Mhe. Said Ali Mbarouk akiwa na 
mwenyeji wake Waziri wa Habari nchini Oman Sheikh Dk. abdulla  wakati  
alipofanya mazungumzo katika ofisi yake tarehe 29 Septemba 2014 akiwa 
katika ziara rasmi ya siku nne kutembelea sekta mbali mbali za Utalii, 
Utamaduni na Michezo.
MUSCAT, OMAN        30/09/2014
Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo Mh. Said Ali 
Mbarouk ameuelezea ushirikiano baina ya Oman na Zanzibar kuwa daima 
utakuwepo na utaendelea kukua kutokana na kutanuka kwa maeneo mapya ya 
ushirikiano katika Nyanja mbali mbali za maendeleo.
Amesema ni jambo la faraja kuona 
kuwa hivi sasa Zanzibar na Oman zinatambua umuhimu wa kutanua maeneo 
hayo ya ushirikiano katika sekta za uchumi, utalii na michezo kwa lengo 
la  kuwanufaisha watu wa pande zote mbili.
Mhe. Saidi Ali Mbarouk ameyaeleza 
hayo katika nyakati tofauti wakati alipokuwa na mazungumzo na Mawaziri  
wa sekta za Habari, Michezo, Utamaduni na Utalii mjini Muscat Oman leo, 
akiwa katika ziara yake ya siku nne ya kukutana na viongozi mbali mbali 
wa nchi hiyo kwa lengo la kukuza ushirikiano baina ya nchi hizo mbili.
Mapema akizungumza na Waziri wa 
Habari wa Oman, Sheikh Dk. Abdulla Monaim Bin Mansoor Al Husani, alitoa 
shukrani zake kwa Serikali ya Oman kwa misaada yake kwa Zanzibar na 
kusifu nidhamu   ya vyombo vya habari vya nchi hiyo katika kuwaunganisha
 watu na kuwawezesha kujenga uchumi imara.
Alisema hatua hii ya  mfano wa 
kuigwa inatokana na usimamizi  madhubuti  kwa vyombo vya habari na 
kujali kuwajibika kwa jamii kwa vile vinatoa nafasi ya kuwapatia taarifa
 za kutosha juu ya harakati za kujiendeleza na kujenga ustawi na 
maendeleo   yao.
Ameshauri haja ya kuwepo na 
utaratibu wa kubadilishana wataalamu na vipindi ili kila nchi iweze 
kujifunza kutoka upande mwengine kwa  kutambua maendeleo yanayofikiwa na
 kila upande na hivyo kutoa fursa za kuwawezesha vijana na vyombo vya 
habari kuongeza kasi ya utekelezaji wa majukumu yao kwa pamoja hasa kwa 
vile ni tegemeo kubwa la taifa katika kujenga uchumi.
Katika ziara yake hiyo ya siku 
nne, Mheshimiwa Saidi Ali Mbarouk pia alipata fursa ya kubadilishana 
mawazo na Naibu Waziri wa Utamaduni na Mambo ya Kale, Sheikh Hamad Hilal
 Al Maamari na Waziri wa Michezo, Sheikh Shallal Saad Moh’d Al Saad na 
kutuwama zaidi katika masuala ya kubadilishana wataalamu wa michezo na 
kuyahuisha majengo ya kihistoria yenye mnasaba na Oman.
Wakati huo huo,  Mhe. Said Ali 
Mbarouk ameitaka Oman kufungua fursa nyengine kwa kuisaidia Zanzibar 
katika kuanzisha Hoteli za kitalii za Halal utaratibu ambao Oman tayari 
imeuanzisha na kupata mafanikio yake.
Amefahamisha kuwa utaratibu wa 
hoteli kama hizo za Halal ni muafaka katika visiwa vya Zanzibar kwa vile
 zitaongeza soko la idadi ya watalii wanaohitaji kupumzika katika maeneo
 yenye utulivu wa maadili ya kidini na kiutamaduni.
Katika ziara yake hiyo Waziri huyo
 wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo alipata fursa ya kushiriki 
katika  karamu rasmi iliyoandaliwa kwa ajili yake  na ujumbe  wa watu 
watatu aliyofuatana na Mwenyeji wake Waziri wa Habari wa Oman Sheikh Dk.
 Abdulla Monaim iliyofanyika katika jumba la serikali la Opera mjini 
Muscat.
IMETOLEWA NA IDARA YA HABARI HABARI AMELEZO ZANZIBAR 

No comments:
Post a Comment