Naibu
 Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Michael John akitoa 
tamko kuhusu  Siku ya Soko la Afya  iliyoandaliwa na Wizara hiyo kwa 
kushirikiana na Shirika la GIZ , itakayofanyika Oktoba 2 katika ukumbi 
wa Diammond Jubelee jijini Dar es salaam.
Naibu
 Meneja wa Miradi ya Afya wa GIZ Bw. Christian Ptleiderer akizungumza na
 waandishi wa habari kutoa wito kwa mashirika mengine yanayotoa huduma 
za afya nchini kuendelea kusaidia na kusambaza huduma zao katika maeneo 
yenye changamoto ya miundombinu na uhaba wa watumishi wa afya.Kulia ni 
Mtaalam na Mawasiliano wa shirika la GIZ nchini Bi. Vida Mwasalla.
Na. Aron Msigwa – MAELEZO.
30/9/2014.Dar es salaa.
Wizara ya Afya na Ustawi wa 
Jamii imesema kuwa itaendelea kushirikiana na Shirika la Ujerumani la 
GIZ katika uanzishaji na uendelezaji wa programu mbalimbali za utoaji wa
 huduma za afya zinazolenga kupunguza vifo vya watoto walio chini ya 
umri wa miaka 5. 
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya 
Afya na Ustawi wa Jamii, Michael John ameyasema hayo leo jijini Dar es 
salaam wakati akitoa tamko kuhusu Siku ya Soko la Afya  nchini 
iliyoandaliwa na Wizara hiyo kwa kushirikiana na Shirika la Ujerumani la
 GIZ  itakayofanyika Oktoba 2,  jijini Dar es salaam.
Amesema Tanzania na GIZ zimekuwa
 zikishirikiana katika uboreshaji wa miradi mbalimbali ya afya kwa 
kusogeza huduma za afya karibu na wananchi kuanzia ngazi ya taifa, mikoa
 na Halimashauri za wilaya.
Ameeleza kuwa mikoa ya Lindi, 
Mbeya, Mtwara na Tanga imeendelea kunufaika na miradi mbalimbali ya 
ushirikiano  chini ya shirika hilo inayolenga kuimarisha miundombinu ya 
kutolea huduma za afya katika maeneo hayo, uimarishaji wa mifuko ya Afya
 ya Jamii na ushiriki wa moja kwa moja kusaidia upatikanaji na 
uendelezaji wa wataalam wa kutoa huduma za afya maeneo ya vijijini. 
Ameongeza kuwa GIZ imekuwa 
ikishirikiana na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii katika kuhakikisha 
kuwa jamii inamudu huduma bora za afya kupitia Mifuko ya Hifadhi ya Afya
 ya Jamii iliyopo katika maeneo yao.
Aidha, amebainisha kuwa 
maonyesho ya siku ya Soko la Afya yatakayowahusisha wadau mbalimbali na 
mashirika yanayotoa huduma za afya nchini yanalenga kuwakutanisha wadau 
hao ili waweze  kujadili changamoto za utoaji wa huduma za afya nchni, 
kujifunza mafanikio yaliyopatikana katika baadhi ya maeneo na kuweka 
mikakati ya kuyafikia maeneo mengi zaidi.
Kwa upande wake Mtaalam na 
Mawasiliano wa shirika la GIZ nchini Bi. Vida Mwasalla ameeleza kuwa 
maonesho ya mwaka huu yazilenga Wizara, Taasisi , Washirika wa 
Maendeleo, Makampuni, Mashirika binafsi  na Wakala zinazojihusisha na 
utoaji na uendelezaji wa sekta ya afya nchini.
Amesema katika maonesho hayo GIZ
 kwa kushirikiana na Wizara ya Afya itaonyesha mikakati mbalimbali ya 
kuwaokoa watoto wadogo wenye matatizo ya afya, namna walivyofanikiwa 
kuwapata watumishi wa afya katika maeneo ya Lindi na Mtwara, maeneo  
ambayo hapo awali walikuwa hawakai katika vituo vyao.
Ameongeza kuwa mbali na Siku ya 
Soko la Afya kuhusisha huduma za utoaji wa elimu, vipimo, machapisho 
mbalimbali inalenga kuwaweka pamoja wadau hao ili waweze kubadilishana 
uzoefu na kuweka  mikakati ya kuchangia maendeleo ya sekta ya afya hapa 
nchini. 
Naye Naibu Meneja wa Miradi ya 
Afya wa GIZ Bw. Christian Ptleiderer ametoa wito kwa mashirika mengine 
yanayotoa huduma za afya nchini kuendelea kusaidia na kusambaza huduma 
zao katika maeneo ambayo bado yanakumbwa na changamoto mbalimbali za 
miundombinu na uhaba wa watumishi wa afya.
Amesema wao kama GIZ kwa kuanzia
 wameanza na mikoa 4, na wanaendelea kujenga uwezo wa kuyafikia maeneo 
mengi zaidi kwa kushirikiana na Serikali ya Ujerumani na Tanzania.
No comments:
Post a Comment