Naibu Waziri wa Afya Zanzibar
Mahmoud Thabit Kombo akizungumza na waandishi wa habari kuhusu
maadhimisho ya siku ya kisukari Duniani Ofisini kwake Mnazimmoja Mjini
Zanzibar.
…………………………………………………………………………..
NA RAMADHANI ALI
Wananchi wameshauriwa kujiepusha
na vihatarishi vinavyoweza kupelekea kupata ugonjwa wa kisukari na
kujenga tabia ya kupima afya zao ili kujuwa matatizo yanayowakabili.
Naibu Waziri wa Afya Mahmoud
Thabit Kombo ametoa ushauri huo alipokuwa akizungumza na waandishi wa
habari Ofisini kwake Mnazimmoja katika kuadhimisha siku ya kisukari
Duniani.
Alisema tatizo la ugonjwa wa
kisukari na vifo vinavyosababishwa na ugonjwa huo limekuwa kubwa na
inakisiwa zaidi ya watu milioni 346 duniani wanasumbuliwa na ugonjwa
huo.
Alisema ongezeko kisukari katika
nchi nyingi linasababishwa na watu kubadili mfumo wao wa maisha na
mabadiliko ya kijamii na kiutamaduni.
Naibu Waziri ameongeza kuwa kwa
mujibu wa utafiti uliofanywa mwaka 2011 hapa Zanzibar, unaonyesha
kiwango cha ugonjwa wa kisukari ni asilimia 3.7 ambayo ni sawa na watu
50,000.
Alisema kwa mujibu wa takwimu
zinazokusanywa katika Hospitali kuu ya Mnazimmoja pekee kunawastani wa
wagonjwa wapya wa kisukari 300 kila mwaka na zaidi ya watu 180,000 wapo
hatarini kupata maradhi hayo kutokana na uzito uliokithiri.
Amewakumbusha wananchi kuwa
ugonjwa wa kisukari hauponi na mtu akishaupata hulazimika kutumia dawa
katika uhai wake wote na kufuata ushauri wa wataalamu wa afya.
“Jambo la msingi ninalosisitiza ni
kwamba ugonjwa wa kisukari hauponi, mtu anapothibitika kuwa nao
inamaana ataendelea kuwa nao katika maisha yake yote na atalazimika
kutumia dawa ama sindano katika uhai wake wote,” alieleza Naibu Waziri.
Katika kujikinga na ugonjwa huo
Naibu Waziri amewasisitiza wananchi kufanya mazoezi, kujiepusha na
matumizi ya pombe na matumizi ya bidhaa zinazotokana na tumbaku pamoja
na kuzingatia umuhimu wa lishe bora.
Amewashauri wananchi kuweka
umuhimu wa kuchunguza afya zao kama ni njia moja wapo ya kinga kwani
inakadiriwa kuna zaidi ya asilimia 50 ya watu wenye ugonjwa wa kisukari
ambao hawajijui.
Akizungumzia kadhia ya kisukari
Mkuu wa Kitengo cha ugonjwa wa kisukari Dkt. Faiza Kassim Suleiman
alisema tatizo kubwa linalowapata wenye maradhi hayo ni ganzi, kupoteza
nuru ya macho na kupungua nguvu za kiume.
Hata hivyo amesema bado hakujawa
na mikakati imara iliyoandaliwa kukabiliana na ongezeko kubwa la ugonjwa
huo licha ya kuwepo dawa katika Hospitali na vituo vya Afya.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya watu
wanaoishi na ugonjwa wa kisukari Zanzibar Waziri Said Othman amesema
dawa za ugonjwa huo zinapatikana lakini tatizo linalowakabili ni dawa
za maradhi mengine ambayo yanaenda sambamba na kisukari ikiwemo sinikizo
la damu.
Amewashauri madaktari kuongeza
juhudi katika kuwashughulikia wagonjwa wa kisukari wenye vidonda kwani
tiba yake huchukua muda mrefu kabla mgonjwa kupona.
No comments:
Post a Comment