Mkuu wa Wilaya ya Hanang’ Mkoani Manyara, Christina Mndeme amesema atawachukulia hatua kali wazazi na walezi wanaowadanganya watoto wao wafeli mtihani makusudi kwa vile hawana fedha za kulipia ada za masomo.
Mndeme aliyasema hayo juzi kwenye kikao cha wadau wa elimu wa wilaya ya Hanang’ na kudai kuwa wazazi na walezi wasikwepe jukumu la kuwasomesha watoto wao wa jamii ya kifugaji na wakulima kwani elimu ndiyo urithi.
“Kuwashawishi watoto wasifaulu masomo kwa vile mzazi hana fedha za kumsomesha ni makosa makubwa sana na kukwepa majukumu, endapo nitabaini mtu anayefanya hivyo nitamshughulikia ipasavyo,” alisema Mndeme.
Alisema wazazi na walezi wanaofurahia watoto wao wakachunge mifugo au wakalime badala ya kuwapeleka shuleni, hawana nafasi kwenye wilaya hiyo hivyo atahakikisha jambo hilo analikomesha.
Kwa upande wake, Ofisa elimu msingi wa wilaya ya Hanang’ Oscar Kapinga alisema wilaya hiyo ina jumla ya shule za msingi 114, ambapo wanafunzi 5,140 wa shule 96 walifanya mtihani wa kumaliza elimu ya msingi mwaka jana.
Kapinga alisema wanafunzi 193, kati yao 115 ni wavulana na 78 ni wasichana hawakufanya mtihani kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo utoro, vifo, ugonjwa na wanafunzi wanne wa uoni hafifu walifanya mtihani.
“Miongoni mwa mafanikio ya elimu wilayani kwetu kwa mwaka uliopita ni kuongezeka kwa kiwango cha ufaulu kwa asilimia 100 kutoka asilimia 16 mwaka 2012 hadi asilimia 32.72 mwaka 2013,” alisema Kapinga.
No comments:
Post a Comment