Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema.PICHA|MAKTABA
……………………………………………………………………………………
Arusha.Polisi
mkoani Arusha imekamilisha uchunguzi wake kuhusiana na kuungua kwa
Ofisi za Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na kusema wanachama
wa chama hicho ndio waliohusika.
Hata
hivyo, Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema amepinga kauli
hiyo na kulipa jeshi hilo siku nne kuwakamata na kuwahoji watuhumiwa
watano baada ya kulipatia majina hayo akidai kuwa ndio wanaohusika na
uchomaji moto ofisi za chama hicho.
“Tumewapatia
polisi majina… tunaamini walihusika moja kwa moja la sivyo, chama
kitatumia vijana wetu wa Red Brigade kuwakamata na kuwafikisha polisi,”
Lema aliwaambia waandishi wa habari jana.
Ofisi
cha Chadema zilizoko katika eneo la Ngarenaro, zilinusurika kuteketea
kwa moto juzi baada ya watu wasiojulikana kuwasha moto katika moja ya
vyumba vyake.
Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari jana, Kaimu Kamanda wa Polisi mkoani Arusha, Japhet Lusinga alisema:
“Katika
uchunguzi wetu, tumebaini kuwa hakuna mahali palipovunjwa kutoka nje ya
uzio na kuruhusu watu kuingia ndani… tumegundua kuna tundu dogo darini
eneo la kuelekea bafuni la upana wa futi moja na nusu kiasi haliwezi
kuruhusu mtu kupita.
“Tumejiridhisha kuwa hakuna mtu anayeweza kupita hapo na ndani tulikuta majivu na baadhi ya vitu vilivyoungua na vifaa vingine.”
Lema
akiwa na Mwenyekiti wa Chadema Wilaya ya Arusha, Ephata Nanyaro
alisema: “Tumebaini polisi wanataka kulifanya jambo hili kama la siasa
ndiyo sababu juzi badala ya kuanza kuchunguza waliohusika, waliwakamata
Mtunza Ofisi na mlinzi wetu na kuwalaza rumande hadi leo (jana) asubuhi
kwa madai eti wanawahoji.
“Hatukubaliani
na taarifa yao, hii ni siasa. Kulitokea mauaji ya bomu, wakasema
Chadema wamejilipua, leo ofisi imechomwa wanasema Chadema wenyewe, hili
hatukubali, “ alisema.
Msajili alaani
Msajili
wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis Mutungi amelaani tukio la
kuchomwa moto ofisi hizo za Chadema na kusisitiza kuwa wananchi hususan
wanasiasa wasiwe wepesi kuingiza hisia kwenye makosa ya kijinai.
Alisema kuwa tukio hilo linapaswa kukemewa kwa hali yoyote ile kwa kuwa linavuruga na kuhatarisha amani ya nchi.
Dk Slaa aanza ziara
Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Wilbrod Slaa amesema hakuna mtu yeyote mkubwa kuliko katiba ya chama hicho.
Dk
Slaa aliyasema hayo jana kwenye Uwanja wa CDT, Kahama mkoani Shinyanga,
alipokuwa akihutubia mamia ya wanachama na mashabiki wa chama hicho
akiwa katika ziara yake kuimarisha chama katika mikoa ya Shinyanga na
Kigoma.
“Chadema
ni chama makini, kina kila kitu kwenye katiba yake kuliko hata CCM,
kina itifaki, kina maadili hata mimi na Mwenyekiti Mbowe (Freeman)
imetuwekea mipaka ya utendaji… “Chama hakiwezi kumwonea mtu, kinatenda
haki na yanayotokea sasa ni msukumo wa baadhi ya vyombo vya usalama na
hayakuanza leo.”
Kauli
yake ilionekana kutoa ufafanuzi wa hatua ya Kamati Kuu ambayo ilimvua
nyadhifa zake zote aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu, Zitto Kabwe na wenzake
wawili kwa madai ya kuandaa waraka kuhamasisha mabadiliko hatua
iliyosababisha mvutano mkubwa ndani ya chama hicho kikuu cha upinzani
nchini.
No comments:
Post a Comment