Moja ya Kikosi cha Mgambo Shooting mechi za nyuma katika michuano ya ligi kuu soka Tanzania bara. Picha na Maktaba
VIBONDE
 wa ligi kuu soka Tanzania bara, Mgambo Shooting ya mkoani Tanga imeanza
 mazoezi ya kujiandaa na mikikimikiki ya kukwepa mkasi wa kushuka daraja
 msimu  wa 2013/2014.
Akizungumza
 leo baada ya mazoezi ya timu hiyo, kocha msaidizi , Moka Shaban Dihimba
 amesema wameongeza wachezaji wanne katika dirisha dogo la usajili, 
hivyo watakuwa na nguvu mpya.
“Tulikuwa
 na mapungufu mengi, wachezaji walikuwa na hofu kubwa,  ndio maana 
tulifanya vibaya na kushika mkia. Tumewasajili Suleiman Khatib, Bolly 
Ajali, Amri Sambinga na Issa Ali ambao watatusaidia kupambana kufa na 
kupona”. Alisema Dihimba.
Dihimba
 alisema mazoezi yanakwenda vizuri chini ya kocha mkuu, Ramadhan Kampira
 na kikubwa wanachofanya kwa sasa ni kutafuta kasi na kumiliki mpira ili
 kuzikabili timu pinzani kwa umahiri.
“Timu
 za ligi kuu si kwamba zina mpira mkubwa sana, zote zinacheza soka la 
kawaida na sisi tunaweza kuwamuda kabisa. Nakuhakikishia kuwa kwa mechi 
13 zilizobaki, tutabaki ligi kuu”. Aliongeza Dihimba.
Kocha
 huyo alikiri kufanya vibaya zaidi mzunguko wa kwanza kwasababu 
walishinda mchezo mmoja tu, wakatoa sare tatu na kufungwa mechi tisa, 
hivyo kujikusanyia pointi 6 tu katika nafasi ya mwisho.
Alipoulizwa
 kwanini timu imekuwa na matokeo mabaya hata msimu wa mwaka jana, 
Dihimba alieleza kuwa wachezaji wao wanakosa uzoefu na wanatawaliwa na 
hofu hasa wanapokutana timu kubwa.
“Tunakaa
 na wachezaji kwa muda mwingi na kuwaelekeza nini cha kufanya, lakini 
wamekuwa wakifanya makosa makubwa yanayoigharimu timu. Wana makosa ya 
kiufundi na tumeyaona, lakini kwa sasa tumejipanga vizuri kushindana”. 
Alitamba Dihimba.

No comments:
Post a Comment