SHIRIKA la Taifa la Hifadhi ya
Jamii (NSSF) Mkoa wa Temeke limefanya semina kwa maofisa ajira na Fedha
zaidi ya 150 kutoka katika makampuni na taasisi anuai za eneo hilo ikiwa
ni jitihada za kutoa elimu juu ya shughuli mbalimbali zinazofanywa na
taasisi hiyo.
Semina hiyo iliyofunguliwa na
Mkurugenzi wa Uendeshaji wa NSSF, Cresentius Magori imefanyika leo
jijini Dar es Salaam, ambapo washiriki mbali na kupewa elimu juu ya
mafao saba yanayotolewa na shirika hilo pia wameelezwa namna ya mfumo
mpya wa ukokotoaji mafao kwa mujibu wa sheria ya Mamlaka ya Usimamizi wa
Sekta ya Hifadhi ya Jamii (SSRA).
Akifungua semina hiyo Mkurugenzi
Uendeshaji wa NSSF, Cresentius Magori aliwataka washiriki kuitumia
vizuri elimu watakayoipata juu ya shughuli za shirika hilo ikiwemo
kuwaelimisha wafanyakazi umuhimu wa mafao mbalimbali yanayotolewa na
NSSF ili waweze kuzitumia vema fursa zilizopo katika mafao hayo.
Alisema wapo baadhi ya wafanyakazi
ambao hukimbilia kujitoa mara baada ya kuacha kazi jambo ambalo
alieleza lina athari kubwa kwao hapo baadaye kwani kitendo cha kujitoa
mara kwa mara huenda kikamkosesha sifa za kupata mafao hapo baadaye.
“Fao la kujitoa lipo…lakini hii
kitu ya kujitoa sio nzuri maana inaweza kumkosesha mwanachama kupata
penseni hapo baadae. Maana ili mwanachama apate pensheni kuna idadi ya
michango ambayo inatakiwa awe ametimiza…sasa kama ataendelea kujiunga na
kujitoa anaweza asifikishe,” alisema Magori.
Aidha alisema wapo baadhi ya
wafanyakazi wamefikia hatua ya kugushi barua kuwa wameacha kazi ili
wachukue michango yao jambo ambalo ni hatari na kinyume cha sheria,
hivyo kuwataka maofisa ajira hao kuwa makini na mchezo huo mbaya kwani
unaweza kuwaingiza matatizoni endapo watabainika kushiriki ulaghai huo.
Akizungumzia uhai wa NSSF
aliwahakikishia wanasemina hao kuwa shirika hilo lipo salama kutokana na
mafanikio na mikakati iliyonayo hivyo wasidanganyike na taarifa zozote
zisizo rasmi ambazo wakati mwingine zimekuwa zikiwaongopea wananchini.
“…Mfuko wetu upo salama na imara
hatujafilisika na hatuwezi kufilisika, maana kwa ukaguzi ambao ulifanywa
hivi karibuni unaonesha shirika liposalama kwa miaka 50 ijayo sasa
tutafilisika kwa vipi? Bado tumekuwa wa kwanza kimataifa kufanya vizuri
kiutendaji kadri ya tulivyojipangia katika utoaji huduma na huduma
zimeboreshwa,” alisema Magori.
Kwa upande wake Meneja Kiongozi wa
NSSF Mkoa wa Temeke, Yahya Mhamali alisema licha ya uboreshaji wa
huduma ndani ya shirika hilo kwa sasa mtu atakayemshawishi mteja/wateja
wapya kujiunga na mfuko huo atapata asilimia 10 ya mchango wao wa kwanza
mara baada ya kuanza kuchangia ikiwa ni kama asante kwake.
“…Hii sio rushwa maana sisi kila
siku tunazunguka kushawishi wananchi kujiunga na mfuko wetu sasa kama
wewe umetusaidia na mwanachama akaja kwetu kwanini tusikupe asante?
Maana hapa umelisaidia taifa kwa mwanachama huyu kuingia katika eneo
salama kwa maisha yake ya baadae,” alisema Mhamali.
Akitoa ufafanuzi katika mada yake
kwa wanasemina, Meneja Mafao Mkoa wa Temeke, James Oigo alisema NSSF kwa
sasa inaendelea kutoa mikopo kwa wanachama wake kupitia Saccos
mbalimbali ikiwa ni hatua ya kuwajali wanachama wake hivyo kuwashauri
wanachama kutumia fursa hiyo kujiletea maendeleo kwa kupata mikopo iliyo
na riba nafuu.
*Imeandaliwa na www.thehabari.com
No comments:
Post a Comment