INAWEZEKANA baada ya dakika 90 za mtanange wa kesho baina ya Young Africans dhidi ya Azam fc, Uwanja wa Taifa, jijini Dar es salaam, picha ya timu gani inaweza kupewa nafasi ya kutwaa ubingwa wa ligi kuu soka Tanzania bara msimu wa 2013/2014 ikafahamika.
Mchezo wa kesho umevuta hisia za mashabiki wengi na kuwafanya makocha wa timu zote, Joseph Marius Omog wa Azam fc na Hans Van Der Pluijm wa Yanga kutuliza akili zao kwa lengo la kupata ushindi mechi ya kesho.
Kitendawili kinachosubiriwa kuteguliwa ni je, Azam fc watawafunga Yanga kwa mara ya pili msimu huu katika mechi za ligi kuu?.
Ikumbukwe septemba 22 mwaka jana, timu hizi zilikutana katika mchezo wa ligi kuu na Wana Lambalamba kuibuka na ushindi wa mabao 3-2.
Lakini kabla ya mechi hiyo, Yanga waliwafunga bao 1-0 Azam fc katika mchezo wa Ngao ya jamii kuashiria kufunguliwa kwa pazia la ligi kuu soka Tanzania bara msimu 2013/2014.
Mechi zilizopita, Yanga walitoka suluhu dhidi ya Mtibwa uwanja wa Jamhuri, wakati Azam fc walishinda mabao 4-0 dhidi ya Coastal Union.
Azam fc wapo kileleni wakijikusanyia pointi 43 katika mechi 19 walizocheza, wakati Yanga wameshuka dimbani mara 18 na kujikusanyia mzigo wa pointi 39 katika nafasi ya pili.
Mtandao huu ulipata nafasi ya kuzungumza na kocha wa zamani wa Yanga, Kennedy Mwaisabula `Mzazi` , lengo likiwa ni kujua mtazamo wake kuelekea mechi ya kesho.
Katika mahojiano hayo maalumu, Mwaisabula alianza kwa kusema mchezo wa kesho utakuwa mgumu kwa Yanga, kwasababu wameathiriwa na matokeo ya mechi iliyopita dhidi ya Mtibwa Sugar, uwanja wa Jamhuri mkoani Morogoro.
“ Kutoka suluhu na Mtibwa kutawafanya wacheze kwa nguvu kutafuta matokeo ya ushindi. Hawatakubali kufungwa au kutoka sare kwani wakipata matokeo hayo, kutawafanya wapunguze hadhi yao ya kutetea ubingwa wao”.
No comments:
Post a Comment