Jana tarehe 29 Julai, 2014 nimefanya mahojiano katika kipindi cha
PowerBreakFast kinachorushwa na Clouds FM. Baadhi ya vyombo vya habari
vimeandika mahojiano yale. Napenda nitoe ufafanuzi kidogo kuhusu msimamo
wangu kuhusu mchakato wa Katiba.Kwanza, Mimi sijawahi kuwa UKAWA wala
kundi lolote lile katika Bunge Maalumu la Katiba isipokuwa kundi
linalotaka maridhiano. Msimamo wangu kuhusu Muungano ni Serikali Tatu
Zilizoboreshwa (S3z) ili kuwa na Muungano imara usio tegemezi wala
egemezi kwa Washirika wake. Pili, Mimi niliunga mkono ‘protest’ ya
baadhi ya Wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba kupinga lugha za matusi na
lugha za kibaguzi zilizokuwa zinaendelea ndani ya mkutano ule. Vilevile
niliunga mkono kwamba Rasimu inayopaswa kujadiliwa ni Rasimu iliyotokana
na Tume ya Marekebisho ya Katiba iliyoongozwa na Jaji Joseph Sinde
Warioba.
Nasisitiza umuhimu wa kupata Katiba BORA itakayoimarisha DOLA ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Tatu,
kwa hali ya sasa kuna mkwamo katika kupatikana kwa Katiba Bora. Mkwamo
unaotokana na kutokuwepo kwa nia ya dhati ya kupata maridhiano ya pande
zinazopingana. UKAWA hawataki mazungumzo na Viongozi wa Bunge la Katiba
badala ya kujenga maridhiano kila siku wanawabeza UKAWA jambo ambalo
kamwe haliwezi kujenga mwafaka.Ushauri wangu ni kuahirisha
mchakato mzima wa kuandika Katiba mpaka mwaka 2016 baada ya Uchaguzi
Mkuu wa mwaka 2015. Katiba ya sasa ifanyiwe marekebisho machache kama
ifuatavyo;
i) Tume
ya Uchaguzi ili iwe huru na ionekane kuwa huru, ikiwemo kuwaondoa
watumishi wa Halmashauri za Wilaya, Miji na Majiji katika kusimamia
uchaguzi
ii) Kuruhusu mgombea binafsi
iii) Kuondoa Mafuta na Gesi kama Jambo la Muungano ili Zanzibar ianze
mara moja kusimamia kwa uhuru utafutaji wa Mafuta katika vitalu
vilivyopo upande huo wa Muungano
Mkutano wa Bunge Maalumu utakaofanyika bila kuwepo kwa maridhiano
utakuwa hauna maana yeyote na itakuwa ni sawa na kupoteza muda na fedha
za walipa kodi ambazo zingeweza kununua madawa vijijini.
No comments:
Post a Comment