Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu. mchimati@gmail.com au
Wenyeviti wa vyama vya upinzani nchini, kutoka kushoto ni James Mbatia (NCCR-Mageuzi), Freeman Mbowe (Chadema) na Profesa Ibrahim Lipumba (CUF).
Dodoma.
Wenyeviti
wa vyama vya Upinzani vya Chadema, Chama cha Wananchi (CUF) na Chama
cha NCCR-Mageuzi, jana usiku walikutana ili kutoa kauli ya pamoja,
kutokana na hotuba ya ufunguzi wa Bunge kwa maelezo kuwa tayari Rais
amevuruga mchakato mzima wa kupata Katiba Mpya.
Wakati
viongozi hao wakikutana, Mwenyekiti wa Chama cha DP Mchungaji,
Christopher Mtikila alisema, Rais ameingilia mchakato na kutoa maelezo
jinsi ya kuandika Katiba.
Wakizungumza
na wanahabari wa Full Utamu mara baada ya hotuba hiyo, Freeman Mbowe, James
Mbatia na Profesa Ibrahim Lipumba, walisema wameipokea kwa masikitiko
makubwa hotuba hiyo.
“Tunakwenda kujadili hotuba ya Rais na tutatoa msimamo wetu,” alisema Mbowe.
Awali
Katibu wa muda wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Julius Mtatiro
alisema Rais Jakaya Kikwete amevuruga mchakato wa Katiba, kwani
walitarajia angetumia mamlaka yake kama Rais kuwaunganisha.
“Rais
tulitarajia angeongea kama mkuu wa nchi, lakini amezungumza kama
Mwenyekiti wa CCM na kutoa msimamo juu ya muundo wa Muungano jambo
ambalo hatukulitegemea,” alisema Mtatiro.
Alisema kwa Rais kutoa msimamo ni sawa na mwongozo jambo ambalo limevuruga mchakato mzima.
Hofu ya kuvunjika Bunge
Wakizungumza nje ya Bunge, baadhi ya wajumbe wameeleza kuwa hotuba ya
Rais Kikwete kama ikitekelezwa uwezekano wa kupata Katiba Mpya utakuwa
mgumu.
Mjumbe
Luhaga Mpina alisema kwa jinsi rasimu ilivyoandikiwa na kama muundo wa
serikali mbili ukipita basi rasimu ya Katiba itabidi iandikwe upya.
“Rasimu yote imetengenezwa kwa mfumo wa serikali tatu sasa hapa kuna hatari ya Bunge kukwama ,” alisema.
Mtatiro
kwa upande wake alisema sasa kuna hofu ya kushindwa kupatikana Katiba
Mpya kwani Rais amewachanganya wajumbe na kama watapitisha maoni yake
itabidi rasimu kuandikwa upya.
Mjumbe Mustapha Akoonay, alisema upatikanaji wa katiba upo shakani kwani sasa upinzani utakuwa mkubwa juu ya muundo wa muungano.
“Kwa sasa nadhani itabidi turudi upya kwa wananchi kupata kura ya maoni juu ya muundo wa muungano,” alisema.
Lucy
Owenya alisema Rais amegeuza mkutano wa Bunge kuwa ni mkutano wa Chama
Cha Mapinduzi, kwani ameshindwa kabisa kutoa mwelekeo wa nchi na badala
yake ametoa msimamo wa CCM.
“Kutokana
na hili, naamini kabisa Bunge halitakuwapo na ni bora iwe hivyo kwa
kuwa amejibu hotuba ya Warioba na kwa maana hiyo amepingana na mawazo ya
wananchi.”
Godbles Lema alisema kuwa Rais hakuja kuhutubia taifa bali alikuja kufanya semina na kujibu hotuba ya Warioba.
Mjumbe
huyo ambaye ni mbunge wa Arusha Mjini alionyesha shaka kuwa baada ya
muda wa wiki tatu hakutakuwa na Bunge la Katiba kwa kuwa wako baadhi ya
watu ambao hawatakubali kilichofanywa na Rais Kikwete.
“Waliochukua
fedha ni vyema wakaenda kumalizia nyumba zao kwa kuwa kiongozi wetu
amefanikiwa kwa kiasi kikubwa kuwafurahisha wanaCCM lakini kwa
Watanzania hatutakubali,” alisema Lema.
John
Cheyo alisema, “Mimi ninachokiona ni maridhiano tu, suala la kufumua
rasimu halinipi shida kwa kuwa vitu vyote vinavyoletwa bungeni huwa ni
mali ya Bunge na hivyo tutafanya tunavyoona sisi inafaa.”
Mchungaji
Peter Msigwa, alisema kuwa kosa kubwa ambalo lilifanywa na upinzani ni
kukubali na kuruhusu Jaji Warioba atangulie kuwasilisha rasimu yake
akasema hilo ndilo lililowagharimu.
Alitaka
Bunge livunjwe mara moja ili warudi kwa wananchi wakaamue na kuwahukumu
kutokana na kile ambacho walikifanya katika Bunge ambalo kwa maoni yake
wamekula fedha za walipa kodi bure.
Naye Waziri Mkuu Mstaafu, Edward Lowassa aliipongeza hutuba ya Rais Jakaya Kikwete ya uzinduzi wa Bunge la Katiba.
Lowassa
ambaye pia ni Mjumbe wa Bunge la Katiba, alisema kwa kifupi hotuba ya
Rais Kikwete ni nzuri. Lowassa alitoa kauli hiyo, wakati akitoka nje ya
Bunge, muda mfupi baada ya Rais Jakaya Kikwete kumaliza hotuba ya
uzinduzi wa Bunge hilo.
Naye Mjumbe wa Bunge Maalumu la Katiba, Mchungaji Ernest Kadiva, alisema hotuba ya Rais imetoa mwanga kwa wajumbe.
“Rais
ameonyesha upungufu wa hoja mbalimbali hasa katika mfumo wa serikali
tatu na sasa ameacha kazi ya kuamua tuwe na mfumo wa serikali mbili au
tatu ni ya wajumbe,” alisema Mchungaji Kadiva.
Hata
hivyo, mjumbe mmoja ambaye hakupenda kutaja jina lake alisema Rais
alizungumza kama si mkuu wa nchi bali Mwenyekiti wa CCM kwa sababu
amesimamia hoja za chama chake.
Alisema
hata kama mapendekezo ya Rais Kikwete yatatekelezwa, kamwe hayatakuwa
mwarobaini wa muungano. Mbunge wa Mwibara, Khangi Lugora alisema hotuba
hiyo waliitarajia na ndio maana kulikuwa na ubishi wa nani atangulie
kati ya Jaji Joseph Warioba na yeye kwa mujibu wa kanuni.
“Hotuba
ilikuwa ikijaribu kumjibu Jaji Warioba na kwangu mimi nilikuwa naona
kuwa Rais naye alikuwa anachangia katika kuitunga Katiba kwa kupitia
hotuba yake hiyo. Tumeyasikia na sisi tutakwenda kutafakari katika
kutunga Katiba ambayo itakuwa ya Watanzania wote,” alisema.
Kwa
upande wake Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema) Mkiwa Kimwanga, alisema
kilichofanyika ni Rais kwenda kutoa uamuzi juu ya mchakato uliokuwa
ufanywe na Bunge hilo.
Kwa
upande wake, Profesa Ibrahim Lipumba, alisema hakuitendea haki Tume ya
Mabadiliko ya Katiba na kwamba Bunge hilo haliwezi kutengeneza Katiba
ambayo inalenga katika mfumo wa serikali la mbili.
“Itakuwa
ni vigumu zaidi kupata Katiba Mpya, alikuwa anapinga mambo ya msingi
yaliyoelezwa katika rasimu ya kwanza. Hayo angeyaeleza katika hatua ya
awali ili rasimu hiyo ibadilishwe na si katika hatua hii ya mwisho kabla
ya kwenda kupigiwa kura na wananchi,” alisema.
Alisema
ndani ya siku 70 haiwezekani kubadili rasimu hiyo ambayo imejikita
katika muundo wa serikali tatu kwenda katika muundo wa serikali mbili.
Ezekiah Olouch alitahadharisha wajumbe wenzake kutodharau maoni ya wananchi waliyoyatoa katika rasimu hiyo ya pili.
Alisema
haiwezekani tume zote ambazo zimeundwa kuangalia aina ya muundo wa
serikali zije na jibu moja kuwa namna ya kuimarisha muungano ni kuwapo
kwa serikali tatu.
Jussa Ismail Ladu alisema kwa ufupi kwamba hotuba ya Rais Kikwete imekuwa yenye sura ya CCM zaidi.
Naye
Mbunge wa Lulindi, Jerome Bwanausi, aliielezea hotuba ya Rais kuwa
imeibua mambo mengi ambayo baadhi ya watu walikuwa wakiyaelewa tofauti,
hivyo imeweka uelewa mzuri katika baadhi ya maeneo.
Profesa Costa Mahalu alisema ni hotuba ambayo imewaachia changamoto,
hasa katika eneo la muungano kwa sababu wanahitajika kuunda muungano
usiotetereka.
Chanzo: Mwananchi.
No comments:
Post a Comment