
Na Mwandishi wetu
KAMANDA
wa meli ya kivita ya Ujerumani FGS Lübeck, inayofanya doria katika
ukanda wa Bahari ya Hindi kama sehemu ya jeshi la kimataifa
linaloendesha operesheni Atalanta, Peter Christian Semrau, amesema
jumuiya ya kimataifa imepata mafanikio makubwa kwa kuwezesha njia
inayotumika sana na meli kuwa salama.
Akizungumza
katika mahojiano ndani ya meli hiyo ambayo imetia nanga katika bandari
ya Dar es Salaam, Kamanda Semrau alisema kwamba kwa mwaka huu hapakuwepo
na tukio kubwa ambalo limetikisa eneo hilo la Pwani ya Pembe ya Afrika
inayopakana na Somalia na Yemen.
Alisema
kuanzia shughuli za kimataifa kukabili uharamia na ujambazi baharini
kuanza mwaka 2009 kumekuwepo na ushindi wa kimataifa kutokana na
kuendelea kupungua kwa matukio katika eneo hilo ambapo awali ilikuwa ni
tishio kubwa.
Alisema
pamoja na kupungua kwa matukio ya kijambazi na utekaji nyara kazi
ambayo inatarajiwa kufanywa mwakani ni kuhakikisha kwamba mataifa
yanayopakana na bahari ya Hindi yanawezeshwa kujilinda yenyewe dhidi ya
matukio ya baharini.

Meli
hiyo ambayo inafanya doria kuanzia kaskazini mwa Afrika hadi Kusini
imetia nanga Dar es salaam ikitokea Madagascar ambako nako ilipata
mapokezi makubwa.
Operesheni
Atalanta inaendeshwa na vikosi vya Umoja wa Ulaya vikilinda eneo la
bahari ambalo lina shughuli nzito kwa meli za biashara
Meli hiyo ambayo itakuwa katika operesheni hadi februari mwakani itapokewa kazi hiyo na meli nyingine ya FGS Bayern.
Naye
Balozi wa Ujerumani nchini Mh. Egon Kochanke akizungumza na waandishi wa
habari akiwakaribisha katika melivita hiyo alisema kwamba amefurahishwa
na mchango wa taifa lake katika kuhakikisha pwani ya Bahari ya Hindi
upande wa Afrika inakua salama na watu wanapata huduma zinazotakiwa.

Alisema
pamoja na meli hiyo kutia nanga Dar es Salaam kuonesha ushirikiano wa
kutosha kati ya taifa lake na Tanzania, anatarajia mwakani mahusiano ya
Tanzania na Ujerumani yatazidi kuimarika hasa katika nyanza za hifadhi
na maendeleo ya jamii.
Aidha
balozi huyo alisema kwamba taifa lake linaongeza fedha zaidi kwa ajili
ya uanzishaji wa mamlaka ya wanyamapori nchini Tanzania kwa lengo la
kuifanya iwe na nguvu na uwezo wa kulinda wanyama hao.
Pia
alisema inafikiria namna ya kufanya na meli ya MV Liemba ambayo alisema
ni moja ya vielelezo hai vilivyopo vyenye maana kubwa katika uhusiano wa
Tanzania na Ujerumani.
Aidha
alisifu ukuaji wa demokrasia nchini Tanzania hasa kwa kuzingatia uhuru
uliopo wa vyombo vya habari na majadiliano yenye afya bungeni yenye
lengo la kujenga taifa lenye nguvu.
Aidha
alisema Ujerumani itaendelea kukuza uhusiano na Tanzania ambayo ni
nanga ya usalama kwa mataifa ya Afrika Mashariki na ukanda wa Bahari ya
Hindi kwa upande wa Afrika.






Mkurugenzi
Mtendaji wa kampuni ya CFAO Motors, Bw.Wayne McIntosh akihoji jambo kwa
mmoja wa wanakikosi cha maji wa meli ya kivita ya ya Ujerumani FGS
Lübeck ambaye jina lake halikuweza kufahamika kiurahisi.



Afisa
wa kitengo cha habari Ubalozi wa Ujerumani nchini Tanzania, John
Meirikion akipata picha ya pamoja na mmoja wa wageni waalikwa ndani ya
meli ya kivita ya Ujerumani FGS Lübeck iliyotia nanga bandari ya Dar es
Salaam.
No comments:
Post a Comment