Maelfu ya waasi ambao walitarajiwa kusaidiwa kuondoka kutoka kambi ya wakimbizi ya Yarmouk na maeneo ya karibu hawakuondoka kama ilivyotarajiwa, ripoti zinasema.
Mpango huo umekawishwa kutokana na hofu za kiusalama na mauaji ya kiongozi wa kundi moja la waasi jana.
Wapiganaji hao na familia zao walikuwa wamepangiwa kusafirishwa kutoka kambi hiyo kusini mwa Damascus hadi maeneo yanayodhibitiwa na makundi yao, chini ya mkataba kati ya serikali na waasi.
Takriban raia 18,000 wamekwama Yarmouk kutokana na mapigano na kuzingirwa na vikosi vya serikali tangu 2012.
Wapiganaji wa Islamic State (IS) walitwaa udhibiti wa baadhi ya maeneo ya kambi hiyo mapema mwaka huu.
Lakini walifurushwa na wapiganaji wa Kipalestina na wapiganaji wengine wa Syria baada ya mapigano makali.
Tangu wakati huo, kambi ya Yarmouk imekuwa imegawanywa kwa maeneo yanayodhibitiwa na IS, kundi la al-Nusra Front lenye uhusiano na al-Qaeda na wapiganaji wa Kipalestina wanaounga mkono na wanaopinga serikali.
Wanajeshi wa serikali wameweka vizuizi kuzingira eneo hilo na huzuia raia kuondoka.
Chini ya makubaliano ya sasa, wapiganaji hao walitarajiwa kuruhusiwa kuondoka Yarmouk na maeneo jirani ya Hajar al-Aswad na al-Qadam.
Mabasi 18 tayari yalikuwa yamewasili eneo hilo Ijumaa kuwasafirisha.
Runinga ya kundi la Hezbollah la Lebanon kwa jina al-Manar imesema mpango wa kuwahamisha umeahirishwa kwa sababu msafara wao ungepitia maeneo yanayodhibitiwa na kundi la Jaysh al-Islam, ambalo kongozi wake aliuawa baadaye Ijumaa.
Kambi ya wakimbizi ya Yarmouk ilijengwa kwa ajili ya Wapalestina waliokuwa wakitoroka vita vya Waarabu na Waisraeli vya 1948. Kabla ya vita kuanza Syria 2011, ilikuwa na wakimbizi 150,000.
No comments:
Post a Comment