Na Masau Bwire, Ikwiriri
MGOGORO
mkubwa uliozuka Ikwiriri, Rufiji, mkoani Pwani kati ya wakulima na
wafugaji kwa siku mbili mfululizo na kusababisha uharibifu mkubwa wa
mali umemalizika jana.
Utulivu katika eneo la Ikwiriri, umerejea
baada ya Mkuu wa Operesheni Maalum za Jeshi la Polisi nchini, SACP Simon
Siro, kutumia njia za kidiplomasia kutatua mgogoro huo.
Juzi
jioni mwanadiplomasia huyo aliwaita na kukutana faragha kwa mazungumzo
ya nini kifanyike ili kuleta amani katika eneo hilo kwa kushirikisha
wananchi, viongozi wa dini, wanasiasa, baadhi ya viongozi wa Serikali,
wafanyabiashara wakubwa na wazee mashuhuri.
Mazungumzo hayo
yaliyodumu kwa zaidi ya saa nne, yalizaa matunda baada ya viongozi hao
kukubali kuwatangazia wananchi kuacha vurugu na kuingia katika meza ya
mazungumzo kati yao na Jeshi la Polisi ili kurejesha amani kwa njia
salama.
Kamanda Siro aliwaambia viongozi hao kuwa, amani ya
Ikwiriri haitapatikana kwa mabomu ya machozi au risasi za moto bali kwa
njia ya mazungumzo ili kutafuta namna ya kuondoa kasoro zilizojitokeza
na kusababisha vurugu hizo.
Viongozi hao walielewa somo la
Kamanda Siro na kushiriki kuwaeleza wananchi umuhimu wa kuacha vurugu na
kuwasihi washiriki mkutano wa hadhara kati yao na Kamanda Siro ambao
ulifanyika jana katika Viwanja vya Africana mjini hapa.
Katika
mkutano huo ambao ulihudhuriwa na watu lukuki, wananchi wa pande zote
mbili, wafugaji na wakulima walipewa nafasi ya kuzungumza kero zao na
zikajadiliwa kwa pamoja chini ya usimamizi wa Kamanda Siro na kupatiwa
ufumbuzi.
Wananchi kupitia mkutano huo, walikubaliana kuacha
vurugu na kuweka maazimio matano ya nini kifanyike ili vurugu hizo
zisijitokeze tena na kuazimia wafugaji warudi katika mipaka yao na
wasivuke kuingia maeneo ya wakulima na viongozi wasiotekeleza majukumu
yao ipasavyo wawajibishwe.
Maazimio mengine ni kuhusu viongozi,
polisi na watendaji wengine wa Serikali wanaojihusisha na rushwa
wachukuliwe hatua, wafugaji waliohusika katika mauaji ya mkulima,
Bw.Shamte Kawangala (80), wakamatwe na wafikishwe mahakamani.
Azimio
lingine ni wananchi 53 waliokamatwa na kufikishwa mahakamani mashtaka
yao yachunguzwe kwa kina na wale wasiohusika waachiwe na watakaobainika
kuhusika sheria ichukue mkondo wake.
Akizungumza na Majira muda
mfupi kabla ya kuondoka na helikopta kutoka eneo la mkutano, Kamanda
Siro alisema maazimio yaliyofikiwa katika mkutano huo yameanza kufanyiwa
kazi.
Baadhi ya wakazi wa Ikwiriri walipongeza hatua ya Kamanda
Siro jinsi alivyoweza kushughulikia mgogoro huo na kuupatia ufumbuzi kwa
njia ya mazungumzo na maridhiano ya pamoja.
|
Rais
Jakaya Kikwete (katikati) akimsikiliza Waziri wa Nchi katika Ofisi ya
Rais Kazi Maalum, Profesa, Mark Mwandosya, mara baada ya kumuapisha
Ikulu, Dar es Salaam jana, kushoto ni mke wa waziri huyo, Bi. Lucy
Mwandosya. (Picha na Charles Lucas)
|
Na Thomas Dominick
JESHI
la Polisi mkoani Mara, limefanikiwa kukamata bunduki nne aina ya Short
Gun, SMG na risasi 436 katika kipindi cha wiki mbili baada ya kuwakamata
watuhumiwa nane wanaodaiwa kufanya uhalifu na uwindaji katika Hifadhi
ya Taifa ya Serengeti.
Akizungumza jijini , Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Robert Boaz, alisema jeshi
hilo lilipata taarifa za mkazi wa Kijiji cha Bisarara, wilayani hapa Bw.
Marwa Makoba (40), kuwa anamiliki silaha hivyo walikwenda kijijini hapo
ili kumkamata.
“Baada ya kumkamata, tulifanya upekuzi nyumbani
kwake na kupata silaha mbili aina ya SMG na risasi 228, alipofikishwa
kituoni tulifanya naye mahojiano kwa kina na kusema anashirikiana na
wenzake watano,” alisema Kamanda Boaz.
Aliongeza kuwa, Bw. Makoba
aliwataja wenzake kutoka mikoa mbalimbali ambao wakati huo walikuwa
mjini Mgumu ndipo polisi walikwenda eneo hilo na kuwakamata.
Aliwataja
watuhumiwa hao kuwa ni, Bw. Fares Nazareti (37), Bw. Erasto Chubwa
(46), wakazi wa Bukombe Geita, Magina Bathromeo (36) na Yohana Godfrey
(30), wakazi wa Urambo Tabora, Bw. Japhet Bua (28) na Bw. Amosi Kagoma,
wakazi wa Kibondo, mkoani Kigoma.
“Tulipofanya nao mahojiano, Bw.
Kagoma alikubali kutupeleka nyumbani kwao Kibondo na kuonesha SMG moja,
mwingine Bw. Godfrey alitupeleka Tabora na kuonesha silaha nyingine,”
alisema.
Kamanda Boaz alisema, katika tukio jingine ambalo
lilitokea Mei 20 mwaka huu, mtu aliyejulikana kwa jina la Bw. Keringo
Samara (30), baada ya kupekuliwa nyumbani kwake alikutwa na risasi sita
za SMG ambapo jeshi hilo linaendelea kumuhoji ili kujiridhisha kama
anaimiliki kihalali.
|
Na Grace Ndossa
WIZARA
ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, inaendelea kufanya ukaguzi
katika maeneo yote ya wazi ili kuhakikisha waliovamia maeneo hayo
wanaondolewa haraka iwezekavyo.
Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Bw.
Goodluck Ole Medeye aliyasema hayo Dar es Salaam juzi wakati akihojiwa
katika kipindi cha dakika 45 kinachorushwa na televisheni ya ITV.
Alisema Serikali imeacha maeneo ya wazi kwa ajili ya wananchi kupata sehemu za kukaa wanapopata majanga au hatari yeyote.
“Wizara
yangu imeanza kufanya ukaguzi wa maeneo ya wazi katika Wilaya ya
Kinondoni ili kuwaondoa wote waliojenga majengo, ukaguzi huu utaendelea
mikoani si kwa Dar es Salaam pekee. “Matumizi ya maeneo ya wazi
hayabadiliki, watu wasidanganywe, watu wengi wamejenga hulka ya kuvamia
viwanja vya watu, kujenga na kuuza, tukibaini hilo nyumba itabomolewa na
muhusika ataondolewa bila serikali kumpa kiwanja kingine,” alisema.
Alisema
Wizara hiyo kwa sasa imeboresha nyenzo za kufanyia kazi kwa kutumia
teknohama ili waweze kuweka kumbukumbu za ardhi vizuri na kuongeza kuwa,
Wenyeviti na Watendaji wanapaswa kusimamia ardhi zilizopo katika
maeneo yao na hawana mamlaka ya kuuza ardhi.
|
|
Na Suleiman Abeid, Kishapu
MADIWANI
wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu, mkoani Shinyanga, wamefikia azimio
la pamoja na kumkataa Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo, Bw.
Theonas Nyamuhanga. Mbali ya kumkataa Mkurugenzi huyo ambaye
hakuwepo katika kikao hicho, pia walimuomba Mkuu wa Polisi wa Wilaya
hiyo (OCD), kuhakikisha anamtafuta Bw. Nyamuhanga na kufikishwa katika
vyombo vya sheria. Sambamba na
hatua hiyo, madiwani hao pia wameagiza Benki ya NMB, Tawi la Manonga,
ishtakiwe kwa kuhusika na upotevu wa fedha za halmashauri sh. bilioni
6.7. Madiwani hao walifikia uamuzi huo jana katika kikao cha
kawaida cha Baraza la Madiwani wakidai kushangazwa kwao na kitendo cha
Serikali kushindwa kumchukulia hatua Mkurugenzi huyo.
Kutokana na
hali hiyo, madiwani hao wametishia kufunga na kulala nje ya ofisi za
Mkurugenzi ili kuhakikisha haingii tena ofisini. “Ndugu
Mwenyekiti, inasikitisha sana, huyu Mkurugenzi leo ni mara ya tatu
tumekuwa tukimkataa lakini haondoki,” walisema madiwani hao na kuongeza
kuwa, wameguswa na tuhuma mbalimbali zinazomkabili na kama Serikali
itashinikiza aendelee na kazi basi, watajiuzulu nyadhifa zao.
|
Posted: 22 May 2012 11:27 PM PDT
Mkurugenzi
Mtendaji wa Benki ya CRDB Dkt. Charles Kimei, akizungumza nawaandishi
wa habari (hawapo pichani) Dar es Salaam jana, kuhusu upanuzi wa huduma
kwa wateja wa benki hiyo, kusho ni Naibu Mkururugenzi Mtendaji Uendesha
na Huduma kwa Wateja, Bw. Saugata Bandyopadhyay. (Picha na Peter Twite)
|
|
No comments:
Post a Comment