TUZO
za Wanamichezo Bora wa Tanzania zinazotolewa na Chama cha Waandishi wa
Habari za Michezo Tanzania (TASWA) zinatarajiwa kufanyika Desemba 12
mwaka huu, huku Kampuni ya Said Salim Bakhresa (SSB) Group Limited
ikijitokeza kuwa mdhamini mshiriki wa tuzo hizo kwa kutoa Sh. Milioni
10.
Akizungumza
na waandishi wa habari katika mgahawa wa City Sports Lounge, Dar es
Salaam katika hafla ya kutangaza udhamini huo jana, Meneja Mkuu wa SSB
Limited, Said Muhammad Said alisema wameamua kudhamini tuzo hizo kama
hatua mojawapo ya kuinua michezo nchini.
Aliupongeza
uongozi wa TASWA kwa juhudi kubwa inazofanya katika kuhamasisha michezo
na kwamba wameona waunge mkono juhudi hizo kwa kutoa fedha hizo.
Kwa
upande wake Mwenyekiti wa TASWA, Juma Pinto alisema kampuni mbalimbali
zimeonesha nia ya kudhamini tuzo hizo na watakuwa wanazitangaza kadri
watakavyomalizana nazo.
“Tunaishuku
sana Bakhressa kwa mchango huu mkubwa kwetu, pia tunaomba wadau
tushirikiane kwa kila hali kuhakikisha tuzo zetu zinafanikiwa na
tunaomba kampuni zaidi zijitokeze.
“Bajeti
ya tuzo zetu ni Sh milioni 120, zipo kampuni zimeonesha nia ya
kutusaidia, mwishoni mwa wiki hii au mwanzoni mwa wiki ijayo tutatangaza
wadhamini wengine,” alisema Pinto.
Kwa
upande wake Katibu Mkuu wa TASWA, Amir Mhando alisema Kamati Maalum ya
Tuzo hizo inaendelea na mchakato wake wa kupata wanamichezo hao na
kwamba kadri watakavyokuwa wanapiga hatua watatoa taarifa kwa
wanahabari.
Alisema
maandalizi mengine yanaenda vizuri na wanaamini zitakuwa tuzo bora
kuliko zote zilizowahi kufanywa na chama hicho katika miaka ya hivi
karibuni.
Kwa
miaka mitano iliyopita walioshinda Tuzo ya Mwanamichezo Bora wa TASWA
walikuwa ni Samson Ramadhani (2006), Martin Sulle (2007), Mary Naali
(2008), ambao wote ni wanariadha, wakati 2009 na 2010 alikuwa mcheza
netiboli Mwanaidi Hassan na mwaka 2011 alikuwa beki Shomari Kapombe
ambaye sherehe za kumkabidhi tuzo zilifanyika Juni mwaka 2012. Mwaka
jana tuzo hizo hazikufanyika.
Wakati
huohuo, Mhando alisema chama chake kinaendelea na mazungumzo na
wadhamini mbalimbali kuhusiana na tamasha kwa ajili ya vyombo vya habari
‘Media Day Bonanza’ na kwamba mapema mwezi ujao suala hilo litakuwa
limemalizika.
No comments:
Post a Comment