NA MWANDISHI WETU
KAMPUNI ya Msama Promotions ya jijini
Dar es Salaam, imeomba rasmi kibali cha kufanya tamasha la Pasaka
mwaka 2012, litakalofanyika Aprili 8, mwaka huu katika mikoa mbalimbali
nchini.
Akizungumza
na Dira ya Mtanzania jana jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Kamati
ya Maandalizi ya Tamasha la Pasaka, Alex Msama, alisema tayari
wamepeleka maombi BASATA ili waweze kupata kibali cha kuendesha tamasha
la mwaka huu.
“Tumepeleka maombi yetu ya kuandaa tamasha la Pasaka mwaka huu, tunategemea BASATA watatusikiliza na kutupatia kibali,” alisema.
Msama alisema tamasha la mwaka huu litapambwa na waimbaji wengi wa kimataifa, wakiwemo nyota wa muziki wa injili nchini.
Alisema katika tamasha hilo, kamati yake itakutana kupanga sehemu litakalopofanyika tamasha hilo kwa mwaka huu.
“Miaka yote
tumezoea tamasha kufanyika ukumbi wa Diamond Jubilee, lakini mwaka huu
kazi ya kutafuta sehemu kubwa ya kuweza kushuhudiwa na waumini wengi wa
dini ya kikristo, tumeiachia kamati, ikikamilisha tutatangaza,”
alisema.
Pamoja
na kusema kuwa, tamasha hilo litafanyika mikoa mbalimbali nchini,
Msama alishindwa kuitaja na kusema kuwa, itatangazwa baada ya kamati
yake kuichagua.
Mwenyekiti huyo wa kamati ya maandalizi ya Pasaka, alisema kuwa, mgeni rasmi katika tamasha hilo atatangazwa hapo baadaye.
“Suala la mgeni rasmi naomba kwa sasa mliache, linafanyiwa kazi, mambo yakikamilika, tutamweka hadharani,” alisema.
Msama alisema kuwa, mwaka jana mgeni rasmi katika tamasha hilo alikuwa, Rais Jakaya Mrisho Kikwete.
No comments:
Post a Comment