Na Mwandishi Wetu, aliyekuwa Morogoro
WAKATI wananchi wakiendelea na zoezi la upigaji kura kuelekea Tamasha la Pasaka linalotarajia kuanza Aprili 20, uongozi wa Mkoa wa Morogoro umeeleza kwamba unapata mafanikio makubwa kupitia tamasha hilo, ikiwa pamoja na kukua kwa uchumi na biashara kushamiri katika mkoa huo.
Endapo Tamasha la Pasaka litafanyika mkoani Morogoro ni mara ya pili baada ya lile la Krismasi lililofanyika Desemba mwaka jana ambapo lilifana kwa kukusanya idadi kubwa ya wadau waliojitokeza kwa wingi katika uwanja wa Jamhuri uliopo mkoani humo.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro, Jorvis Simbeye ambaye alieleza baadhi ya faida zinazopatikana endapo Tamasha la Pasaka litafanyika mkoani humo.
Simbeye anasema moja ya faida hizo ni kuongezeka kwa uchumi na kutangaza utalii mkoani humo, kwa maana wafanyabiashara hasa upande wa chakula, nyumba za kulala wageni na mengine mengi.
Mkurugenzi huyo anaunga mkono uwepo wa tamasha hilo kufanyika Manispaa Morogoro hasa ukizingatia lina mlengo wa kusaidia jamii yenye uhitaji maalum.
Pia Mkurugenzi huyo alipoongeza kampuni ya Msama promotions kwa hatua yake hiyo ya kuandaa matamasha hayo kwa ajili ya kuisaidia jamii yenye uhitaji, huku akiwataka wengine kuiga mfano wake.
Kauli ya uongozi wa Uwanja wa Jamhuri
Uongozi wa uwanja wa Jamhuri kupitia Meneja wake, Herman Ndisa anasema kuwa tamasha hilo ni muhimu kwa wakazi wa Morogoro kwa kuwa wanapata ujumbe wa neno la Mungu kupitia waimbaji wanaowapenda.
“Tungependa tamasha lisikose mkoani kwetu kwa kweli Msama Promotions wanafanya kazi kubwa ya kukusanya waimbaji wakubwa,” alisema Ndisa.
Anasema tamasha hilo linakusanya idadi kubwa ya watu kutokana na waimbaji wanaofanya vizuri katika muziki wa Injili wanaoitwa na Msama, ambao ndio wamefanikiwa kwa kiasi kikubwa kuandaa matamasha makubwa katika mji wa Morogoro.
Anasema kuna waimbaji ambao wanasikika ambao wangependa na wao wawepo katika Tamasha la Pasaka la mwaka huu ni pamoja na Bahati Bukuku na Christina Shusho ambako anasema hilo ni jukumu lao waandaaji kuwaleta waimbaji wanaowataka.
Anasema zoezi la upigaji kura ni sahihi kwa kuwapa nafasi wanachi kuchagua waimbaji wanaowapenda lakini pia kamati ijaribu kuchagua waimbaji wa kupigiwa kura kwa nia ya kubadilisha waimbaji kila mwaka.
Ndisa anasema kuwa wapo waimbaji hata wasipobadilishwa ni sawa kwakuwa miaka yote wanamashabiki ambapo alitolea mfano kwa baadhi ya waimbaji kama Rose Mhando na Upendo Kilahiro ambaye nyimbo zake zinawabariki kiroho anapokuwa anaimba jukwaani.
“Tunapendezwa na waimbaji wa nyimbo za injili, kwa hiyo tungependa kila mwaka liwepo kwenye mkoa wetu kwa sababu linawasaidia wananchi kuishi katika imani na kujiepusha na anasa za kidunia,” alisema Ndisa.
Anasema kuwa licha ya kuwa Msama ni msaada mkubwa kwa jamii kupitia matamasha hayo, pia amekuwa msaada kwa baadhi ya waimbaji kwa kuendesha maisha yao kwa kipato anachowapatia.
Pia wafanyabiasha wanaouzunguka uwanja huo wamekuwa wakifanya biashara zao kwa mafanikio makubwa lilipofanyika Tamasha la Krismasi mwaka jana na anaamini kwamba hata kwa Pasaka litafana hali ambayo inakuza uchumi wa mkoa huo.
Uhakika wa usalama wakati wa Tamasha
Ndisa anasema Tamasha la Pasaka ni tamasha la kidini lina usalama wa kutosha, uongozi kwa kushirikiana na jeshi la Polisi umekuwa ukijipanga vilivyo kuhakikisha usalama wa kutosha na utulivu ambako pia watu wanapata kile walichokifuata.
“Usalama upo wa kutosha kwa sababu hakuna ulevi tunawapekuwa watu tunaowatilia shaka kuwa ni walevi au wanataka kuingia na pombe, tunawatoa nje,” alisema Ndisa.
No comments:
Post a Comment