Umoja wa Mataifa waitisha mazungumzo ya amani ya Syria
Duru mpya ya mazungumzo ya kusaka amani ya Syria itafanyika tarehe 25 Januari, kwa mujibu wa mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa kwa mzozo huo, Staffan de Mistura. Taarifa iliyotolewa jana na Umoja wa Mataifa inasema mpatanishi huyo anatarajia ushirikiano kutoka kwa pande zote husika, ikimnukuu kuwa "watu wa Syria wameshateseka vya kutosha." Alhamisi iliyopita, Waziri wa Mambo ya Nje wa Syria, Walid al-Moallem, alisema mjini Beijing, China, kwamba serikali yake ilikuwa tayari kushiriki mazungumzo hayo yanayosimamiwa na Umoja wa Mataifa, lakini "bila ya uingiliaji wa mataifa ya kigeni." Zaidi ya nusu ya raia wa Syria milioni 22 na nusu waliokuwepo kabla ya vita wamelazimika kuyakimbia makaazi yao. Mapema mwezi huu, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilipitisha azimio linaloidhinisha mchakato wa amani unaosimamiwa na Umoja huo kuanzia mwezi Januari. Chini ya mpango huo, Syria inapaswa kuwa na serikali ya mpito ndani ya kipindi cha miezi sita ijayo na uchaguzi mpya ndani ya kipindi cha miezi 18 baada ya serikali hiyo kuundwa.
No comments:
Post a Comment