Naibu
Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mh. Luhaga Mpina
akiwa katika picha ya pamoja na Ujumbe wa kutoka Shirika la Maendeleo
la Umoja wa Mataifa na Wataalamu kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais mara
baada ya mazungumzo baina yao.
…………………………………………………………………………………………………
Na Lulu Mussa
Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa
Rais (Muungano na Mazingira) Mh. Luhaga Mpina hii leo amefanya
mazungumzo na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa
Mataifa (UNDP) Bi. Awa Dabo pamoja na ujumbe aliombatana nao, Ofisini
kwake Dar es Salaam.
Katika mazungumzo yao ujumbe huo
umeonyesha nia ya kufanya kazi kwa karibu na Ofisi ya Makamu wa Rais
hususan katika nyanja ya Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira ikiwa ni
pamoja na kupambana na mabadiliko ya Tabianchi na nishati mbadala.
Awali Naibu Waziri Mpina
aliwafahamisha kuwa Ofisi yake imeandaa Mpango Mkakati wa Kitaifa wa
kupanda miti nchi nzima na kuwataka wadau wa maendeleo kuwaunga mkono.
“Tunaendelea na jitihada za kupanda Miti mingi iwezekanavyo na katika
mwaka huu wa fedha Serikali imetenga fedha kwa ajili ya kazi hiyo”
alisisitiza Naibu Waziri Mpina.
Aidha, Naibu Waziri Mpina ametoa
wito kwa wadau wengine wa maendeleo kujitokeza kuunga mkono kampeni hii
kubwa ya upandaji miti nchi nzima na kusisitiza kuwa uhai wa viumbe
vyote unategema Mazingira hivyo ni vema kuyahifadhi na kuyalinda kwa
faida ya vizazi vya sasa na vijavyo.
Mheshimiwa Mpina pia amesema
Ofisi yake kwa sasa inafanya marekebisho ya Sera ya Mazingira na kujenga
uwezo kwa watendaji wa ngazi zote juu ya kusimamia Sheria ya Mazingira
ya mwaka 2004 pamoja na kuelimisha Umma juu ya kampeni ya Usafi ya kila
mwisho mwa mwezi.
kwa upande wake Bi. Dabo amesema
kuwa shirika lake limeweka vipaumbele vya kutekeleza ndani ya miaka
mitano ambavyo vinaendana na Mpango wa Maendeleo wa Taifa, sambamba na
kusaidia vikundi mbalimbali katika ngazi za vijiji juu ya kutunza vyanzo
vya maji na kuhifadhi mazingira.
Bi Dabo ameahidi kushirikiana na
Ofisi ya Makamu wa Rais katika jitihada za kukabiliana na changamoto za
Mabadiliko ya Tabianchi.
Naibu
Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mh. Luhaga Mpina
akimkaribisha Bi. Awa Dabo Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Maendeleo
la Umoja wa Mataifa. Mazungumzo baina yao yamefanyika leo Mtaa wa
Luthuli, jijini Dar es Salaam.
Ujumbe
kutoka Shirika la Maendeleo ya Umoja wa Mataifa, kutoka kushoto ni Bw.
Nehemia Murusuri, Bi. Getrude Lyatuu na Bi. Awa Dabo, walipomtembelea
Naibu Waziri Mh. Luhaga Mpina hii leo.
No comments:
Post a Comment