*Awaasa wananchi wasikubali kugeuzwa mtaji na wagombea
WAZIRI
MKUU Mizengo Pinda amewaonya Watanzania kuwa makini na watu wanaotumia rushwa
ili kupata nafasi za uongozi na hasa kwenye uchaguzi mkuu unaotarajiwa
kufanyika Oktoba, 2015.
Ametoa onyo
hilo leo mchana (Jumapili, Julai 27, 2014) wakati akizungumza na mamia ya
waumini na viongozi mbalimbali waliohudhuria ibada ya uzinduzi wa dayosisi mpya
ya Ruvuma ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) na kuwekwa wakfu Askofu
Amon Mwenda aliyeteuliwa kuongoza dayosisi hiyo.
“Ninawasihi
wananchi wawe makini na viongozi wanaopenda kutoa rushwa hasa katika kipindi
hiki cha kuelekea kwenye uchaguzi mkuu. Kama mtu ana nia ya kweli ya kuongoza
ni kwa nini atumie fedha ili kupata nafasi ya uongozi?,” alihoji.
“Tatizo ni
kwamba hata wananchi hivi sasa wanakubali kupokea kile kinachotolewa na
wagombea. Atakuja huyu atakupa hiki na mwingine naye atakupa kile, lakini ujue
akiingia madarakani anaanza kurudisha haraka vile alivyowagawia,” alisema.
Aliwaonya
wananchi kuwa makini ili wasije wakageuzwa mtaji wa kuwanufaisha watu binafsi. “Tukikubali
kutumika ni sawa tutapata viongozi wakati wa uchaguzi, lakini watakuwa ni wale
wasio na hofu ya Mungu, wenye kujali maslahi yao kuliko ya wananchi
waliowachagua,” aliongeza.
Aliwaomba
viongozi wote wa dini waliohudhuria sherehe hizo pamoja na waumini wote
waendelee kuliombea Taifa ili Mungu aliepushe na janga hilo la watu kupenda rushwa.
Alitumia fursa hiyo pia kuwaomba wazidi kuuombea mchakato wa kupata Katiba mpya
ili wabunge wote warejee ndani ya Bunge na kuikamilisha kazi waliyoianza.
Alimuomba
Askofu huyo mpya apokee jukumu hilo kwa mikono miwili na kumuahidi kuwa kama
Serikali watakuwa naye bega kwa bega kuwaongoza Watanzania walioko kwenye
dayosisi yake. Dayosisi hiyo mpya inahusisha mkoa wote wa Ruvuma na wilaya ya
Ludewa eneo ambalo lina ukubwa wa kilometa za mraba 72,630. Kati ya hizo km. za
mraba 64,233 ni za mkoa wa Ruvuma na km. za mraba 8,397 ni za wilaya ya Ludewa.
Mapema, akitoa hotuba yake ya kwanza mara
baada ya kusimikwa rasmi, Askofu Mwenda alisema dayosisi mpya ya Ruvuma
imezaliwa katika kipindi chenye changamoto nyingi za kidunia na utandawazi
ukiwemo mmomonyoko mkubwa wa maadili.
Hata hivyo,
akiainisha malengo ya dayosisi hiyo ambayo anakuwa Askofu wake wa kwanza,
Askofu Mwenda alisema mbali ya kufundisha neno la Mungu, dayosisi hiyo
itahimiza ufanyaji kazi ili wakazi wake wawe na akiba ya chakula cha kutosha.
Alisema
watashirikiana na Serikali na wadau wa ndani najje katika kutoa huduma za
kijamii hasa elimu na afya. Aidha alisema atakabiliana na changamoto za sasa
ambazo alizitaja kuwa ni mmomonyoko wa maadili, rushwa, mauaji ya albino,
unajisi wa watoto na ubakaji wa wanawake.
Akitoa
shukrani kwa niaba ya waumini wa kanisa hilo, Askofu Mkuu wa KKKT, Dk. Alex
Malasusa alisema Kanisa lingependa kupata viongozi ambao ni wacha Mungu. Akirejea
mahubiri yake, Askofu Malasusa alisema inashangaza kuona kuna baadhi ya watu
wanagombea nafasi za uongozi lakini hawana mapenzi na Mungu aliyewaumba watu
anaotaka kuwaongoza.
“Bila
kujali imani ya mtu, tunatamani tungepata kiongozi ambaye anamcha Mungu. Awe
anapenda kuhudhuria ibada. Awe anampenda Mungu ndipo atawapenda watu anaowaongoza,”
alisisitiza.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMAPILI, JULAI 27, 2014
No comments:
Post a Comment