24/9/2014 Ukosefu wa uelewa na
imani potofu miongoni mwa wanajamii ni moja ya chanzo cha unyanyapaa kwa
watoto wenye tatizo la usonji (Autism) .
Hayo yamesemwa jana na Mke wa Rais
Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete Mama Salma Kikwete wakati akiongea na Prof.
Andy Shih ambaye ni Makamu wa Rais mwandamizi wa Mambo ya kisayansi
kutoka Taasisi ya Kimataifa ya Autism Speaks yenye makao yake mjini New
York.
Mama Kikwete ambaye pia ni
Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) alisema jamii bado
haina uelewa kuhusu tatizo la usonji kwani kuna baadhi ya watu
wanahusisha tatizo hilo na mambo ya ushirikina lakini kama jamii itakuwa
na uelewa tatizo la unyanyapaa litapungua au kwisha kabisa.
Alisema usonji bado ni tatizo
nchini Tanzania na nchi zingine lakini wazazi wengi wanaona aibu kusema
hadharani wana watoto wenye matatizo hayo na hivyo kuwa vigumu kwa
watoto hao kupata huduma muhimu ikiwemo elimu.
“Tunatakiwa kufanya kazi kwa
pamoja na wataalamu waliobobea katika taaluma hii ili kuhakikisha jamii
inakuwa na uelewa kuhusu tatizo hilo kwa kufanya hivyo watoto hawa
watapata huduma za muhimu kama elimu na afya”, alisema Mama Kikwete.
Kwa upande wake Prof. Shih alisema
Taasisi yake iko tayari kufanya kazi na WAMA ili kuwasaidia watoto
wenye tatizo la usonji ili waweze kupata elimu na huduma ya afya kama
watoto wengine.
Prof. Shih alisema tatizo la
unyanyapaa bado ni kubwa kwa watoto lakini kama jamii itapata elimu na
kulifahamu tatizo hilo itaweza kuwasaidia watu wenye matatizo hayo na
hivyo kupunguza tatizo la unyanyapaa.
Usonji ni hali ya udhaifu katika
ukuaji wa ubongo ambayo huleta athari kubwa katika mawasiliano,
mahusiano ya kijamii na utambuzi.Tatizo hili ni la dunia nzima na bado
hakuna maelekezo kamili ya chanzo chake wala tiba.
Wanaoathirika zaidi ni watoto wa
kiume kuliko wa kike kwa uwiano wa nne kwa moja hii ikiwa na maana kuwa
kila watoto watano wenye usonji wanne ni wa kiume na mmoja wa kike.
Mwaka 1997 wizara ya Elimu na
Utamaduni ikishirikiana na wanachama wa National Association for People
with Autism in Tanzania (NAP-T) walianzisha kitengo cha watoto wenye
usonji katika shule ya msingi Msimbazi Mseto ambacho ni kitengo mama cha
kutoa huduma.
Hivi sasa Serikali inavitengo
vitano, viwili vipo Dar es Salaam, viwili Arusha na kimoja Morogoro. Pia
kuna vitengo kadhaa vilivyoendeshwa na watu binafsi.
No comments:
Post a Comment