ASKOFU
na Nabii George David ‘Geordavie’ wa Kanisa la Geordavie Ministry
‘Ngurumo ya Upako’ lililoko jijini Arusha na Kawe, Dar hivi karibuni
alifanya mkutano mkubwa na kutikisa nchi kwa kuwa na magari ya kifahari
na ndege aina ya helikopta ‘chopa’ iliyokuwa ikirandaranda juu ya anga
kulinda usalama wake, Uwazi lina ushuhuda wa kutosha.
Katika
mkutano huo uliofanyika Karatu mkoani Manyara, mwandishi wetu
alishuhudia msafara wa Geordavie ambaye hutoa huduma ya uponyaji kwa
njia za miujiza, ukiwavutia watu wengi kwa kuwa ulikuwa na ulinzi mkali
ambao haujawahi kutokea.
Mbali
ya kuwa na chopa iliyokuwa ikiimarisha ulinzi ambayo ameinunua hivi
karibuni, askofu huyo alikuwa na msururu wa magari yenye thamani kubwa
yanayomfanya kutajwa kuwa tajiri kuliko maaskofu wengine wanatoa huduma
katika makanisa ya kiroho Tanzania.
Akiwa
Karatu, mbali na ulinzi binafsi, Geordavie alikuwa akilindwa na askari
wa jeshi la polisi, askari kanzu, Askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia
(FFU) na wale wa usalama barabarani.
Mbali
na askari hao wa serikali ambao wamekuwa wakimlinda kila anapofanya
mikutano yake, pia Geordavie analindwa na askari wake binafsi hali
iliyowafanya baadhi ya watu kuamini kuwa ulinzi wake ni kama ule wa Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete ‘JK’.
“Sijawahi
kumuona JK akilindwa na chopa lakini mtumishi wa Mungu Geordavie
analindwa na ndege katika msafara wake! Hii ni mara yangu ya kwanza
kuona,” alisema muumini mmoja ambaye hakupenda kutajwa gazetini.
Hata
hivyo, baadhi ya watu walikuwa wakihoji utajiri wa askofu huyo kutokana
na fedha nyingi anazozitumia anapofanya mikutano katika sehemu
mbalimbali jijini Arusha.
“Tunajua
kuwa ni tajiri, lakini anapata wapi fedha za kutumia hivi?” alihoji
muumini aliyejitambulisha kwa jina moja la Julius ambaye naye
alihudhuria mkutano wa askofu huyo anayetumia kaulimbiu ya Ngurumo ya
Upako katika kutoa huduma yake.
Pia,
waumini wengine walilalamikia ugumu wanaoupata wanapotaka kumuona
mtumishi huyo wa Mungu kutokana na ulinzi mkali anaopewa.
“Kila
mtu alitamani kumuona mtumishi wa Mungu lakini haikuwezekana kutokana
na ulinzi wake kuwa mkali, utajiri wake hakuna mfano, hata kule nyumbani
kwake Arusha, anaishi kama Mfalme Daud,” alisema Fred Mushi.
Gazeti
hili lilimsaka Askofu na Nabii Geordavie kwa lengo la kutaka kujua
sababu ya kuwa na ulinzi mkali na kutumia magari ya kifahari ikiwemo
chopa katika mikutano anayoifanya lakini simu yake iliita bila
kupokelewa.
No comments:
Post a Comment