KLABU
 ya Kagera Sugar inaingia kambini desemba 31 mwaka huu, lakini mazoezi 
yataanza rasmi januari pili mwakani kujiwinda na mzunguko wa pili  ligi 
kuu soka Tanzania bara unaotarajia kuanza kushika kasi januari 25, 2014.
Kocha msaidizi wa klabu hiyo, Murage Kabange ameuambia mtandao huu kuwa nia yao ni kurejesha makali yao kama msimu uliopita.
“Mipango
 ya kambi imekamilika, mimi na kocha mkuu Jackson Mayanja tunajiandaa 
kukisuka kikosi chetu upya. Kuna makosa yaliyokuwepo mzunguko wa kwanza,
 tuliyagundua mapema na sasa kazi ni kurekebisha tu”. Alisema Kabange..
Kabange
 aliongeza kuwa katika dirisha dogo la usajili wamemuongeza  Andrew 
Mathew kazembe kutoka Abajalo FC  ili kukamilisha idadi ya wachezaji 25.
“Tulitumia
 muda mrefu kumchunguza mchezaji huyo, tumezingatia nidhamu na uwezo 
wake, kwa kiasi kikubwa atatusaidia ngwe ya pili  ya ligi kuu bara”. 
Aliongeza Kabange.
Aidha
 kocha huyo alisema tatizo la safu ya ulinzi limepata dawa baada ya beki
 wao wa kati, Amandus Nestar kurejea uwanjani  kufuatia  kupoma tatizo 
lake la mguu.
“Karibu
 mzunguko mzima, Nestar amekuwa akisumbuliwa na mguu, madaktari 
wamefanya jitihada kubwa kuhakikisha anarejea uwanjani. Hivi 
ninavyozungumza na wewe, beki huyo yuko tayari kuanza mazoezi na hali 
hii itaimarisha safu yetu ya ulinzi”. Alisema Kabange.
Kwa 
upande wake mshambuliaji hatari wa Kagera Sugar, Them Felix alisema kuwa
 anajiandaa vikali kuhakikisha anaisadia klabu yake kufanya vizuri na 
hatimaye kuingia tatu bora msimu huu.
Them 
aliongeza kuwa mchezaji wa mpira wa miguu hana mapumziko, pale timu 
inapopewa mapumziko, yeye anatakiwa kutafuta njia mbadala ya kufanya 
mazoezi binafsi ili kulinda uwezo wake na kasi yake.
“Binafsi
 nimekuwa nikifanya mazoezi na Bukoba Veteran, nimejijanga vizuri na 
nina uhakika wa kufanya vizuri. Kikubwa Mwenyezi Mungu atupe afya 
njema”. Alisema Them.
Msimu
 wa mwaka jana, Kagera Sugar ikiwa chini ya kocha Mkongwe, Alhaji 
Abdallah Athuman Seif `King Kibadeni Mputa` ilishika nafasi ya nne 
katika msimamo wa ligi kuu, huku nafasi ya tatu ikishikwa na Simba, ya 
pili Azam fc na mabingwa walikuwa Dar Young Africans.
Msimu
 wa mwaka huu, klabu hii haijawa na matokeo mazuri sana kwani mpaka 
mzunguko wa kwanza unamalizika, tayari imeshajikusanyia pointi 20 katika
 nafasi ya sita.

No comments:
Post a Comment