Waziri
wa Wanawake wa Chuo cha Elimu ya Biashara Dar es salaam (CBE) Bi.
Mwajuma Sangali akiwaongoza wananfunzi wa Kike wa chuo hicho wakati wa
uzinduzi wa mchakato wa kuanzisha mfuko wa Jumuiya ya Wanafunzi wa kike
wenye lengo la kuwakomboa kielimu.
Kikundi
cha maagizo cha chuo hicho kikionyesha namna vitendo vya ukiukwaji wa
maadili unavyodhibitiwa chuoni hapo na namna uongozi wa chuo hicho
unavyowachukulia hatua za kinidhamu wanaokiuka maadili ya chuo hicho. Igizo la wanafunzi wakiwa kwenye majadiliano chuoni hapo bila kujali tofauti za jinsia . Mkurugenzi
wa Utawala na Utumishi wa Wizara ya Viwanda na Biashara Dkt. Mary
Mwangisa (kulia) akizungumza na wanafunzi wa Kike wa chuo cha CBE
kampasi ya Dar es salaam wakati wa uzinduzi wa mchakato wa kuanzisha
mfuko wa Jumuiya ya Wanafunzi wa kike chuoni hapo wenye lengo la
kuwakomboa kielimu. Baadhi
ya wanafunzi wa kike wa chuo hicho wakifurahia matukio mbalimbali
yaliyokuwa yakiendelea wakati wa hafla ya uzinduzi wa mchakato wa
kuanzisha mfuko wa Jumuiya ya Wanafunzi wa kike chuoni hapo wenye lengo
la kuwakomboa kielimu, kisiasa na kiutamaduni leo jijini Dar es salaam.Wanafunzi
wa Kike wa Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) wakiwa katika picha ya
pamoja na mgeni rasmi Mkurugenzi wa Utawala na Utumishi wa Wizara ya
Viwanda na Biashara Dkt. Mary Mwangisa (katikati).
Picha na Aron Msigwa – MAELEZO
…………………………………………………………………………………………….
Na Aron Msigwa – MAELEZO, Dar es salaam.
Wanafunzi wanawake wa Chuo cha
Elimu ya Biashara Dar es salaam (CBE) wamezindua mchakato wa kuanzisha
mfuko wa Jumuiya ya wanafunzi wa kike wenye lengo la kumkomboa na
kumwezesha mwanafunzi wa kike kujitambua, kielimu, kisiasa na
kiutamaduni.
Akizungumza na jumuiya ya
wanafunzi wa kike wa chuo hicho wakati wa uzinduzi wa mfuko huo leo
jijini Dar es salaam Mkurugenzi wa Utawala na Utumishi wa Wizara ya
Viwanda na Biashara Dkt. Mery Mwangisa ambaye alikuwa mgeni rasmi katika
hafla hiyo amesema kuwa kuanzishwa kwa jumuiya hiyo ni ishara ya umoja
na mshikamano wa wanafunzi wa kike chuoni hapo.
Amesema kuanzishwa kwa mfuko
huo kunatokana na kuongezeka kwa changamoto mbalimbali zinazowakabili
wanawake pia kukosekana kwa mifuko ya aina hiyo katika taasisi nyingi
za elimu ya juu hapa nchini.
Ameeleza kuwa malengo ya
mfuko huo ni kumwezesha mwanafunzi wa kike wa CBE kujitambua kielimu,
kisiasa na kiutamaduni na kuongeza kuwa yamekuja wakati muafaka
kufuatia mabadiliko yaliyopo sasa ya kiuchumi, kisiasa, kijamii na
kiutamaduni.
Amefafanua kuwa mfuko huo
ulioanzishwa katika chuo hicho ni fursa pekee ya kuwawezesha wanafunzi
wa kike kunufaika kwa kupata elimu bora bila vikwazo.
“Napenda kutumia fursa hii
kuushukuru uongozi wa chuo hiki kwa kuonyesha njia ya kuwajali wanawake
na pia katika kuweka taratibu nzuri za kulinda maadili, katika maisha
yangu sijawahi kusikia chuo kikuu chochote kimezindua jukwaa la wanawake
lenye malengo mazuri kama yenu” Amesema Dkt. Mwangisa.
Ameeleza kuwa kwa muda mrefu
wanawake kote nchini wamekuwa na juhudi mbalimbali za kujikomboa
kiuchumi pamoja na kulitumikia taifa kwa kushika nyadhifa mbalimbali
serikalini kwa ufanisi mkubwa na kuwataka kuendelea kufanya kazi kwa
bidii pindi wanapokabidhiwa madaraka.
“Ninapowaangalia ninyi nafarijika maana naona viongozi wakuu wa serikali, naona marais na pia wakurugenzi wa biashara”
Akizungumza kuhusu kuanzishwa
kwa mfuko huo na mafanikio yake Dkt. Mwangisa amesema kuwa atatoa
ushirikiano kwa wanafunzi hao ili kuhakikisha kuwa mfuko huo unajengewa
uwezo wa kusimama na kuwanufaisha wanawake wanaokumbwa na changamoto
zinazokwamisha maendeleo yao ikiwemo ukosefu wa fedha.
Amesema kuwa kukamilika kwa
taratibu za jumuiya hiyo ikiwemo maandalizi ya katiba ya jukwaa hilo
kutaliwezesha jukwaa hilo kupanga, kuandaa na kutekeleza mikakati
mbalimbali ya kujiendesha ili kuwawezesha wanafunzi hao kutatua
changamoto zinazowakabili kwa kulinda heshima yao katika jamii.
Kwa upande wake mjumbe wa Bodi
ya Taaluma ya Chuo hicho Dkt. Ellen Oturu Okoedion amesema kuwa
wanafunzi wa kike wa chuo hicho wanahitaji msaada kupitia mfuko huo
utakaowawezesha kupambana na wimbi la wanafunzi wa kike kushindwa
kumaliza masomo yao kwa kushindwa kumudu gharama za masomo.
Amewataka wanafunzi wa kike wa
chuo hicho kutumia ipasavyo taaluma wanayoipata kusaidia mfuko huo
kupata fedha ili uwe endelevu kwa maendeleo ya wanawake na chuo hicho.
“Ninyi mnasoma elimu ya
biashara na ndio watalaam wenyewe sitarajii mfuko wenu ukose uwezo,
naamini mtatumia taaluma yenu mnayoipata hapa chuoni kutafuta fedha kwa
kuwa mnao uwezo huo” Amesisitiza Dkt. Ellen.
Naye Waziri wa Wanawake wa
Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) Bi. Mwajuma Sangali ameeleza kuwa
wanawake kote nchini wana jukumu la kuandaa kizazi cha watu wenye
upendo, uzalendo, kupenda kazi na maendeleo.
Amesema kuanzishwa kwa chombo hicho kunalenga kuboresha maisha ya wanawake hasa katika masuala ya elimu,jamii,uchumi na siasa.
No comments:
Post a Comment