Mwanahabari wa Ufaransa amezuiwa kuendelea kufanya kazi nchini Uchina wiki chache baada yake kuandika makala akikosoa sera za taifa hilo kuhusu watu wa jamii ya Uighers eneo la Xinjiang.
Wengi wa watu wa jamii hiyo ni Waislamu.
Beijing imethibitisha kwamba haitafanya upya kibali cha kufanyia kazi ya uabahabari cha Ursula Gauthier, anayefanyia kazi jarida la Ufaransa la L'Obs.
Taifa hilo limesema makala yake kuhusu machafuko Xinjiang iliunga mkono "ugaidi na vitendo vya ukatili” vilivyosababisha vifo vya watu wengi.
Bi Gauthier anasema madai hayo ni ya kushangaza na amesema Uchina inajaribu kuzuia wanahabari kutoka nchi za nje kufanya kazi huko.
Muda wa kuendelea kuhudumu kama mwanahabari Uchina usipoongezwa, Bi Gauthier hataweza kupata visa mpya na atalazimika kuondoka Uchina ifikapo 31 Desemba.
Atakuwa mwanahabari wa kwanza wa kigeni kutimuliwa nchini humo tangu kufurushwa kwa mwanahabari wa Al Jazeera Melissa Chan mwaka 2012.
Uchina imekuwa ikilaumu wanaharakati wa Kiislamu wanaotaka kujitenga kwa Xinjiang kwa machafuko ya muda mrefu yanayotokea eneo hilo, na inasema baadhi hata wana uhusiano na mataifa ya nje.
Lakini watu wa jamii ya Uighurs wanasema sheria kali za Uchina za kukandamiza uhuru wa kidini na kitamaduni ndizo zinazochochea machafuko.
Bi Gauthier, kwenye makala yake baada ya mashambulio ya Paris mwezi Novemba, alikuwa amedokeza kwamba huenda Uchina ikatumia mashambulio hayo kukabiliana zaidi na makundi yanayotaka kujitenga Xinjiang.
No comments:
Post a Comment