Na:Beatrice Lyimo- Maelezo-DSM.
Serikali ya Marekani na Tanzania
zimetiliana saini kwa ajili ya kuandaa miradi katika sekta ya nishati
itakayofadhiliwa katika awamu ya pili ya Mkataba wa Millennium Challenge
Corporation (MCC).
Utiaji saini wa mkataba huo
ulifanyika katika Wizara ya Fedha jijini Dar es Salaam ambapo Makamu wa
Rais wa MCC Bw. Kamran Khan anayeshughulikia Mikataba na Uendeshaji
wake pamoja na Waziri wa Fedha wa Tanzania , Mhe. Saada Mkuya
ukishuhudiwa na Balozi wa Marekani nchini Mark Childress.
Akiongea wakati wa hafla ya
utiaji saini wa mkataba huo, Waziri wa Fedha, Mhe. Saada Mkuya alisema
kuwa MCC imeipatia Serikali ya Tanzania shilingi bilioni 17 kwa ajili ya
utekelezaji wa mradi wa MCC II ambapo mraadi huo unatarajiwa kuanza
kutekelezwa hapo mwakani ukiwa na lengo la kusaidia miundombinu ya umeme
nchini.
Makubaliano hayo ni muendelezo
wa ubia imara kati ya Marekani na Tanzania kati ya mwaka 2008 na 2013
ambapo MCC ilitekeleza mkataba wa miradi mikubwa ya uwekezaji katika
sekta za maji, barabara, na nishati ya umeme nchini.
Miradi hiyo iligharimu jumla ya
Dola za kimarekani milioni 698, chini ya mkataba huo mtandao wa nyaya za
umeme wenye zaidi ya kilometa 3,000 ulijengwa.
Kwa kuzingatia mafanikio hayo
katika utekelezaji wa wa programu zilizokuwa chini ya mkataba wa kwanza
kuwahi kutolewa na MCC, taasisi hiyo iliichagua tena Tanzania kuingia
katika mkataba wa pili utakaolenga sekta ya Nishati katika miundombinu
pamoja na mageuzi ya kisera na mifumo ya udhibiti na kitaasisi.
Aidha, upembuzi yakinifu
utaiwezesha Tanzania kuandaa miradi itakayoleta mageuzi katika sekta ya
Nishati ikiwa ni pamoja na kuboresha utendaji wa shirika la ugavi wa
umeme Tanzania (TANESCO) na Shirika la Umeme Zanzibar (ZECO) katika
maeneo ya kiufundi, usimamizi wa fedha na uendeshaji na kuongeza kiwango
cha upatikanaji wa huduma ya umeme katika maeneo ya vijijini.
Shirika la Changamoto za Milenia
(MCC) ni Taasisi ya Serikali ya Marekani inayotoa misaada kwa nchi
zinazoendelea, shughuli zake zinajengwa katika misingi kwamba msaada
utaleta ufanisi na matokeo makubwa pale unapoimarisha utawala bora,
uhuru wa kiuchumi na uwekezaji katika watu ambao unakuza uchumi na
kuondoa umaskini.
No comments:
Post a Comment