|
Posted: 25 May 2012 12:37 AM PDT
|
Posted: 25 May 2012 12:35 AM PDT
JANA
Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam,ilitoa hukumu ya kesi iliyokuwa
imefikishwa mbele yake na aliyekuwa mgombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM)
Bi. Hawa Ng'umbi, akipiga matokeo yaliyompa ushindi Mbunge wa Jimbo la
Ubungo,Bw. John Mnyika.
Hukumu hiyo ilisomwa na jaji Bi. Upendo
Msuya, na kubainisha kuwa mdai katika kesi hiyo ameshindwa
kuithibitishia mahakama pasipo kuacha shaka juu ya madai aliyokuwa
akiyalalamikia. Kesi ya kupinga matokea zisifunguliwe kwa jazba
Jaji
Msuya alisema kuwa katika madai hayo ushahidi wa mashahidi wa mdai
haukuwa na nguvu na kwamba mdai hakuleta mashahidi wa kuunga mkono
madai yake.
Hii ni moja kati ya kesi nyingi ambazo zimefunguliwa
na baadhi ya wabunge wakipinga matokeo dhidi ya wapinzani hao.
Tunakumbuka wakati uchaguzi ulipomalizika aliyekuwa Katibu Mkuu wa CCM,
Bw. Yusuf Makamba, aliwataka wagombea wote wa chama hicho walioshindwa
kufungua kesi za kupinga matokeo kwa ahadi kuwa chama kitawasaidia.
Ahadi
hiyo ya Bw. Makamba inatufanya tuamini kuwa iliwafanya baadhi ya
wagombea wa chama hicho walioshindwa kufungua kesi hata kama hawakuwa na
ushahidi wa kutosha.
Japokuwa ni haki yao ya msingi kufanya
hivyo,lakini kesi zinazotupiliwa mbali na mahakama zinatakiwa kuwa
ushahidi kwetu kuwa baadhi yao walifungua kesi kwa shinikizo, bila
ushahidi wa kutosha.
Mfano mzuri ni kama kesi hiyo ambayo hukumu
iliyotolewa jana. Kesi kama hizi mara nyingi zinafunguliwa kwa jazba
bila watu kutafakari,
Kwa msingi huo tunaiomba Serikali sasa
ifikiri upya namna ambavyo inaweza kutunga sheria itakayosaidia kuwabana
watu wanaokimbilia mahakamani kufungua kesi baada ya kushinda bila kuwa
na ushahidi wa kutosha.
Tunasema hivyo kwa kutambua kuwa
Serikali inatumia fedha nyingi kuendesha kesi za aina hiyo. Wote
tunakumbuka kuwa kuna wakati mahakama ilikwama kusikiliza kesi hizo
kutokana na uhaba wa fedha, lakini baada ya mahakama kulalamika ilitoa
fungu hilo ili zianze kusikilizwa.
Lakini baadhi ya kesi
zinaonekana hazikuwa na kichwa wala miguu, matokeo yake zimesababisha
fedha za walipa kodi kupote, ambapo zingetumika kwa ajili shughuli
zingine za maendeleo.
Tunatoa mwito itungwe sheria yenye meno
makali itakayosaidia kuwabana wanaoshindwa na kukimbilia mahakamani bila
kuwa na ushahidi wa kile wanachokidai. Kwa kufanya hivyo tutaokoa fedha
za wananchi zinazotumika kuendesha kesi hizo.
|
Posted: 25 May 2012 12:34 AM PDT
Kaimu
Mkurugenzi wa Idala ya Kinga katika Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii,
Dkt. Geoffrey Kiangi, akizungumza wakati akifungua warsha ya siku moja
kwa waandishi wa habari (hawapo pichani), Dar es Salaam jana, iliyohusu
mafunzo ya uelewa wa ugonjwa wa Malale unaoambukizwa na Mbung'o. (Picha
na Charles Lucas)
|
Posted: 25 May 2012 12:29 AM PDT
Na Stella Aron
NI
miaka mingi sasa tangu kupata uhuru, kumekuwa na harakati mbalimbali za
kuwawezesha wananchi kutambua ama kushiriki mambo mbalimbali ya
kuboresha maisha ya jamii.
Serikali na asasi zisizo za kiserikali zimeshiriki kwa namna moja au nyingine katika kuendesha harakati hizo.
Pamoja
na mafanikio mbalimbali yaliyopatikana katika kuhamasisha wananchi,
bado kuna mambo mengi ambayo yanahitaji kufanyiwa kazi zaidi hasa
katika kipindi hiki cha utandawazi pamoja na kukabiliana na mfumo wa
soko huria.
Bi. Mayrose
Majinge ni mwanaharakati mwenye elimu ya juu anazungumzia zaidi
kuhusiana na nini Watanzania wanahitaji katika kuboresha na kupatikana
kwa maendeleo nchini na hasa katika kipindi hiki cha utandawazi pamoja
na kukabiliana na mfumo wa soko huria.
Anasema harakati za
kuwahamasisha vijana wajue namna ya kukabiliana na umaskini itasaidia
ili kuwawezesha kuendana na utandawazi na kukabiliana na mfumo wa soko
huria.
Mwanaharakati huyo anasema kuwa, asilimia kubwa ya
watanzania bado wanafikiri kwamba jitihada za kuleta maendeleo ni jukumu
la serikali peke yake kwani ni tofauti na mtazamo walionao wananchi wa
mataifa mengine yaliyoendelea kwani hilo ni jukumu la kila mtu katika
nafasi yake.
Bi. Mayrose anasema, mwananchi ana uhuru wa
kuchangia mawazo yake katika kuboresha mipango ya maendeleo bila ya
kuvunja sheria za nchi. Anasema kuwa ili mwananchi aweze kuwa huru zaidi
sasa imefika wakati wa kila mtu kushiriki vema katika mchakato wa
uandaaji wa katiba mpya.
Anasema kuwa kwanza Rais Jakaya Kikwete
anapaswa kupongezwa kwa kukubali kubadilishwa kwa katiba na kuunda kwa
tume ya watu 30 iliyo chini ya Jaji Joseph Warioba kwa ajili ya
kukusanya maoni kwa wananchi kuhusiana na mabadiliko ya Katiba mpya.
Kuundwa
kwa tume hiyo kumeleta sura mpya miongoni mwa wananchi kutokana na
kilio cha muda mrefu ambapo wengi walikuwa wakilia na baadhi ya
vipengele ambavyo inadaiwa kuwa vimepitwa na wakati na vinatakiwa
vifanyiwe marekebisho kulingana na wakati tuliopo sasa.
Historia
ya Katiba yetu tuliyonayo hivi sasa, inaonyesha kulikuwa na
ushirikishwaji hafifu wa wananchi. Hii inaanza kujidhihirisha tangu
kupatikana kwa uhuru Katiba ya kwanza iliandikwa na Waingereza na
kuikabidhi kwa serikali ambao ni wazalendo jambo ambalo lilionyesha kuwa
katiba hiyo ilisheheni mapendekezo ya upande mmoja.
Katiba hiyo
ilionyesha dhahiri kumkera Mwalimu Julius Nyerere kutokana na muundo wa
uongozi ambapo mwaka 1962 aliifuta na kuiunda upya huku ikionyesha kumpa
zaidi yeye madaraka badala ya ile ya awali ambayo watawala wa juu
walikuwa ni Waingereza na yeye alikuwa kama ni Waziri Mkuu.
Kwa
historia hii inaonyesha kuwa maamuzi hayo yalikuwa ni ya busara lakini
hayakuwashirikisha wananchi ambao ndiyo wadau wakuu wa katiba hiyo.
Pia
tume maalum ya Katiba iliyoundwa mwaka 1977 chini ya uongozi wa Sheikh
Thabit Kombo na Pius Msekwa nayo ilionyesha kutokukidhi matakwa ya
wananchi kwa kuwashirikisha vya kutosha katika kuchangia na kutoa maoni
yao ya nini wanakihitaji na hawakitaki.
Katiba ya sasa, maana
yake ni kwamba sasa tunafungua ukurasa mpya ambapo wananchi
watashirikishwa tofauti na Katiba zilizopita ili kuondoa malalamiko na
mapungufu yasiyo na lazima ambayo kwa kiasi fulani yamekuwa yakichangia
kila kukicha kuibuka kwa mizozo isiyo ya lazima.
Wananchi ndiyo
wenye Katiba hivyo wanapaswa kushirikishwa tangu mwanzo wa mchakato hadi
mwisho, tukiangalia historia ya nyuma mwaka 1992, Rais mstaafu Ally
Hassan Mwinyi aliunda Tume ya kuratibu maoni kuhusu mfumo wa vyama vingi
vya siasa, tume hiyo iliyoongozwa na Jaji Francis Nyalali, ilifanya
kazi na kutoa matokeo kwamba asilimia 80 ya Watanzania hawataki mfumo wa
vyama vingi.
Bi. Mayrose anasema kuwa mbali ya mapungufu
yaliyopendekezwa kufanyiwa marekebisho, Serikali ilikubali mfumo wa
vyama vingi lakini ikaendelea kuzikumbatia sheria ambazo zinaonyesha
zimepitwa na wakati.
Wakati ule pia Rais Mstaafu Benjamin Mkapa
naye aliunda Tume ya Jaji Robert Kisanga ya mwaka 1998 ambapo baada ya
kukusanya maoni hayakufanyiwakazi na serikali kwa madai kuwa tume hiyo
imevuka mpaka.
Pia mwaka 2006 rais Mkapa aliunda Tume ya
kuchunguza tatizo la rushwa nchini chini ya Jaji Joseph Sinde Warioba
mbali ya mapendekezo ya mchakato mzima ya nini kifanyike ili kukomesha
tatizo hilo, mapendekezo hayo hayajashughulikiwa ipasavyo hadi leo
rushwa imeota mzizi na inaendelea kulitafuna taifa.
Anasema kuwa
ana imani kuwa kwa tume iliyoundwa hivi sasa itakuwa ni kwa ajili ya
maslahi ya wananchi na taifa kiujumla hivyo kilichobaki kwa wananchi ni
kutoa maoni yao bila ya woga kwani ni kwa faida yao. Na anaamini kwa
dhamira aliyonayo Mhe. Rais Jakaya Mrisho Kikwete atasimamia vema
mapendekezo yote yatakayotolewa na Tume ya Katiba.
Mwanaharakati
huyo anaendelea kusema kuwa Watanzania wanapaswa kuelewa kuwa rais ndiye
mkuu wa nchi hivyo anapaswa kuheshimiwa hata kama atakuwa amemteua mtu
mwenye umri mkubwa zaidi yake.
"Huyu anapaswa kuheshimiwa hata
kama kuna mtu mwenye umri mkubwa zaidi yake kwani ndiye mwenye mamlaka
ya juu zaidi ndani ya nchi yetu,'
Aliongeza "Rais anapaswa
kupewa nguvu zaidi na ulinzi kwani ndiye mkuu wa nchi na asije akatokea
mtu mwingine akawa mkuu zaidi yake na hiyo ni kwa ajili ya usalama wake
ili isifike mahala akawa hana mamlaka ya kutoa maamuzi kwa baadhi ya
vitu kwani taifa litakuwa lisilo kuwa na nguvu ya kutosha, " alisema.
Akizungumzia
kuhusiana na matumizi ya lugha ya Kiswahili, anasema kuwa sasa ifike
mahala kiswahili kitumike kwenye mikutano yote bila ya kujali ni
mikutano ya kitaifa.
Anasema kuwa ni bora sasa kukawa na watu
maalumu watakaokuwa wakifanyakazi ya kuwafundisha wageni lugha ya
kiswahili badala ya kutumika lugha ya kiingereza.
Kutokana na
kujali lugha ya kiingereza hivi sasa kwenye mikataba kumekuwa na
utumikaji wa lugha ya kiingereza huku lugha yetu ikibaki nyuma kama
mapambo.
Mwanaharakati huyo anasema kuwa ana imani kuwa kama
Serikali itasimamia suala hilo kwa kushirikiana na Baraza la Kiswahi
Tanzania (BAKITA) lugha hiyo inaweza kuendelea zaidi kuwa chimbuko la
maendeleo.
Aidha mwanaharakati huyo amewashauri wanawake
kujitokeza kwa wingi katika utoaji wa maoni kwenye katiba ili kwenye
mapungufu yaweze kurekebishwa na kuwepo kwa uwiano sawa.
Anasema
kuwa maendeleo ya taifa hili yanatokana na mwanamke kwani katika familia
mwanamke anapokuwa ameyumba kwa asilimia moja kuhusiana na hali ngumu
ya maisha basi mwanaume atakuwa na asilimia 2.
Aidha
mwanaharakati huyo amewashauri wanaharakati wote nchini watilie mkazo
suala la kila Mtanzania kwa nafasi yake kutimiza wajibu wake
kikamilifu, kwani kazi ndio msingi wa kupata haki zote kwani itaweza
kusaidia kuwakomboa Watanzania ambao baadhi yao wanakabiliwa na hali
ngumu na kupatikana kwa maendeleo nchini.
|
Posted: 25 May 2012 12:28 AM PDT
Bi. Mayrose Majige
|
Posted: 25 May 2012 12:22 AM PDT
Na Florah Temba, Kilimanjaro
JAMII
imetakiwa kuondokana na mitazamo potofu juu ya watu wenye ulemavu,
pamoja na kuzingatia mahitaji ya watu hao wakati wa ujenzi wa
miundombinu ili kuwawezesha kupita kwa urahisi pasipo usumbufu.
Rai
hiyo ilitolewa na Shirikisho la Vyama vya Watu Wenye Ulemavu Tanzania
(SHIVIWATA) mkoani Kilimanjaro wakati wa mafunzo ya kuvijengea uwezo
vyama vya watu wenye ulemavu Manispaa ya Moshi ambapo walijadili mambo
mbalimbali ikiwemo vikwazo na mitazamo hasi iliyojengeka katika jamii
juu ya watu wenye ulemavu.
Katibu wa shirikisho hilo mkoani
Kilimanjaro Bw. Zacharia Masawe alisema walemavu katika mkoa huo na
nchini kote wanakabiliwa na changamoto kubwa ya mtazamo hasi ambapo
wamekuwa wakionekana kuwa ni watu ombaomba na watu wasioweza kufanya
chochote jambo ambalo si sahihi.
Alisema, mitazamo hiyo katika
jamii imekuwa ikisababisha walemavu kudharaulika na kukosa haki zao za
kimsingi ikiwemo elimu ambapo hata wakati mwingine hukoseshwa haki ya
msingi ya kuishi kwa kuuawa.
“Kumekuwepo na mitazamo hasi katika
jamii kuhusiana na sisi watu wenye ulemavu, kwani katika jamii tumekuwa
tukionekana kuwa sisi ni watu ombaomba na hata wakati mwingine unakuta
unakwenda katika ofisi ya kiongozi ikiwemo za serikali, lakini unapotaka
kumuona kiongozi huyo unashangaa unaletewa sh. 500 na kuambiwa uondoke
kwa kweli hii ni udhalilishaji na uonevu kwetu sisi,” alisema Bw.
Masawe.
Bw. Masawe alisema ufike wakati sasa jamii ibadilike na
iwaone walemavu kama watu wengine ambao wanahitaji kuthaminiwa,
kuajiriwa na wasiwanyanyapae kwani hakuna mtu aliyezaliwa na kutaka
kuwa mlemavu.
Kwa upande wake Bw. Rumisha Masam alisema walmavu
wamekuwa wakikumbana na vikwazo mbalimbali ikiwemo miundombinu mingi
kujengwa pasipokuzingatia mahitaji ya watu wenye ulemavu.
“Jamii
kwa saa inapaswa kuthamini watu wenye ulemavu na kuondokana na ile dhana
kuwa walemavu ni watu wa kusaidiwa na hawana msaada wowote kwa jamii na
sasa ibadilike na iwathamini kwani walemavu ni watu kama watu wengine
na wanaweza kufanya kazi endapo wataendelezwa, lakini pia ihakikishe
miundombunu yote inayojengwa inazingatia mahitaji yao,”alisema Bw.
Rumisha.
Aidha aliongeza kuwa ili kuwawezesha walemavu kuweza
kuondokana na hali ya utegemezi katika jamii serikali iweke mpango
mkakati maalumu wenye upendeleo chanya ili kupanua soko la ajira kwa
watu wenye ulemavu hapa nchini.
|
Posted: 25 May 2012 12:19 AM PDT
Bibi
akiwa na wajukuu zake walioacha baada ya mtoto wake wa kike kukimbiwa
na mume.Ukatili unaofanywa na wanaume kutelekeza familia umekuwa kikwazo
kwa maendeleo ya wanawake wengi.
|
Posted: 25 May 2012 12:09 AM PDT
Na Reuben Kagaruki
MWAMKO
wa wazazi kutambua umuhimu wa elimu unazidi kuongezeka nchini,
ikilinganishwa na miaka ya nyuma. Umuhimu wa elimu kwa watoto umechangia
uwekezaji katika sekta hiyo kuongezeka kwa kasi ya aina yake. Jambo
hili ni kati ya mambo ya kujivunia.
Watu
binafsi, mashirika ya dini na wadau wengine wameonesha wazi kusaidia
juhudi za Serikali za kuinua elimu nchini. Kinachotia moyo zaidi wazazi
wengi kuhitaji watoto wao wapate elimu bora si bora elimu.
Kwa
kufahamu hilo, wazazi wamekuwa wakihaha kutafuta shule bora za kusomesha
watoto wao hasa zile zitakazokidhi matakwa wanayohitaji. Mfano, miaka
ya nyuma kulikuwa na kasi kubwa ya wazazi kupeleka watoto wao kusoma nje
ya nchi.
Mfano mzuri ni kwenye nchi za Uganda na Kenya. Kasi
hiyo inazidi kupungua baada ya shule zinazoanzishwa nchini kukidhi
viwango ambavyo wazazi wengi wanahitaji. Katika eneo hili tunastahili
kuipongeza Serikali kwa kufungua milango ili watu wawekeza katika sekta
hiyo.
Kuanzishwa kwa shule hizo pia kumesaidia kuwapunguzia
wazazi gharama, kwani awali walikuwa wakitumia fedha nyingi kwenda
kusomesha watoto nje ya nchi.
Kinachodhihirisha kuwa shule zenye
ubora zipo nchini ni matokeo ya mitihani yaliyotangazwa jijini Dar es
Salaam hivi karibuni. Mkoa wa wa Dar es Salaam ulitangaza shule 10
bora zilizofanya vizuri zaidi katika mtihani wa kumaliza darasa la saba
mwaka 2011, ambapo Tusiime iliyopo Tabata iliongoza kimkoa.
Katika
matokeo hayo rasmi ya Serikali ya Mkoa wa Dar es Salaam shule hiyo
ilikuwa ya kwanza baada ya kufaulisha wanafunzi wake wote 139 waliofanya
mtihani wa kuhitimu darasa la saba mwaka jana.
Matokeo hayo rasmi yanaonesha shule zilizofuatia kimkoa ni St Joseph, Montfort, Masaka, Filbert Bayi, Azanaki, Mountain Hill, Hollycross, Moga
na Canossa. Matokeo hayo yalitangazwa rasmi wakati wa mkutano kati ya
Ofisa Elimu Mkoa wa Dar es Salaam, Bw. Benard Makali na Maofisa Elimu na
walimu wakuu wa shule za msingi jijini Dar es Salaam.
Bw. Makali anasema matokeo rasmi yanaonesha kuwa shule ya Tusiime iliyopo Tabata ndiyo imekuwa ya kwanza kimkoa kwa kufaulisha wanafunzi wote wa shule ya msingi kwenye mitihani ya kumaliza darasa la saba mwaka 2011.
Katika matokeo ya Wilaya ya Ilala Tusiime pia imekuwa ya kwanza ikifuatiwa na shule za St Joseph, St Theresoflisieux, African, Agens Michael, Mkoani, Boma, Christ The King, Al Madrasa-Tus Asaifiya na New Ambasador.
Akifafanua kuhusu taarifa ambazo zimekuwa zikiwachanganya Watanzania kuhusu baadhi ya shule jijini Dar es Salaam kujitangaza kwamba zimekuwa za kwanza kiwilaya na kimkoa wakati sio kweli, anasema; "Nitazichunguza shule hizo na kuchukua hatua."
Bw. Makali alionesha kuchukizwa na tabia ya shule hizo na aliahidi kufuatilia taarifa hizo na itakapobainika kwamba ni kweli, hatua kali zitachukuliwa kwa shule husika ili iwe fundisho.
“Mimi sitambui matokeo mengine zaidi ya haya yanayoonesha kuwa Tusiime
ndiyo imeongoza kimkoa na kiwilaya, hao wanaojitangaza kwenye vyombo
vya habari kuwa wamekuwa wa kwanza hayo matokeo wameyatoa wapi? Huu ni
uongo wa hali ya juu na itabidi nifanyie kazi tabia hii ili Watanzania
wasiendelee kupotoshwa,” alisema.
Katika matokeo rasmi ya Wilaya ya Kinondoni shule 10 bora ni
Filbert Bayi ambayo ndiyo imekuwa ya kwanza ikifuatiwa na Drive Inn,
Ali Hassan Mwinyi Elite, Sunray, Msisiri ‘B’, Sunrise, Sahara, Mirambo, Bethel Mission na Anininduni.
Temeke shule ya kwanza ni Montfort, Hollycross, Al-Hikma, Fraylouisamigo, Shalom, Chang’ombe, Minazini, St Marys International, Kurasini na Mivinjeni.
Kutokana na kufanya vizuri zaidi, Manispaa ya Ilala jijini Dar es Salaam, iliiipa tuzo maalum shule ya Tusiime kwa kufanikiwa kufaulisha wanafunzi.
Tuzo hiyo ilitolewa hivi karibuni na manispaa hiyo kwa mkuu wa shule hiyo, kama ishara ya kutambua mchango wa shule hiyo katika kukuza elimu nchini.
Bw.
Makali, alisema shule ya Tusiime inastahili kupewa tuzo hiyo maalum
kutokana na kufaulisha wanafunzi wote na kwa kuwa ya kwanza kimkoa miaka
miwili mfululizo.
“Wamekuwa wa kwanza kimkoa kwa miaka miwili mfululizo na tuzo waliyopata ni kutokana na kufaulisha wanafunzi wote kwa asilimia 100, haya ni mafanikio makubwa kielimu nawapongeza,” alisema.
Mwalimu wa taaluma wa shule hiyo, Bw. Philibert Simon, anasema wanafunzi 19 walichaguliwa kujiunga na shule za vipaji maalum.
Alitaja
baadhi ya shule za vipaji maalum walizochaguliwa wanafunzi hao kujiunga
nazo kuwa ni Ilboru, Kibaha, Tabora Boys, Mzumbe, Ifunda Ufundi na
Iyunga Ufundi.
Aliongeza kuwa si mara ya kwanza kwa shule hiyo
kupewa tuzo ya aina hiyo, kwani Julai 2010 ilipewa tuzo ya aina hiyo na
manispaa hiyo hiyo kwa kufaulisha wanafunzi kwa daraja A mwaka 2009.
“Siri ya mafanikio ni uongozi wa shule kutoa ushirikiano wa kutosha kwa walimu, wazazi kwa upande wao wamekuwa wakitimiza wajibu wao na haya ndiyo yametufikisha hapa tulipo,” anasema.
Anasema mazingira mazuri ya shule nayo yamekuwa na mchango mkubwa katika kuhakikisha wanafunzi wanapata muda wa kutosha wa kusoma na kushiriki michezo mbalimbali.
"Tunaamini kwamba matokeo haya hayakuja kwa bahati mbaya, bali kumetokana na moyo wa kujituma kwa wanafunzi na walimu wao. Kufaulisha wanafunzi wote si jambo la bahati kwani tumeshuhudia shule nyingi zikifelisha nusu ya wanafunzi katika mitihani ya mwisho," anasema.
Hakuna shaka kwamba ufaulu huo mkubwa umetokana na jitihada za walimu kufuatilia wanafunzi kuhakikisha wanafuata misingi ya masomo na kujisomea ili waweze kufanya vyema.
Anasisitiza
kuwa walimu wa shule zingine nao wanapaswa kuwa na moyo wa uzalendo kwa
kufundisha kwa ari na moyo wa kujituma ili kuboresha elimu nchini.
Anaongeza
kuwa pamoja na mazingira magumu ya baadhi ya walimu kwenye shule
mbalimbali hasa za serikali wajitaidi kusahau ugumu huo na kufanya kazi
kwa bidii na maarifa ili kuinua kiwango cha taaluma.
Hata hivyo
anakiri kuwa mazingira ya shule nayo yanachangia kwa kiasi kikubwa
kiwango cha ufaulu kwa shule za binafsi na za Serikali zinapaswa kuiga mfano huo.
Anasema
vifaa vya kujifunzia kama maabara navyo vina nafsi yake, kwani
mwanafunzi kujifunza bila vitendo haiwezi kumsaidia siku za usoni.
Mwanafunzi akiambiwa kuhusu kifaa sayansi ili aweze kukielewa vyema ni muhimu zikawepo maabara za shule hiyo ili kuhakikisha wanapata ufahamu wa hali ya juu.
|
Posted: 25 May 2012 12:08 AM PDT
Wananfunzi wakifuatilia moja ya matukio yaliyohusu mijadala ya elimu.
|
Posted: 24 May 2012 11:59 PM PDT
Na Mwali Ibrahim
NAIBU
Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Amos Makalla jana
alikabidhi bendera ya taifa kwa timu ya taifa ya Wanawake ,Twiga Stars,
kabla ya kuelekea Ethiopia kwa ajili ya Fainali za Nane za Kombe la
Afrika kwa Wanawake (AWC), zitakazofanyika Novemba mwaka huu, Equatorial
Guinea.
Twiga Stars waliondoka
nchini jana saa 11 jioni kwa ndege ya Shirikia la Ndege la Ethiopia,
kikosi hicho kikiwa na msafara wa watu 24 wakiwemo wachezaji, benchi la
ufundi na viongozi itacheza na Ethiopia katika mechi ya kwanza ya raundi
ya pili ya michuano ya mchujo kwa ajili ya fainali hizo, ambapo mechi
yao inatarajiwa kuchezwa Jumapili kwenye Uwanja wa Addis Ababa, kabla ya
kurudiana wiki mbili baadaye Dar es Salaam.
Timu ya Twiga Stars ikifanikiwa kuitoa Ethiopia itakuwa imepata tiketi ya kwenda Equatorial Guinea.
Wachezaji
walioondoka na kikosi hicho ni Amina Ally, Asha Rashid (nahodha), Ester
Chabruma, Ettoe Mlenzi, Evelyn Sekikubo, Fadhila Hamad, Fatuma Bashiri,
Fatuma Khatib, Fatuma Mustafa, Fatuma Omari, Maimuna Said, Mwajuma
Abdallah, Mwanahamisi Omari, Mwanaidi Tamba, Mwapewa Mtumwa, Rukia
Hamis, Semeni Abeid na Zena Khamis.
Kwa upande wa Benchi la
Ufundi ni Charles Mkwasa (Kocha Mkuu), Nasra Mohamed (Kocha Msaidizi),
Furaha Francis (Meneja wa Timu), Mwanahamisi Abdallah (Mtunza Vifaa) na
Christina Luambano (Daktari wa Timu).
Twiga Stars ambayo msafara
wake uliongozwa na Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu kwa Wanawake
Tanzania (TWFA) ambaye pia ni mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho
la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Lina Mhando itarejea nyumbani siku
moja baada ya mchezo huo saa 6 mchana kwa ndege ya Shirika la Ndege la
Ethiopia.
Kabla ya mechi hiyo, Twiga walishajipima nguvu na mechi
za kimataifa dhidi ya Zimbabwe na kufungwa mabao 4-1 na Banyana Banyana
ya Afrika Kusini ambayo iliwafunga mabao 5-2.
|
Posted: 24 May 2012 11:57 PM PDT
Na John Gagarini, Pwani
KITUO
cha Afya wilayani Kibaha Mkoa wa Pwani kinahitaji kiasi cha shilingi
bilioni 13 kwa ajili ya upanuzi wa kituo hicho ili kuwa hospitali ya
wilaya hiyo.
Akizungumza na wandishi wa habari ofisini kwake jana
Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Mji wa Kibaha Dkt. Kaniki alisema kuwa
tayari ujenzi huo umeanza.
Dkt.
Kaniki alisema kuwa wamepeleka maombi maalumu serikalini kwa ajili ya
ujenzi huo ambapo waliomba kiasi cha shilingi milioni 500 na kuwapatiwa
shilingi milioni 290.
“Kiasi hicho cha fedha kilitolewa mwaka
2008 na 2009 ambazo zilitumika kwa ajili ya kujenga jengo la wagongwa
nje yaani OPD, ” alisema Dkt. Kaniki.
Alisema kuwa, majengo
ambayo yataongezwa ni jengo la wazazi na watoto wachanga, upasuaji
mkubwa na akinamama, jengo la maabara, exray, wodi za wagonjwa wanawake
na wanaume, jengo la magonjwa ya kuambukizwa jengo la kuhifadhia maiti
na jengo la usafi.
“Mbali ya kupeleka maombi maalumu pia
tumepeleka kwenye balozi za Korea Kusini kitengo cha misaada kwa huduma
za afya na ubalozi wa Ireland ambako kote kwa bahati mbaya fedha
hazikuweza kupatikana,” alisema Dkt. Kaniki.
Mganga Mkuu huyo wa
halmashauri ya mji Kibaha alisema kuwa eneo la hospitali hiyo lina
ukubwa wa hekari zaidi ya 10 na kuwataka wadau mbalimbali kujitokeza
kufanikisha ujenzi huo.
Aidha aliwaomba wafadhili kujitokeza
kuwasaidia ili waweze kufanikisha ujenzi huo ambapo michango imekuwa ni
changamoto kubwa kufanikisha upanuzi huo ili kuisaidia Hospitali ya
Tumbi ambayo itakuwa ya mkoa.
|
Posted: 24 May 2012 11:56 PM PDT
Mchungaji
wa Kanisa la Pentekoste la LIFT HIM UP lililopo eneo la SanawariJuu
mkoani Arusha Orche Mgonja (kushoto) akimuiombea mmoja wa waumini wa
kanisa hilo Sabrina Masirori, wakati wa Maombi kwenye Kituo cha Maombezi
maarufu Hospitali ya Rufaa juzi, aliyekuwa katika matatizo mbalimbali
ya kiimani. (Picha na Richard Konga)
|
Posted: 24 May 2012 11:53 PM PDT
Na Moses Mabula, Tabora
KATIBU
Mkuu wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali Kuu na Afya taifa (TUGHE) Bw.
Ally Kiwenge ameitaka Serikali itekeleze kwa vitendo ahadi yake ya
kupandisha mishahara kwa watumishi wa umma ifikapo Julai Mosi mwaka huu
ili kuepusha mivutano baina ya pande hizo mbili.
Bw.
Kiwenge alitoa kauli hiyo jana mjini Tabora alipokuwa akizungumza na
watumishi wa afya katika Hospitali ya Mkoa wa Tabora Kitete.
Alisema
kwamba, Serikali ni lazima itekeleze ahadi yake hiyo kwa watumishi wake
kama ambavyo Rais Jakaya Kikwete alivyoahidi siku ya maadhimisho ya
wafanayakazi Duniani Mei Mosi yaliyofanyika mkoani Tanga.
Alisema
kuwa, kila mwaka Serikali imekuwa ikitangaza nyongeza hewa ya mishahara
kwa watumishi wake hususan wale wa sekta ya afya hali ambayo inafanya
watumishi kutokuwa na imani na ahadi za Serikali yao na kupekelekea
kufanya kazi chini ya kiwango.
“Chonde chonde mheshimiwa Rais
Kikwete ninakuomba ahadi yako iwe ya kweli, sisi hapa tunasubiri tu,
ifikapo Julai mwaka huu 'kahela ketu' kawe kameongezeka kwenye akaunti
zetu,” alisisitiza Bw.Kiwenge.
“Sisi hatuna ugonvi na Serikali
hata kidogo ugonvi wetu ni masilahi duni, lakini 'kamshahara ketu'
kakiongezeka' sisi hatuna mgogoro kabisa na Serikali,” alisema Bw.
Kiwenge.
Akiwageukia watumishi wa afya Bw. Kiwenge aliwataka
wauguzi wote hapa nchini kutoa huduma ya afya kwa wagonjwa kwa moyo wa
upendo, huruma na kutowanyanyapaa.
Alisema kuwa, kiapo cha
muuguzi ni kuwa na upendo, huruma kwa wagonjwa wanaowahudumia sanjari na
kujiupusha na vitendo vinavyokwenda kinyume na viapo vyao vya kazi yao
ya uuguzi.
Alisema kuwa, kazi ya muuguzi ni kutoa huduma bora kwa
mgojwa anayefika kutibiwa hospitalini na kwamba kwenda kinyume na kiapo
cha cha kazi yake ni kutenda dhambi kwa Mungu.
Katibu Mkuu huyo
wa TUGHE taifa alieleza kuwa kazi ya mtumishi wa idara ya afya imebeba
dhamana kubwa ya usalama wa afya katika taifa, hivyo ni lazima
wahakikishe wanatoa huduma kwa jamii isiyokuwa na mashaka wala
malalamiko.
|
Posted: 24 May 2012 11:52 PM PDT
Na Elizabeth Mayemba
SIMBA
sasa imepania kufanya kweli katika usajili ambapo wanataka kuziba pengo
la kiungo wao Patrick Mafisango aliyefariki katika ajali ya gari hivi
karibuni, hivyo wameanza mazungumzo na viungo wanne kutoka Kenya na
Uganda.
Mbali ya viungo hao,
pia klabu hiyo inampango wa kuwasajili washambuliaji Juma Abdallah wa
JKT Ruvu na Jerrson Tegete wa Yanga, lengo ni kuwa na timu bora katika
michuano ya Kombe la Kagame na Ligi Kuu Tanzania Bara msimu ujao.
Akizungumza
na gazeti hili jana mmoja wa Wajumbe wa Kamati ya Usajili ya Simba,
ambaye aliomba kuhifadhiwa jina lake kwa madai wakati wa kuweka
hadharani usajili bado, alisema tayari wameanza mazungumzo na viungo
watano ambapo wawili kutoka Kenya na wawili wanatokea Uganda, na kwa
hapa nchini wameanza mazungumzo na washambuliaji wawili.
"Tutavunja
rekodi katika usajili wetu wala hatutaki kukurupuka lengo ni kuwa na
kikosi kilicho bora na si bora kikosi," alisema Mjumbe huyo.
Aliwataja
viungo hao ambao mmoja wapo ataziba pengo la Mafisango kuwa ni kiungo
wao wa zamani Jerry Santo ambaye kwa sasa anachezea Tusker ya Kenya,
Salim Kije wa FC Leopard ya Kenya, Owen Kasule na Mike Muchaba wote wa
Bunamwaya ya Uganda.
Mjumbe huyo alisema baada ya kamati yao
kuorodhesha majina hayo wataanza mara moja kupeleleza rekodi ya mchezaji
mmoja mmoja na watakayevutiwa naye watamsajili na kumtangaza moja kwa
moja.
Pia kwa wachezaji wazalendo Abdallah Juma hana tatizo
lolote ni makubaliano tu, ila Tegete kuna baadhi ya vitu wanamchunguza
na wakijiridhisha watamsajili katika kikosi chao.
|
No comments:
Post a Comment