Na Mohammed Mhina, wa Jeshi la Polisi –Zanzibar
ZANZIBAR
JUMATATU DESEMBA 2, 2013. Wananchi wa Shehia ya Mwanyanya nje kigogo ya
mji wa Zanzibar wakiongozwa na Kikundi cha Vijana wa Green Society cha
eneo hilo, wameshiriki katika kazi ya ukusanyaji na uzoaji wa taka
katika shehia hiyo.
Wakizungumza
mara baada ya kazi hiyo, Mwenyekiti wa Green Society Bw. Ali Abdallah
Ali na Ali Bakari Khatibu, wamesema mbali ya kikundi hicho kushiriki
katika kazi hiyo ya uzoaji taka, pia kikundi hicho kitaendelea na kazi
ya ustawishaji wa mazingira ikiwa ni pamoja na kupanda miti ya kisasa na
kuitunza ile ya uwoto wa aslai iliyopo katika eneo hilo.
Wamesema
Kikundi hicho cha Mwanyanya Green Society kitahakikisha kuwa kila
kijana na mwananchi wa eneo hilo la Mwanyanaya anashiriki kwa hali na
mali katika kazi za usafi wa mazingira na kulifanya eneo la Mwanyanaya
kuwa lenye kijani kibichi na lisilokuwa na taka.
Awali
Mkuu wa Kitengo cha Elimu ya Mazingira Zanzibar Bi. Zuwema Juma Hamadi,
ambaye alikuwa mgeni Rasmi katika shughuli hiyo, alisema kuwa ofisa
yake imeanzisha operesheni ya uzuiaji wa uchimbaji wa mchanga kiholela
ikiwa ni sehemu ya kuzuia uharibifu wa mazingira.
Vijana
hao wa Green Society, wameitumia siku hiyo kama sehemu ya uzinduzi wa
kikundi chao ambacho mbali ya kujihusisha na masuala ya ustawishaji wa
mazingira pia kinalenga katika kumkwamua kijana katika matumizi ya dawa
za kulevya na kumjengea mazingira ya kujiajiri.
Aidha
Vijana hao wametoa wito kwa wananchi katika maeneo mbalimbali ya
Zanzibar na Tanzania kwa ujumla kujitolea katika masuala ya usafi na
usawishaji wa mazingira kwani kwa kufanya hivyo kutaiwezesha nchi yetu
kuwa ya kijani kibichi.
No comments:
Post a Comment