IS yatishia kuishambulia Israel kwa mara ya kwanza
Kiongozi wa kundi la kigaidi lijiitalo Dola la Kiislamu (IS), Abu Bakr al-Baghdadi, ametishia kuishambulia Israel, kupitia mkanda wa sauti uliotolewa jana. Katika kitisho cha nadra kwa taifa hilo la Kiyahudi, al-Baghdadi anasikika kwenye mkanda huo akisema kundi lake halijaisahau Palestina, huku akiapa kuigeuza ardhi hiyo kuwa makaburi ya Mayahudi. Ujumbe huo wa kwanza kutolewa na al-Baghadadi ndani ya kipindi cha miezi saba, unazitaja pia Marekani, Urusi na Ulaya kuwa walengwa wa mipango ya mashambulizi hayo. Bado rikodi ya mkanda huo haijathibitishwa na vyanzo huru. Kundi la Dola la Kiislamu, ambalo linatawala sehemu kubwa ya Syria na Iraq, limedai kuhusika na mashambulizi kadhaa ya kigaidi ulimwenguni, katika kampeni yake ya kijeshi iliyosambaa katika mataifa mbalimbali mnamo miezi ya hivi karibuni.
No comments:
Post a Comment