on MARCH 17, 2014 in BURUDANI
Na Mwandishi Wetu
MUIMBAJI wa muziki wa Injili raia wa Zambia, Ephraim Sekeleti naye amepata nafasi ya kushiriki kwenye tamasha la Pasaka linalotarajia kuanza Aprili 20 jijini Dar es Salaam.
Sekeleti ni mmoja wa waimbaji wa muda mrefu katika tamasha hilo amekubali kushiriki kwa sababu ana kiu ya kufikisha ujumbe wake kwa Watanzania.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Msama Promotions ambao ni waandaaji wa tamasha hilo, Alex Msama taratibu za kuwapata waimbaji mbalimbali watakaoshiriki katika tamasha hilo linaendelea.
Msama alisema muimbaji raia wa Kidemokrasia ya Kongo, Faraja Ntaboba naye pia amechomoza kushiriki tamasha hilo ili kufikisha ujumbe wa Neno la Mungu.
Rebecca Malope ni miongoni mwa wasanii kutoka nje ya Tanzania watakaotumbuiza kwenye Tamasha la Pasaka mwaka huu ambaye naye amethibitisha kuwepo kwenye tamasha hilo.
Waimbaji wengine watakaotumbuiza kwenye tamasha hilo ambao tayari wameshathibitisha ni Upendo Nkone, John Lissu, Upendo Kilahiro, Rose Muhando na kwaya ya Kwetu Pazuri wote wa Tanzania.
Aidha Msama alifafanua kuwa tamasha hilo linatarajia kuanza Aprili 20 jijini Dar es Salaam wakati siku inayofuata litafanyika mkoani Morogoro huku mikoa mingine ikiendelea kupigiwa kura.
No comments:
Post a Comment