Na Nyakongo Manyama-Maelezo
Jumla ya watahiniwa 813 ambao ni sawa na asilimia 14.3 wamefaulu mitihani ya Bodi ya Taifa ya Wasahibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania (NBAA) na uliofanyika Novemba 2015 kote nchini.
Katika matokeo hayo, wahitimu wengine 1867 ambao ni sawa na asilimia 32.9 wamefaulu baadhi ya masomo katika ngazi mbalimbali kati ya watahiniwa 6404 waliosajiliwa katika mitihani iliyofanyika novemba mwaka huu.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mtendaji Bodi NBAA Bw. Pius Maneno katika kikao cha wakurugenzi wa bodi hiyo kilichokaa kuidhinisha matokeo hayo leo jijini Dar es salaam.
Bw. Pius amesema kuwa jumla ya watahiniwa 725 ambao ni sawa na asilimia 11.3 walishindwa kufanya mitihani kutokana na sababu mbalimbali hivyo kufanya jumla ya watahiniwa waliofanya mitihani hiyo kuwa 5,679 ambayo ni sawa na asilimia 88.7.
“Kati ya watahiniwa waliofanya mitihani hiyo, watahiniwa 236 ambao ni sawa na asilimia 4.2 wamefaulu mitihani katika mkao mmoja na wengine 258 sawa na asilimia 4.5 wamefaulu kwa kufaulu masomo waliyokuwa wameshindwa katika miaka ya nyuma na wengine 319 sawa na asilimia 5.6 wamefaulu katika masomo waliyokuwa wamebakiza” alisema Bw. Pius.
Aidha, Bw. Pius aliongeza kuwa katika mitihani ya Novemba 2014 na ya Novemba 2015 kiwango cha ufaulu kimeshuka kutoka asilimia 53.1 hadi kufikia asilimia 47.2 ikiwa ni pungufu ya asilimia 5.9 pia kuna upungufu wa watahiniwa 107 sawa na asilimia 1.8.
Bw. Pius aliwapongeza watahiniwa waliofuzu na kuwataka ambao hawajafuzu kutokata tamaa bali waongeze juhudi zaidi katika masomo yao ili waweze kufanya vizuri katika mitihani ijayo ya bodi.
Mitihani ya bodi ya Taifa ya wasahibu na wakaguzi wa hesabu Tanzania ni ya tatu chini ya mfumo mpya a elimu na mafunzo unaozingatia weledi ambayo ilifanyika katika vituo 11 vya mitihani vilivyopo Tanzania Bara na Visiwani na ilihusisha watahiniwa katika hatua ya kwanza na ya pili katika ngazi ya Cheti cha Utunzaji wa Hesabu, hatua ya awali, kati na hatua ya mwisho.
No comments:
Post a Comment