Dar es Salaam. Waziri
wa Viwanda na Biashara, Dk Abdallah Kigoda amesema kuwa, Serikali
itaendelea kutengeneza mazingira mazuri ya kufanya biashara ili
wawekezaji wa nje na ndani waweze kutekeleza majukumu yao bila kikwazo.
Dk
Kigoda aliyasema hayo juzi usiku alipokuwa kwenye hafla ya kuzitambua
Kampuni 100 Bora zinazokua kwa kasi nchini (Top 100 Mid–Sized
Companies), ambapo Kampuni ya Kipipa Millers Limited ya jijini Mwanza
ilishika nafasi ya kwanza.
Kampuni
hizo zilitambuliwa na kupewa tuzo kutokana na shindano linaloendeshwa
na Kampuni ya Mwananchi Communications (MCL) na KPMG Tanzania na
kudhaminiwa na Benki ya NBC pamoja na Soko la Hisa la Dar es Salaam
(DSE).
Dk
Kigoda alisema shindano hilo linaimarika kila mwaka na lina nafasi
kubwa ya kuimarisha uchumi kwa Kampuni za Afrika Mashariki.
Alisema
ili kampuni hizo ziweze kufikia mafanikio, Serikali itajitahidi kuweka
mazingira yatakayoziwezesha kufanya shughuli zake vizuri na kufanya
uzalishaji kwa gharama nafuu.
Alizitaka
kampuni zilizofanikiwa kuingia kwenye kundi la kampuni 100 bora,
kujitambua kuwa sasa wao ni washindi na hivyo wajitahidi kufanya
shughuli zao kitaalamu zaidi.
“Kwa kiwango hiki mlichofikia sasa ni washindi, mfanye kazi zenu kitaalamu zaidi,” alisema Dk Kigoda.
Alisema
kwa sasa Tanzania imeshuka kwenye nchi zenye viwango vizuri vya kufanya
biashara duniani, hali inayofanya baadhi ya wawekezaji kukimbia.
Alieleza
suala hilo linaipa Serikali changamoto ya kutengeneza mazingira bora na
rafiki ili kuvutia wawekezaji kufanya shughuli zao kwa faida.
Kwa
upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Mwananchi Communications Limited
(MCL), Zuhura Muro alisema kwa kushirikiana na KPMG, wanaendesha
shindano hilo kwa sababu wanaelewa kuwa hiyo ni njia muhimu ya
kuhamasisha kampuni kufanya vizuri.
Alisema
kuwa, kampuni hizo ni muhimu kwa uchumi wa nchi na ustawi wake kwani
kodi wanazolipa ndizo zinazotumika kwa maendeleo ya nchi.
“Sasa
ni wakati wetu wa kuinuka, lakini hatuwezi kuinuka bila kuwa na watu
muhimu kama ninyi (kampuni 100 bora) kwani ndiyo mnaotengeneza ajira,
nyie ni watu muhimu sana kwa uchumi wa nchi hii,” alisema Muro.
Huu
ni mwaka wa tatu wa shindano hilo, mwaka 2011 Kampuni ya BQ Contractors
ya Dar es Salaam ilishika nafasi ya kwanza, huku mwaka 2012 Kampuni ya
Helvetic Solar Contractors ya jijini Arusha ikichukua nafasi hiyo.
Mara
baada ya kutangaza kuwa mshindi jana, Mkurugenzi Mkuu wa Kipipa
Millers Limited, Oliver Matemu alisema hakutarajia kushika nafasi hiyo.
“Nilipokuwa
hapo ndani nilikuwa nasikia tu wakitangaza, walipofika nafasi ya 50
bila kusikia tukiitwa nilijua kuwa sisi tumerukwa,” alisema Matemu.
Matemu
alisema kuwa, kampuni yake inajishughulisha na usagaji wa nafaka na
kuzisambaza pamoja na kusambaza bidhaa za Kiwanda cha Bia cha Tanzania
(TBL).
“Kilichotufanya tukaibuka washindi ni namna ambavyo tunajitahidi kuandaa hesabu zetu,” alisema Matemu.
Alisema
kuwa, alianza shughuli hiyo kwa kununua unga kwenye mashine za watu na
kuusambaza wakati huo akiwa na mtaji wa kati ya Sh1.5 milioni.
“Kwa sasa kwa mwaka nafanya biashara ya kama Sh5 bilioni,” alisema.
Kampuni
nyingine zilizoingia kwenye 10 bora ni Otonde Group of Companies
Tanzania Limited, iliyoshika nafasi ya pili, SEEDCO Tanzania Limited ya
tatu, Kays Logistics Company Limited ya nne, Sihebs Technologies Company
Limited ya tano na Techno Brain Tanzania Limited ya sita.
Kampuni
nyingine ni Anjari Soda Factory Limited nafasi ya saba, NPK
Technologies Limited nane, Palray limited ya tisa na Fomcom
International Limited nafasi ya 10.
No comments:
Post a Comment