoaji wa huduma za afya kwa wananchi,” alisema Waziri Mkuu.
Akizungumza na waandishi wa
habari mara baada ya kufungua mkutano huo, Waziri Mkuu alisema Serikali
inaendelea kudhibiti ugonjwa wa ebola kwenye vituo vya mipakani na
kwenye viwanja wa ndege.
“Mpaka sasa hatujapata kesi ya
ugonjwa wa ebola hapa nchini… changamoto kubwa ni ukubwa wa mipaka yetu.
Si wageni wote wanaoingia nchini wanapita kwenye vituo rasmi, wapo
wanaotumia njia za vichochoroni. Rai yangu ni kuwaomba Watanzania wawe
waangalifu kutambua ni wageni gani wanaingia kwenye maeneo wanayoishi,”
alisema.
Mkutano huo wa siku mbili unamalizika kesho (Jumamosi, Novemba 15, 2014).
Waziri Mkuu amerejea mjini Dodoma kuendelea na kikao cha Bunge.
No comments:
Post a Comment